Utitiri vyama hewa ushirika uwe fundisho

07Jan 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Utitiri vyama hewa ushirika uwe fundisho

KUNA taarifa kwamba serikali inakusudia kuvifuta vyama hewa vya ushirika 3,436, kutokana na kubainika kuwa vimekosa sifa ya kuendelea kuwapo.

Serikali imesema kuwa itavifuta kwa mujibu wa sheria ya ushirika baada ya kuvifanyia uchuguzi na kubaini kuwa havipo katika maeneo ambayo vinaonyesha vilisajiliwa wala viongozi wake hawajulikani.

Mpango huo ulitangazwa na Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Jumapili jijini Dodoma.

Hasunga alisema mpaka sasa daftari la mrajisi wa vyama vya ushirika nchini lina jumla ya vyama 11,149, vilivyoandikishwa, na kwamba kati ya hivyo 3,436 havijulikani vilipo na vyama 1,250 vimesinzia na vyama 6,463 vipo hai.

Kwa mujibu wa waziri huyo, kutokana na kuwapo kwa vyama hewa katika daftari la mrajisi wa vyama vya ushirika, aliagiza kutangaza kwenye gazeti serikali kusudio la kuvifuta vyama hivyo kwa mujibu wa sheria ya vyama vya ushirika kifungu 100, ambacho kinaeleza kuwa chama kinaweza kufutwa kwa sababu mbalimbali.

Kufuta vyama vya ushirika ni hatua ya kusikitisha, lakini ni uamuzi wa maana kwa kuwa bila kufanya hivyo, hawatanufaika kwa njia yoyote.

Ikumbukwe kuwa lengo kuu la kuanzishwa kwa vyama vya ushirika, lilikuwa ni kuwawezesha wakulima, hivyo kama inafika mahali baadhi vikatoka katika msingi huo, hakuna sababu ya kuvifumbia macho.

Umuhimu wa vyama vya ushirika ulibainika baada ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, kuvifuta kutokana na kasoro kadhaa, lakini baada ya kuona kuwa uamuzi huo uliwaathiri walengwa, serikali yake iliamua kivirejesha.

Kwa hiyo tunaunga mkono kusudio la serikali la kuvifuta vyama vya ushirika hewa, ambavyo malengo yake hayajulikani, ili kuepusha kutumika vibaya kimyume cha malengo ya ushirika nchini.

Hatutarajii kuwa kutakuwapo na lawama kuhusiana na hatua hiyo kwa kuwa sababu ambazo zinaweza kusababisha chama cha ushirika kufutwa ni kutokuwa na ofisi tangu kuandikishwa, hakijulikani kilipo na viongozi wake hawafahamiki na hawapatikani.

Sababu nyingine ni kushindwa kutekeleza takwa la kisheria la kutayarisha makisio ya mapato na matumizi na kuyapeleka kwa marajis kuyapitia, kutayarisha taarifa ya mwaka, kufunga mahesabu na kuyapeleka COASCO, kwa ukaguzi na kutofanya mikutano ya mwaka ya wanachama wote na bodi zao.

Hata hivyo, tunaona kuna umuhimu kwa mamlaka zenye dhamana ya kusimamia ushirika kuwa na utaratibu wa kuratibu na kufuatilia vyama vya ushirika kila wakati, kwa lengo la kuhakikisha kuwa vinatekeleza matakwa ya kisheria.

Kwa kufanya hivyo, hakutakuwapo na uwezekano wa kuibuka kwa vyama hewa kama ilivyotokea hadi ukafikia utitiri wa vyama 3,436.

Hali hii iliachwa hivi inaweza kusababisha vyama hewa vya mifukoni kama hivi kutumia ujanja kufanya utapeki kwa kutumia mwavuli wa ushirika nchini.

Bila shaka maagizo ya Waziri Hasunga kwa mrajisi wa vyama vya ushirika nchini ya kuzingatia sheria No. 6 ya mwaka 2013 ya vyama vya ushirika kifungu 100 na kanuni ya 26, ambayo inamtaka mrajisi anatakiwa kutoa notisi ya kusudio la kutaka kufuta vyama vya ushirika kwenye gazeti la serikali kwa muda wa siku 90.

Habari Kubwa