Utoaji vyeti vya kuzaliwa kwa watoto uchangamkiwe

10Jan 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Utoaji vyeti vya kuzaliwa kwa watoto uchangamkiwe

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo, ameingilia kati sakata la wazazi na walezi wanaoandikisha watoto kwa ajili ya kuanza darasa la kwanza, kwa kulazimishwa kuwa na vyeti vya kuzaliwa.

Wakuu wa shule katika maeneo yote nchini tangu Jumatatu shule zilipofunguliwa, wamekuwa wakiwataka wazazi na walezi wanaokwenda kuandikisha watoto wa darasa la kwanza kutimiza takwa la kisheria la kuwa na vyeti hivyo, ambavyo hutolewa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita).

Hata hivyo, wazazi wengi na walezi hususan maeneo ya vijijini wameshindwa kutimiza sharti hilo, kutokana na kutokuwa na vyeti hivyo, na kulalamika baada ya kukataliwa kuwaandikisha watoto.

Kutokana na hali hiyo, Waziri Jafo juzi aliingilia kati kwa kutangaza kuwa ni marufuku mwanafunzi kuzuiliwa kuandikishwa darasa la kwanza, kwa sababu ya kukosa cheti cha kuzaliwa.

Jafo alitangaza mafuruku hiyo wakati wa ziara yake wilayani Bahi Mkoa wa Dodoma kukagua uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la kwanza kwa shule za msingi pamoja na mapokezi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule za sekondari.

Alieleza kuwa amepokea malalamiko kutoka baadhi ya maeneo nchini kwamba wanafunzi wa darasa la kwanza hawaandikishi kama hawana vyeti vya kuzaliwa.

Waziri huyo alifafanua kuwa cheti cha kuzaliwa ni haki ya kila mtoto, lakini isimzuie mtoto huyo kuanza shule eti kwa sababu tu hajapata cheti hicho, na kuagiza kuwa watoto wote wapokelewe, waandikishwe na waanze masomo wakati wazazi wao wakiendelea na mchakato wa kuwatafutia vyeti hivyo.

Alisema hataki kusikia eneo lolote mtoto ameachwa kupokelewa na kuanza shule kwa sababu ya kukosa cheti cha kuzaliwa, hivyo mzazi ahakikishe ndani ya miezi minne amepata cheti hicho, lakini mtoto huyo aanze masomo wakati masuala ya cheti yanaendea kushughulikiwa kwenye mamlaka husika.

Uamuzi wa Jafo ni wa kupongeza, kutokana na hataruki iliyoibuka katika maeneo mengi nchini kutokana na vyeti vya kuzaliwa kukwaza mchakato wa kuwaandikisha wanafunzi wa darasa la kwanza.

Huo ndio uwajibikaji kwa viongozi wa umma; kwamba pale linapotokea tatizo kubwa la msingi kama hilo linaloathiri wananchi, anachukua hatua haraka za kulitatua.

Ni ukweli kuwa vyeti vya kuzaliwa kwa wananchi kadhaa hususan wa vijijini bado ni changamoto, hivyo ipo haja kwa mamlaka husika hususan Rita kuangalia utaratibu mzuri zaidi wa kuvitoa hususan katika maeneo ya vijijini, ambako kinamama wanajifungulia majumbani.

Katika mazingira kama haya, inakuwa vigumu watoto kuwa na vyeti vya kuzaliwa, hivyo tunaishauri jamii kujenga utamaduni wa kufuatilia vyeti vya kuzaliwa kwa watoto baada ya kuzaliwa kwa kuwa kwa sasa ni nyaraka muhimu.

Ikumbukwe kuwa cheti cha kuzaliwa ni miongoni mwa nyaraka zinazotakiwa wakati wa kuanza elimu ya msingi, sekondari, kujiunga na vyuo, kupata pasi za kusafiria na huduma nyinginezo.

Kwa siku za karibuni, Rita imekuwa na utaratibu mzuri na endelevu wa kutoa vyeti vya kuzaliwa katika maeneo mbalimbali kama maonyesho ya Sabasaba, Nanenane na shughuli nyingine, hivyo wananchi tuichangamkie ili kila mmoja awe na cheti cha kuzaliwa hususan watoto.

Kwa kufanya hivi, changamoto zinazojitokeza kila mara ikiwamo ya uandikishaji wanafunzi zitakuwa historia.

Habari Kubwa