Utolewe mwongozo kuelimisha watoa huduma za fedha

16Oct 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Utolewe mwongozo kuelimisha watoa huduma za fedha

HIVI karibuni Benki Kuu ya Tanzania (BoT), iliongeza miezi sita ya maombi ya leseni na usajili kwa watoa huduma za fedha ikiwamo vikundi vya kifedha vya kijamii (VICOBA), SACCOS na vikundi vinginevyo.

Muda uliotolewa tangu Novemba mwaka jana unaisha Oktoba 31, mwaka huu, na kwa mujibu wa Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2018, yeyote atakayekutwa anatoa huduma hiyo bila leseni atachukuliwa hatua za kisheria.

Kabla ya nyongeza ya muda huo utakaokwisha Aprili 30, 2021, vikundi mbalimbali ambavyo vingi ni vya wanawake vilikuwa katika taharuki kubwa ya namna ya kukimbizana na muda uliosalia ili kujisajili, lakini vilikosa taarifa.

Aidha, vikundi vingi vilijikuta katika wakati mgumu kwa kuwa kila walipokwenda halmashauri au manispaa kwa Maofisa Maendeleo Jamii, waliambiwa wajisajili na kulipa ada ya Sh. 50,000 wakati wanasubiri mwongozo wa BoT na namna watakavyopata leseni ya kuendesha vikundi vyao.

Vikundi hivi ni vya watu walioungana kwa lengo la kupambana na umaskini, yaani kupitia katiba zao wameweka makubaliano ya namna watakavyoweka mtaji au hisa anzia.

Pia, vikundi hivyo vina taratibu tofauti ikiwamo kuvunja vibubu kila baada ya miezi 12 kwa kuchukua fedha zote na kuanza mzunguko upya na wengine huchukua hisa, lakini fedha ya mtaji hubaki kwa ajili ya kurahisisha utoaji wa mikopo.

Vikundi hivyo hutoa mikopo kwa wanachama kulingana na viwango walivyokubaliana, riba na muda wa kurejesha na fedha zote haziruhusiwi kuvuka mwaka, huku wengine wakienda mbali zaidi kutoa mikopo ya maendeleo kuwawezesha wanachama wasio na vyombo vya usafiri kuvimiliki, au wasio na nyumba kuanza ujenzi.

Pia, hutoa mikopo kwa ajili ya kuanzisha biashara, na lengo kubwa ni kuwawezesha kujikwamua kwa kutumia fedha za wanachama ambazo huzunguka kutoka kwa mmoja hadi mwingine.

Hakuna ubishi vikundi hivi ni mkombozi kwa wanawake wengi kwa kuwa ndiko walikopata mtaji wa kuanzisha biashara, kumiliki vyombo vya usafiri, nyumba, kusomesha watoto katika shule nzuri, matibabu na kulipa kodi za nyumba.

Wanawake kupitia uwekezaji huo wamejipatia mitaji na kuondokana na adha ya kukopa benki ambako riba si rafiki na hakuna cha kuweka rehani ili kupata fedha hizo.

Katika jitihada hizo zilijitokeza changamoto kama za baadhi ya wanachama kukimbia na fedha za wenzao kiasi cha kupelekana polisi, na ndipo serikali ikaja na utaratibu ikiwamo kuwa na sheria ya kuhudumia vikundi hivi.

Lengo ni zuri, lakini bado wanachama wa vikundi hivi wamejikuta katika taharuki kiasi cha wengine kufikiria kuvunja kabisa, kwa kuwa hadi sasa haiko wazi kiasi cha kodi ambacho kitatozwa katika fedha za wanachama walizokusanya na kukopeshana.

Na bahati mbaya baadhi ya Maofisa Maendeleo ya Jamii wameshindwa kuelimisha wanavikundi, zaidi ya kuwataka kulipa fedha na kuweka viambatisho, huku kukiwa na maswali baada ya hapo nini kinafuata? Je, ndiyo kikundi kimesajiliwa? Watapata wapi leseni?

Kabla ya mwogozo huo wapo waliokwenda mbali zaidi kwa kuamua kugawana fedha zao, ili kubaki salama kabla ya kukatwa au vinginevyo, lakini yote hiyo ni kukosekana kwa taarifa ngazi za halmashauri wanakokwenda kujisajili.

Tunasema muda ulioongezwa utumike vizuri kwa vikundi kufuata utaratibu wa kujisajili, lakini ni vyema BoT ikaweka wazi mwongozo na kodi zitakazotozwa kwenye vikundi hivi.

Taarifa zilizopo halmashauri bado hazijitoshelezi na vikundi vingi ambavyo vinatoa huduma za kijamii vinakwenda ngazi hiyo kupata uelewa wa kina kwa ajili ya kuwafikishia wanachama wao.

Ikiwa wanachama wataona na kusoma mwongozo husika maana yake hakutakuwa na taharuki wala maswali mengi yasiyo na majibu hasa katika usalama wa fedha zao ambazo zinahifadhiwa katika benki mbalimbali.

Habari Kubwa