Utulivu, umakini muhimu kuelekea lala salama Bara

10Apr 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Utulivu, umakini muhimu kuelekea lala salama Bara

ZIKIWA zimebakia raundi tisa ili kumalizika kwa msimu wa mwaka 2020/21 wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo inashirikisha timu 18 za hapa nchini, mambo mbalimbali ya kuzingatia yanahitajika ili kuhakikisha msimu husika unamalizika vizuri.

Ligi Kuu Bara ndio ligi ya juu kwa upande wa Tanzania Bara ambayo hutoa mwakilishi wa mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika, wakati bingwa wa michuano ya Kombe la Shirikisho hupata nafasi ya kwenda kupeperusha bendera ya nchi katika Kombe la Shirikisho Afrika.

Kuelekea hatua ya lala salama, klabu zinatakiwa kutumia muda wake mwingi katika kuimarisha vikosi vyake kwa lengo la kusaka matokeo chanya wanaposhuka dimbani na si kufanya mambo mengine ambayo yanaweza kuwapoteza.

Inafahamika wapi timu iliyoandaliwa vyema au wachezaji waliopitia misingi inayostahili ndio wenye nafasi ya kuzalisha matokeo chanya na si jambo lingine lolote nje ya hapo.

Nipashe inazikumbusha timu zote zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara kuhakikisha zinaendelea kuchanga vyema karata zake na hatimaye kufikia malengo waliyojiwekea kwa sababu muda wa kujiimarisha bado upo.

Mechi tisa kwa timu ambazo hazina viporo zinaweza kubadilisha nafasi uliopo katika msimamo na hatimaye kumaliza msimu kwa kicheko kwa timu ambayo itafanikiwa kutwaa ubingwa lakini pia kwa wale ambao watanusurika na janga la kushuka daraja ambalo hakuna timu inayopenda kulishuhudia.

Kama nafasi ya kutwaa ubingwa bado iko wazi, ni vyema kwa klabu zote kuendelea kupambana kuhakikisha wanaondoka na ushindi wanapoingia uwanjani kwa sababu huwezi kujua Mungu amewaandalia zawadi gani kutokana na jitihada walizozionyesha wakati wote wa msimu.

Vile vile katika upande wa timu zinazoburuza mkia, kwa idadi ya mechi zilizosalia hakuna klabu ambaye imejihakikishia kujinasua kwenye janga hilo kwa sababu katika soka lolote linaweza kutokea na 'bundi' akahamia kwenye klabu yako.

Tunawakumbusha huu si wakati wa kupoteza katika kuendesha michakato ya nje ya uwanja kwa sababu haitasaidia timu kuvuna pointi za uwanjani na matokeo yake mtawakosesha mashabiki wetu furaha ya kushuhudia michezo ya Ligi Kuu pale timu hizo zinapokuwa kwenye viwanja vya nyumbani.

Vita ya kushuka daraja inawezekana ikaonekana ni vita nyepesi, lakini vile vile ni vita yenye ushindani mkubwa kwa sababu timu zilizoko mkiani zinatofautiana kwa pointi chache hivyo kikosi kinachofanikiwa kupata ushindi wa mechi moja, mbili au sare, hupaa kwa nafasi zaidi ya moja na kurejesha matumaini ya kusalia kwa ajili ya msimu ujao.

Ingawa tunawakumbusha ni makosa kukata tamaa kabla ya filimbi ya mwisho ya halijapulizwa, lakini dalili za 'kuzama' au kuibuka mfalme wa msimu huanza kuonekana wakati hatua ya lala salama ikianza kukaribia.

Hata hivyo baadhi ya timu zinatakiwa zibadilishe mwenendo wake kwa sababu kila msimu zinaonekana kutoonyesha ushindani wowote wa kuwania ubingwa na badala yake wamekuwa wasindikizaji kwa kuridhika pale wanapobaini wako kwenye nafasi salama.

Mbali na Ligi Kuu Tanzania Bara, bado kuna nafasi ya kujirekebisha kwa timu ambazo zimesalia katika mashindano ya Kombe la FA ambayo bingwa wake naye hukata tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Kupanga ni kuchagua, timu inayohakikisha inaendelea kupanga vyema hesabu za kusaka ushindi uwanjani zitafanikiwa na wale ambao watatumia muda wao katika masuala ya 'porojo', watajichimbia kaburi wenyewe.

Nidhamu na utulivu ndio silaha muhimu inayohitajika katika kipindi hiki ili kila timu itimize malengo chanya iliyojiwekea na hatimaye kuanza maandalizi ya msimu mpya kwa weledi.