Uvamizi wa Makonda haukubaliki kamwe

21Mar 2017
Mhariri
Nipashe
Uvamizi wa Makonda haukubaliki kamwe

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, akiwa na askari wenye bunduki alivamia ofisi za kampuni ya habari ya Clouds Media Jumamosi iliyopita hivyo kuibua hofu kubwa kwa wafanyakazi wa kituo chake cha televisheni waliokuwa kazini.

Mengi yamesemwa na uongozi wa Clouds Media ambayo kwa ujumla yanaonyesha dhahiri kuwa kitendo hicho hakikuwa cha kawaida na kilichowashtua mno hasa kwa kuwa uvamizi huo umefanywa na kiongozi wa juu mkoani.

Mkuu wa Mkoa, tunasema Nipashe, ni wadhifa wa mtu ambaye anapaswa kufahamu sheria na taratibu za kuwasilisha malalamiko dhidi ya chombo chochote cha habari nchini kama anayo.

Hivyo tuchukue fursa hii, Nipashe, kwanza kuwapa pole wenzetu wa kampuni ya Clouds Media kwa taharuki iliyowakuta kiasi cha baadhi ya wafanyakazi wake waliopatwa na kadhia hiyo kuugua shinikizo la damu.

Tunawatakia kila la kheri wafanyakazi walioathirika kiafya na kisaikolojia ili warejee kwenye hali zao za kawaida na hatimaye kuendelea na kazi adhimu ya kuhabarisha umma.

Lakini tuchukue fursa hii pia, Nipashe, kueleza tunalichukulia tukio hili kama uhalifu kwa kuwa ni uvunjaji wa sheria kwa maana ya matumizi mabaya ya madaraka.

Aidha, tunaona kitendo cha Makonda kuwa ni uhalifu kwa kuwa ameingia sehemu isiyoruhusiwa bila ridhaa ya muhusika, tena kwa vitisho ili kupata ambacho siyo stahili yake.

Kwa kuwa hizi ni tuhuma za ukiukaji wa hali ya juu wa maadili ya ungozi ambazo ziko mbele ya Makonda kwa sasa, tunaamini, Nipashe, tayari zimeivunjia serikali heshima na kudhalilisha mamlaka ya utawala mbele ya wananchi wake.

Bahati mbaya zaidi, Makonda amevamia kituo cha habari wakati serikali ikiwa imetoka kukamilisha utungwaji wa Sheria ya Upatikanaji Habari kwa lengo la kuiwezesha tasnia hiyo kufanya kazi kwa weledi zaidi na si chini ya vitisho vya mamlaka ya utawala.

Tunapongeza lengo zuri la serikali la kuboresha sheria zinazosimamia utendaji wa vyombo vya habari, ili pamoja na mambo mengine viweze kutimiza wajibu wake ipasavyo kwa nia ya kuwawezesha wananchi wazifikie taarifa mbalimbali kwa ajili ya kujikwamua kimaendeleo.

Tumesikia Waziri mwenye dhamana na masuala ya habari, Nape Nnauye, ameunda timu ya watu watano kufanya uchunguzi wa kina ili kujua kwa yakini ni nini hasa kilitokea ili kupata ripoti itakayoisaidia serikali kuchukua maamuzi stahiki juu ya kadhia hii.

Pamoja na kusubiri kwa shauku kubwa matokeo ya uchunguzi huo ili kuona hatua zitakazochukuliwa na serikali, tungependa kuchukua fursa hii kulaani kwa nguvu zetu zote tukio hili ambalo kwetu tafsiri yake ni moja tu - kuingiliwa kwa uhuru wa vyombo vya habari.

Ni dhahiri wanahabari wanapokuwa kazini hawatumii silaha yoyote ya moto. Silaha pekee za wanahabari ni kalamu na kamera zao.

Hata katika uwanja wa vita, kwenye maeneo yenye mgogoro na mapigano wanahabari hujipambanua kwa kuvaa mabango makubwa yenye maandishi 'PRESS' ili kujiweka mbali na pande zinazovutana. Kwamba wao siyo wapiganaji, ila ni wakusanya habari na kuziwasilisha kwa umma.

Hivyo kwa kiongozi yeyote kushindwa kuelewa hilo kiasi cha kukusanya askari wenye silaha usiku wa saa tano, kuvamia kituo cha habari, kisha kulazimisha kuingia ndani na kwenda kuwatisha wafanyakazi kwa mitutu ya bunduki, Nipashe tunasema, ni kitendo kinachoibua maswali magumu sana juu ya uelewa wa kiongozi huyo.

Uvamizi wa Makonda haukubaliki kamwe, Nipashe tunasema.

Habari Kubwa