Uwajibishwaji huu kwa ulevi ni somo kwa wote

22May 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Uwajibishwaji huu kwa ulevi ni somo kwa wote

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli aliendeleza kasi yake ya kudhihirisha uwajibikaji wa vitenbdo miongoni mwa viongozi wa serikali kwa kumfuta kazi aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga.

Katika taarifa iliyotolewa na Ikulu na kisha kukaririwa na vyombo vya habari jana, ilielezwa kuwa Rais alichukua uamuzi huo baada ya kubainika kuwa Waziri Kitwanga aliingia bungeni jana na kujibu maswali ya wizara aliyokuwa akiiongoza huku akiwa amelewa.

Uamuzi huo wa Rais umeibua mjadala mpana, huku wengi wakiwa bado kama hawaamini kutokana na kile kilichotokea. Ni kwa sababu uamuzi huo wa kumfuta kazi waziri kwa sababu ya ulevi ni mzito na haujazoeleka sana.

Kwa baadhi ya watu, imani iliyopo ni kwamba wakubwa, kwa maana ya viongozi kama mawaziri hawawezi kamwe kuchukuliwa hatua kali za kiwango cha kufutwa kazi kwa sababu ya kulewa kazini. Kwamba, miongoni mwa wakubwa huwa kuna kulindana.

Hivyo, uamuzi wa Rais kumfuta kazi waziri kwa ulevi ni jambo jipya kulisikia.

Aidha, sisi tunaamini kuwa uamuzi huo haukuwa rahisi. Ni miongoni mwa yale yaitwayo kuwa ni ‘maamuzi magumu’ kwa sababu haikutarajiwa hapo kabla kusikia kuwa waziri fulani nchini akiondoshwa katika nafasi yake kutokana na kosa la kulewa akiwa kazini.

Kadri tunavyoamini, uamuzi huo wa Rais ulikuwa na dhamira moja kubwa. Nayo ni kufikisha ujumbe kuwa Serikali ya awamu ya tano haina mzaha linapokuja suala la nidhamu kwenye mahala pa kazi.

Hakuna atakayelindwa kwa kutozingatia nidhamu na uwajibikaji. Na jambo hilo hupaswa kuzingatiwa kwa vitendo na siyo kwa ngonjera na maneno yenye wingi wa nahau.

Ni kwa sababu hiyo, Nipashe tunaona kwamba zipo sababu zaidi ya dazeni moja kwa kila Mtanzania kujifunza kuhusiana na tukio hili. Kwamba, miiko ya kazi iheshimiwe mahala popote pale.

Na yeyote anayekiuka anapaswa kumulikwa pasi na kujali nafasi yake. Bila shaka yoyote, kushindwa kuzingatia nidhamu katika mahala pa kazi kumechangia kwa kiasi kikubwa kuwapo kwa uamuzi wa kutengua nafasi ya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

Kadri tunavyofahamu, ni mwiko kwa kiongozi wa ngazi ya uwaziri kulewa akiwa kazini.

Ni jambo lisilokubalika hata kidogo kwa mkulima au mfanyabiashara kuwa katika mahala pake pa kazi akiwa amelewa. Vivyo hivyo, haistahili pia dereva, mwanafunzi na hata viongozi wa taasisi binafsi kuwa wamelewa wakiwa kazini.

Ni mwiko kwa sababu kufanya hivyo ni utovu mkubwa wa nidhamu na pia ni hatari katika kufikia ufanisi wa kile kinachokusudiwa. Kujibu maswali kwa niaba ya serikali bungeni huku mhusika akiwa amelewa ni kosa kubwa la utovu wa nidhamu.

Kwa kuzingatia yote hayo, ndipo sisi tunapoona kwamba tukio hili la kuondolewa waziri kwa sababu ya ulevi halipaswi kuachwa hivihivi.

Bali, kila mmoja anapaswa kulichukulia kuwa ni somo kwake katika kuzingatia nidhamu mahala pa kazi. Ujumbe huu utokanao na uamuzi wa Rais Magufuli katika kusimamia misingi ya nidhamu unapaswa kuwafikia viongozi wengine wote katika taasisi za umma na binafsi. Uwafikie pia wakulima na wafanyabiashara.

Ni somo linalopaswa kuzingatiwa na kila mmoja miongoni mwa Watanzania. Na wala siyo jambo la kujadiliwa juujuu kwa kumuangalia waziri aliyewajibishwa.

Kwa kuzingatia yote hayo, kwa maana ya kila mmoja kuzingatia nidhamu ya kazi yake, Nipashe tunaamini kuwa haitachukua muda mrefu kabla taifa halijafika kule linakopaswa kuwa kimaendeleo. Kila mmoja azingatie. Hongera Rais kwa kuonyesha namna sahihi ya uwajibikaji kwa kila mmoja.

Habari Kubwa