Uwazi ulitakiwa suala la vyeti kidato cha sita

24Feb 2016
Mhariri
Dar
Nipashe
Uwazi ulitakiwa suala la vyeti kidato cha sita

JANA tulichapisha habari iliyoeleza kuwa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), limeagiza kusitishwa kwa ugawaji wa vyeti vya kidato cha sita kwa wanafunzi waliohitimu mwaka 2015, huku vile vilivyokwisha gawanywa kwa watahiniwa hao vikitakiwa kurejeshwa kwenye chombo hicho.

Hatua hiyo haijawahi kuchukuliwa nchini, hivyo kuwashangaza baadhi ya wadau na kuhisi kuwa pengine kuna maamuzi makubwa yatafanywa na serikali.

Inawezekana wadau hao wakiwamo wazazi, umma na maofisa elimu wameshangazwa na kuingiwa na wasiwasi kufuatia maamuzi hayo ya Necta kufanyika ghafla na bila kuwapo uwazi kutokana an kutotolewa taarifa kwa umma hadi hivi sasa.

Baadhi ya wadau wanahisi kuwa hatua hiyo huenda inalenga kuvibadili vyeti hivyo kutoka kwenye mfumo wa wastani wa alama (GPA), kwenda kwenye mfumo wa jumla (divisheni).

Maofisa elimu wa mikoa na wakuu wa shule kadhaa walithibitisha kupewa maelekezo ya kurejesha vyeti hivyo Necta na kusitisha kuvitoa kwa watahiniwa. Aidha, kuna wazazi ambao wamesema kuwa wameshapewa maelekezo na shule walizosoma watoto wao kurejesha vyeti hivyo, wakiwamo walioko katika masomo ya elimu ya juu ughaibuni.

Licha ya hisia za wadau, Necta kupitia kwa Katibu Mtendaji wake, Dk, Charles Msonde, alizikanusha na kueleza kuwa vyeti hivyo havitabadilishwa kutoka kwenye mfumo wake isipokuwa vimesitishwa kugawanywa ili baraza lijiridhishe na baadhi ya vitu.
Uamuzi huo wa Necta kwa namna moja au nyingine umeonekana kusababisha usumbufu kwa baadhi ya watahiniwa wa mwaka huo na unaweza kuwaathiri.

Tunasema hivyo kwa kuwa baadhi ya wazazi wamelalamika kuwa wanalazimika kuwasiliana na watoto wao waliotumia vyeti hivyo kudahiliwa katika vyuo vikuu nje ya nchi ili wavirejeshe baada ya kutakiwa na virejeshwe Necta.

Ikiwa vyeti hivyo vitafanyiwa mabadiliko ya kuondolewa katika mfumo wa GPA na kuingizwa katika mfumo wa divisheni, bila shaka baadhi yao wanaweza kujikuta wakikosa sifa katika vyuo wanavyosoma kwa sasa, hivyo kuwaingiza katika usumbufu kwani kuna uwezekano wa kufutiwa udahili wakati wameshatumia fedha nyingi kugharimia masomo yao.

Inawezekana Necta imechukua hatua hiyo kwa nia njema kabisa, lakini kasoro inayoonekana na kusababisha hofu na hisia ni kutokuwa wazi kwa wadau wake na umma kwa ujumla.

Kama baraza lingetoa taarifa kwa umma kuelezea uamuzi huo na sababu zake, pasingekuwapo na hofu, wasiwasi au hisia kwa kuwa lengo lake lingeeleweka kuliko kufanya kimya kimya.

Ingawa Necta inaeleza kuwa haijaagiza vyeti virudishwe ili vibadilishwe mfumo, isipokuwa kilichofanyika ni utaratibu wake wa kawaida wa kuangalia uhalali wa vyeti vyake na kujiridhisha kama vyeti hivyo vimetawanyika sawasawa, lakini bado utoaji wa taarifa kwa wadau na umma lilikuwa jambo muhimu.

Cheti cha taaluma kina umuhimu mkubwa kwa kila mtu kwa sababu kinagusa maisha yake. Bila kuwa na cheti hicho ni vugumu kupata fursa ya ajira pamoja na ya masomo zaidi. Kutokana na unyeti huo, kila mtu anawajibika kukitunza kama moja ya mali zake muhimu katika maisha yake.

Tunashauri kwamba mamlaka zetu zinapofanya maamuzi ya ghafla yanayogusa maisha ya watu, ni vizuri zikaweka uwazi kwa kutoa taarifa kwa umma, badala ya kushtukiza na kuzua malalamiko, hofu na hisia miongoni katika jamii.

Habari Kubwa