Vijana wachangamkie ajira mpya jeshini

24Sep 2017
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe Jumapili
Vijana wachangamkie ajira mpya jeshini

RAIS John Magufuli, jana alitangaza kuwa serikali iko katika hatua za mwisho kuajiri askari wapya 3,000 katika Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ikiwa hatua ya kuimarisha taasisi nyeti katika ulinzi na usalama wa taifa.

Akihutubia taifa kupitia hafla ya kuwatunuku kamisheni maofisa wapya 422 waliohitimu mafunzo ya uofisa wa jeshi katika chuo cha Uongozi wa Kijeshi (TMA) Monduli mkoani Arusha, Rais Magufuli alisema lengo la ajira hizo ni kufanya jeshi kuwa na nguvu kazi imara katika kutumiza wajibu wake wa kulinda mipaka ya nchi.

Katika sherehe hizo zilizofanyika kwa mara ya kwanza kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid, Rais Magufuli ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, alisema kipaumbele katika ajira hizo ni vijana waliomaliza mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) hivi karibuni. Mara nyingi sherehe za kuwatunuku maofisa hao hufanyikia Monduli na mara moja zilifanyika ikulu, Dar es Salaam.

Bila kuuma maneno, Rais alisema vijana hao waliomaliza mafunzo yao katika kambi mbalimbali nchini baada ya kumaliza elimu ya kidato cha sita na baadhi yao wakitarajiwa kuendelea na elimu ya juu katika vyuo vikuu mbalimbali nchini, ndio wapewe nafasi ya kwanza.

Kutokana na tamko hilo la Rais, serikali imedhihirisha kuwa pamoja na kuimarisha vyombo vyake vya ulinzi na usalama, pia ina nia ya dhati ya kupunguza tatizo la ajira kwa vijana ambalo kwa miaka mingi limekuwa likielezwa kuwa ni bomu linalosubiri kulipuka.

Aidha, kwa kutoa kipaumbele hicho kwa vijana waliomaliza mafunzo ya JKT ni dhahiri kwamba serikali ina nia ya dhati ya kuajiri watu wenye weledi katika taasisi hiyo nyeti.

Vijana hao ambao wamepitia mafunzo hayo kwa miezi mitatu, wamefunzwa mambo mbalimbali yakiwamo ya kimaadili na kizalendo, hivyo kuingia kwao katika chombo hicho kutasaidia kudumisha nidhamu ya jeshi.

Kabla ya kutumia vijana waliopitia mafunzo ya JKT, ajira katika vyombo vya ulinzi na usalama zilikuwa zikitolewa kwa kuzingatia sifa kama vile elimu angalau ya kidato cha nne na waombaji wapitishe barua za maombi ofisi za wakuu wa wilaya wanakotoka.

Utaratibu huo ulikuwa ukilalamikiwa kujaa upendeleo kwa baadhi ya watu wenye nafasi ndani ya vyombo hivyo kuwaingiza jamaa zao na matokeo yake kuingizwa watu wasio na sifa wakiwamo wenye rekodi zisizofaa.

Pia utaratibu huo ulikuwa ukidaiwa kugubikwa na vitendo vya rushwa na hata kuibuka kwa magenge ya kitapeli yaliyokuwa yakiwarubuni watu kuwa watawasaidia kupata nafasi hizo za ajira.

Kutokana na mfumo huu mpya wa kuajiri vijana waliopitia JKT, ni wazi kwamba vitendo vya kilaghai na rushwa havitakuwapo tena na watakaoajiriwa watakuwa wamechunguzwa kwa kiasi kikubwa ili kupata watu safi na wasio na rekodi mbaya ambao wanaweza kuharibu sifa ya jeshi.

Ni wakati sasa wa vijana waliomaliza mafunzo ya kijeshi JKT kuchangamkia fura hiyo ya ajira kwa kuwa itawawezesha, pamoja na kuajiriwa kuwa na nafasi za kujifunza utaalamu wa fani mbalimbali kama ilivyo kwa askari na maofisa wa sasa ndani ya JWTZ.

Habari Kubwa