Vijana wapewa nafasi Stars dhidi ya Nigeria

24Jul 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Lete Raha
Vijana wapewa nafasi Stars dhidi ya Nigeria

KOCHA Mkuu wa Tanzania, ‘Taifa Stars’, Charles Boniface Mkwasa kesho kutwa Jumanne amepanga kutaja kikosi kwa ajili ya kambi ya awali ya wiki moja kujiandaa na mchezo wa kukamilisha ratiba Kundi G dhidi ya Nigeria kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani Gabon.

Mkwasa maarufu kama Master, amesema lengo la kambi hiyo itakayoanza Agosti 1, 2016 ni kuwaweka sawa kisaikolojia wachezaji kabla ya kuita kambi nyingine rasmi wiki ya mwisho ya Agosti kujiandaa na mchezo dhidi ya Super Eagles ya Nigeria unaotarajiwa kuchezwa Lagos Septemba 2, mwaka huu.

Taifa Stars ipo Kundi G pamoja na Misri na Nigeria baada ya Chad kujitoa katika mbio za kuwania nafasi ya kushiriki AFCON ya mwakani nchini Gabon. Tayari Misri imejihakikishia nafasi hiyo baada ya kufikisha pointi 10, ikifuatiwa na Nigeria yenye pointi mbili, wakati Taifa Stars ina pointi moja.

Kwa sababu kambi ijayo ya Taifa Stars haiijengei timu ya taifa nafasi ya kushiriki michuano hiyo hivyo kuna umuhimu zaidi ya kuwaweka sawa kisaikolojia wachezaji vijana kwa kuwapa fursa ya kujiandaa na kushiriki kwenye mechi hiyo huku wakiwapumzisha wachezaji wakongwe ambao wanaweza kushindwa kutoa mchango kwenye timu ya taifa miaka mitatu ijayo.

Ingawa hatakiwi kusahau wachezaji wazoefu ambao bado wanaweza kukitumikia kikosi hiko kwa zaidi ya miaka mitano.

Tunamshauri Kocha Mkwasa kuwa na wachezaji wengi chipukizi na wenye uwezo wa juu ili waanze kupata uzoefu. Pia kuwapa nafasi ya kushirikiana na wachezaji wazoefu kama nahodha Mbwana Samatta anayechezea KRC Genk ya Ubelgiji., Thomas Ulimwengu anayechezea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Licha ya kuwa mechi hiyo haitaibeba Tanzania kwenye michuano hiyo, tunaona ni bora Samatta aje kutokana na umuhimu wa mechi hiyo kwenye rekodi zake binafsi kama mchezaji, lakini pia kuwapa moyo na ushauri kwa wachezaji chipukizi ambao atakuwa amewaita.

Tunatambua kuwa Samatta anakabiliwa na mechi muhimu za klabu yake za kufuzu hatua ya makundi ya Europa League lakini taifa kwanza kwani Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) linatuhimiza tuwe na utaifa kwanza na ndiyo maana inapotokea kuwa kuna michuano inayotambulika na shirikisho hilo na inayohitaji mchezaji kwenye timu yake ya taifa, tunawaruhusu wajiunge nayo mara moja.

Umuhimu wa Samatta kwenye klabu ni mkubwa lakini taifa ni zaidi, nahodha wetu huyo kwa sasa ametokea kuwa tegemeo la KRC Genk japokuwa amejiunga nayo Januari tu akitokea TP Mazembe ya DRC.

Samatta alifunga penalti ya tatu Alhamisi usiku, Genk ikishinda kwa penalti 4-2 dhidi ya wenyeji Buducnost usiku huu Uwanja wa Pod Goricom mjini Podgorica, Montenegro katika mchezo wa marudiano Raundi ya Pili ya mchujo wa kufuzu hatua ya makundi ya Europ League.

Timu hizo zilifikia kwenye matuta baada ya sare ya jumla ya 2-2, Genk ikianza kushinda 2-0, mabao ya Neeskens Kebano kwa penalti dakika ya 16 na Samatta dakika ya 79 Alhamisi wiki iliyopita kabla ya Buducnost kulipa kisasi kwa ushindi wa 2-0, mabao ya Radomir Dalovic dakika yakwanza na Milos Raickovic dakika ya 39.

Katika mikwaju ya penalti, mbali na Samatta wengine waliofunga upande wa Genk ni Thomas Buffel, Bryan Heynen na Dries Wouters ya mwisho, wakati za Buducnost zilifungwa na Risto Radunovic na Radomir Dalovic, huku Momcilo Raspopovic na Luka Mirkovic wakikosa.

Genk ilimaliza mchezo huo pungufu baada ya kungo wake Mghana, Bennard Yao Kumordzi kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 75 na sasa itamenyana na Cork City FC ya Ireland katika Raundi ya Tatu, mechi ya kwanza ikichezwa Julai 28 nyumbani na marudiano Agosti 4 ugenini.

Ikumbukwe timu zitakazoshinda zitakwenda hatua ya mwisho ya mchujo kuwania kupangwa kwenye makundi, ambako sasa vigogo kama Manchester United ya England wataanzia huko.

Ni matumaini yetu kuwa Samatta ataweza kuwa kiongozi kwa kuwafundisha wachezaji chipukizi ambao wataunda kikosi cha Stars kwa miaka ijayo.

Hivyo hatuna budi kuanza kufikiria kuachana na wachezaji wakongwe nakuwapa nafasi wachezaji chipukizi na wale wazoefu wenye umri mdogo ili kujenga kikosi bora kwa miaka minne au mitano ijayo.

Habari Kubwa