Vijengwe viwanda vya kurejeleza plastiki

30May 2019
Mhariri
DAR
Nipashe
Vijengwe viwanda vya kurejeleza plastiki

WATANZANIA bila shaka wanafahamu kuwa siku imefika kwa taifa kuingia kwenye zama za mwisho za kutumia mifuko ya plastiki.

Hapa nchini mifuko hiyo ni bidhaa ambazo zimetumiwa kwa miongo kadhaa.

Mifuko ambayo kuanzia sasa haitatumiwa ni kuanzia ile laini yenye viwango duni kiasi kwamba hata ukiweka bidhaa zinaweza kudondoka wakati wote kwa vile kifungashio hicho hakina kiwango wala sifa za kuhimili uzito.

Mifuko hiyo ikiwamo mingine mikubwa inayoitwa Rambo ina sifa mbaya ya kuchafua mazingira kuanzia viwanja vya nyumbani, shule, sehemu za wazi, vyanzo vya maji pamoja na baharini.

Kwa ujumla huharibu mazingira ya juu na chini ya ardhi kwa kasi ya kutisha na isiyo na dawa wala ufumbuzi wa haraka  kwa kuwa pamoja na kuua viumbe wa baharini na nchi kavu, taka hizi haziozi zikielezewa kuwa zinaishi kwa miaka zaidi ya 500 hata 1,000.

Kwa hali kama hiyo ni lazima plastiki iondoke na kwa kuanza ni kuchukua hatua kama hizo, ndiyo maana serikali imepiga marufuku matumizi ya mifuko hiyo ambayo kuanzia Juni mosi haitatumiwa popote,  badala yake mifuko yenye viwango vinavyokubalika ambavyo vimeshaidhinishwa na wataalamu wa mazingira, afya, ubora na usalama wa bayoanuai vitachukua nafasi yake.

Tunaunga mkono juhudi za serikali kupiga marufuku matumizi ya mifuko duni ya plastiki ambayo ni kitisho kwa maisha, lakini tunapenda kuishauri kuwa ni lazima kuwa na vifungashio bora na mbadala wa plastiki.

Tunasisitiza kwa uzito wa kipekee kujenga maeneo maalumu ya kukusanya bidhaa zote za plastiki ili zitumike kama malighafi za viwanda vya kurejeleza.

Ni wazi kuwa mbali na mifuko ya plastiki kuna tani kadhaa za mabaki ya bidhaa hizo kama vyombo vya nyumbani, maua, matairi, vifaa vya ofisini, maturubai, makasha ya kufungashia bidhaa kama soda na bia na kwa ujumla, mbali na mifuko hiyo nchi ina mabilioni ya tani hizo za  mipira ambazo haiozi.

Shime serikali na wadau, kupiga marufuku mifuko ya Rambo na jamii za plastiki kunakoanza kesho kutwa, kuwe mwanzo wa kuhimiza ujenzi wa viwanda vya kurejeleza na pia maeneo  mengi yakiwamo mijini na vijijini yatakayotumika  kukusanya taka zote za plastiki ili  kudhibiti uchafuzi wa mazingira.

Bidhaa za plastiki hutumiwa popote kuanzia mijini hadi vijijini tena kila dakika hutumiwa kufungasha bidhaa, mizigo, shehena  na zama hizi imeibuka kuwa miongoni mwa bidhaa zenye bei nafuu ikilinganishwa na chuma.

Kwa maneno mengine ni wazi kuwa matumizi ya plastiki yasiyo ya mifuko hayakwepeki. Cha kuangalia sasa ni ubunifu wa namna ya kufanya maandalizi mazuri ya kulinda watu na  bayoanuia isiangamizwe na bidhaa hizo.

Kwa kuwa ufungashaji bidhaa nao ni jukumu la kudumu kutengeneza vifungashio mbadala ni kazi ya kila mmoja.

Tunashauri wanaozalisha bidhaa waone umuhimu wa kuwa na vifungashio visivyoharibu mazingira na kuachana na plastiki.

Pengine ni wakati wa kuandaa sera za kuhamasisha viwanda, kampuni maduka makubwa na wawekezaji kuzalisha vifungashio vinavyooza ili kuondoa plastiki.

Tunaishauri taasisi za kitafiti na mafunzo ya ufundi kubuni teknolojia rahisi za kutengeneza vifungashio ili ziwe fursa za ajira kwa vijana, lakini pia kuendeleza harakati za kuondokana na plastiki zinazoharibu mazingira.

Habari Kubwa