Viongozi kwa hili la shule Dar mbadilike

22Jan 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Viongozi kwa hili la shule Dar mbadilike

WAKATI huu viongozi wa Dar es Salaam, wakiwamo mkuu wa mkoa na wengine kadhaa wanatafuta njia zote na kujituma kwa kila namna kufanikisha ujenzi wa madarasa ya sekondari King’ong’o ambayo wanafunzi wanakaa chini kutokana na kukosa madawati.

Lakini pia, wengine wanasongamana kwenye vyumba vya madarasa kwa sababu hawana madarasa ya kutosha.

Kwa kuzingatia maelekezo ya Rais John Magufuli, watendaji na viongozi wanafanya juhudi zote kukamilisha ujenzi huo, jambo ambalo limepata msukumo baada ya kuonywa na Rais kuwa kama hawatafanikisha jukumu hilo, waanze kutafakari njia zao.

Rais anachozungumzia hapa ni uwajibikaji na si kufanyakazi kwa utaratibu huo wa zima moto.

Viongozi kuwa karibu na wananchi ili kuhamasisha, kuanzisha na kusimamia miradi na shughuli za maendeleo ni jambo muhimu.

Kwa kutumia maelekezo ya Rais, anayowapa watumishi na viongozi mkoani Dar es Salaam, watendaji na wakuu wengine sehemu nyingine wabadilike.

Suala la madawati lipo. Ni sugu, viongozi walipatie ufumbuzi wa kudumu. Si hivyo, changamoto ya madarasa haijawahi kumalizika.

Ni suala linalohitaji ufumbuzi ili ufanikishaji wake uwe endelevu. Haipendezi kila mara kusubiri mpaka Rais azungumze, inaonekana kuwa viongozi wamepumzika na wanafanyakazi kwa mazoea.

Pamoja na changamoto za ukosefu wa madarasa, madawati na mabweni, vyoo shuleni ni changamoto.

Mara nyingi viongozi wanashindwa kusimamia uchimbaji wa mashimo na kujenga vyoo vya kisasa kwa ajili ya wanafunzi wetu. Tusijisahau huu ndiyo wakati wa kuwajibika na kuendesha shule kwa ujasiriamali.

Ni vyema viongozi wa mkoa na wilaya wakafikiria kuendesha shule kijasiriamali kwa kuanzisha migahawa na maduka ya kuuza bidhaa za wanafunzi ili fedha zinazopatikana zitumiwe kwa maendeleo ya shule.

Kwa mfano shule ziwe na maduka ya kushona sare, kuanzia suruali, mashati, sketi, sweta na soksi kwa ajili ya wanafunzi wake.

Kadhalika ziwekeze kwenye kuuza , daftari, kalamu, mifuko, karatasi , utoaji wa huduma za kuchapisha na kurudufisha nakala mbalimbali na fedha zinazopatikana ziingie kwenye mfuko wa shule.

Kadhalika wanafunzi wengi ni wateja wa vyakula, vinywaji na vitafunwa, kwa hiyo pengine ndiyo fursa kwa shule kufikiria utaratibu wa kuanzisha migahawa ya kupika na kuuza vyakula.

Tunaamini kuwa yote hayo yatawezekana iwapo kutakuwa na kamati za mapato na uchumi zinazolenga kufanikisha upatikanaji wa pesa za kuinua uchumi wa shule pamoja na kukuza uwekezaji.

Usimamizi wa biashara hasa za sare siyo mgumu kwa vile idadi ya wanafunzi inafahamika na hivyo mapato yao yanafuatiliwa kwa utaratibu unaojulikana.

Ni wazi wakati umefika kwa walimu, kamati kwa shule za msingi na bodi kwa zile za sekondari kubadilika na kuanza ujasiriamali.

Imekuwa ni kawaida kuendesha shule, hospitali na taasisi nyingine nyingi za umma kwa mazoea bila kuwa na mabadiliko wala mbinu za utafutaji na ujasiriamali.

Mbali na kukumbushwa jukumu la kusimamia na kujenga shule ni wakati wa viongozi, kuangalia namna bora ya utendaji kazi wao.

Tunaona kuwa kuna maeneo mengi yana upungufu, mathalani, uzoaji taka na usafi kwenye miji na majiji yetu.

Kuanzia Januari hadi Desemba miji, mitaa, mitaro na makazi yetu ni machafu. Kila mahali taka zimelundikana na harufu mbaya, tunajiuliza,tutaishi hivyo mpaka lini?

Kwenye maeneo mengine viongozi wameendelea kulega hasa kusimamia barabara, madaraja, utiririshaji maji taka na ufanyanyaji biashara holela.

Ni wakati wa kutafakari njia zetu na mabadiliko badala ya kuendeleza umangimeza na uzembe.

Habari Kubwa