Viongozi vyama vya soka mikoa tunataka maendeleo

09Jan 2017
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Viongozi vyama vya soka mikoa tunataka maendeleo

TAYARI vyama vingi vya soka vya mikoa ambavyo ni wanachama wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), vimefanya uchaguzi wake kwa mujibu wa katiba zinavyoviongoza na ile ya TFF.

Vipo vingine ambavyo vinaendelea na mchakagto wa uchaguzi ili kupata viongozi watakaoviongoza kwa vipindi visivyozidi miaka minne kabla ya kuitisha uchaguzi mwingine.

Ni wazi pamoja na kuwapo kwa changamoto nyingi zilizosababisha malalamiko kutoka kwa baadhi ya wajumbe kwenye chaguzi hizo, viongozi wameshapatikana kwa baadhi ya mikoa iliyofanya chaguzi zake.

Nipashe inaamini chaguzi hizo zimepita na kinachofuata ni viongozi kuchapa kazi na kuleta maendeleo yaliyokusudiwa na kuisaidia TFF kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya soka nchini.

Tunafahamu wazi yapo maeneo ambayo kumekuwa na ‘figisufigi’ nyingi za kiuchaguzi na kusababisha kuwapo kwa mgawanyiko kwa wajumbe wa mikoa husika.

Tunawakumbusha kuwa sehemu yoyote yenye mgawanyiko wa kiuongozi hakuna maendeleo ya kweli na kila jambo litakuwa halifanikiwi.

Ni vyema washindi na washindwa kwenye chaguzi hizo kwa mikoa ambayo tayari imeshafanya chaguzi zao na hata ile ambayo ipo kwenye mchakato, wakakaa pamoja baada ya uchaguzi na kupanga mikakati ya maendeleo.

Nipashe inafahamu yapo mengi yanayoongelewa juu ya chaguzi hizo huku kukiwa na mikoa ambayo imekuwa ikilalamika kuwa chaguzi zao ziliingiliwa na mamlaka ya juu ya soka nchini, TFF.

Wapo ambao walienda mbali na kudai mamlaka ya juu ya nchini inajaribu kuweka ‘watu wao’ kwenye mikoa ili kujihakikishia kuendelea kukaa madarakani katika uchaguzi ujao.

Pamoja na kuwa hakuna ushahidi katika hilo, Nipashe tunaamini kuwa kama ni kweli hilo si jambo sahihi na litaendelea kudumaza soka letu kwani viongozi watakuwa wakiingia madarakani kwa manufaa yao binafsi.

Tunatoa wito kwa viongozi wote wa mikoa ambao wameingina madarakani kipindi hiki, kufanya kile kilichokusudiwa, husuan kuhakikisha wanaleta maendeleo ya soka katika mikoa husika.

Kadhalika, kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF ambao ndio wapiga kura, wafahamu kura zao kwenye uchaguzi mkuu wa TFF ni ndio mustakabali wa maendeleo ya soka letu.

Ni udhaifu mkubwa kukubali kununuliwa na mgombea fulani ili tu kufanikisha hitaji la mgombea.

Kwa mikoa ambayo haina wawakilishi katika Ligi Kuu Tanzania Bara kama Iringa, Tabora, Mara, Dodoma, Lindi, Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Kigoma na mingineyo, ni wakati sasa kwa viongozi waliochaguliwa kuhakikisha wanalichukulia hilo kama moja ya changamoto muhimu katika kazi zao.

Hilo linawezekana kama tu mikakati itawekwa na viongozi waliopo madarakani kwenye kila mkoa husika.

Kwa mikoa ambayo tayari wanatimu shiriki kwenye ligi, waongezea maarifa ya kuzisaidia timu zao kufanye vizuri na hata kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara, bila kusahau kuanzisha ligi zitakazoibua vipaji vipya na kuviendeleza.

Habari Kubwa