Viongozi wapya Yanga wanahitaji ushirikiano

11May 2019
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Viongozi wapya Yanga wanahitaji ushirikiano

HATIMAYE baada ya mvutano wa muda mrefu, Klabu ya Yanga imepata uongozi mpya uliopatikana katika uchaguzi mkuu uliofanyika Jumapili iliyopita katika Ukumbi wa Bwalo la Maafisa wa Polisi Oysterbay jijini Dar es Salaam.

Viongozi hao ambao watakuwa na jukumu la kuiongoza Yanga kwa kipindi cha miaka minne ni Mwenyekiti Dk. Mshindo Msolla na Makamu wake, Fredrick Mwakalebela.

Aidha, viongozi hao watakuwa wakifanya kazi kwa karibu na Kamati ya Utendaji iliyochaguliwa siku hiyo ambayo inaundwa na Franck Kamugisha, Arafat Haji, Salum Rupia, Bahati Mwaseba, Saad Kimji, Rogers Gumbo, Ahmad Islam na Dominic Kata.

Kwanza kabisa Nipashe kama wadau wakubwa wa michezo nchini tunaipongeza Yanga kwa kufanya uchaguzi kwa amani na utulivu huku walioshindwa wakikubali matokeo. Huo unaonyesha ndio ukomavu na kukubali demokrasia iliyotumika.

Sisi tunasema huo ndio uanamichezo kama ilivyo mchezo wa soka ambao walikuwa wakiwania nafasi hizo ili kuusimamia ambao una matokeo matatu, kushinda, kushindwa na kutoka sare.

Na kwa bahati nzuri au mbaya katika uchaguzi huo hapakuwa na sare (kulingana kwa kura) na kilichotokea ni kushinda na kushindwa tu. Hata hivyo, uchaguzi sasa umepita na kinachotakiwa ni kuvunja makundi kisha kuwa kitu kimoja katika kuijenga Yanga imara.

Tunafahamu viongozi waliochaguliwa wanahitaji ushirikiano mkubwa kutoka kwa wagombea walioshindwa pamoja na Wanayanga wote.

Aliyekuwa mgombea wa nafasi ya Mwenyekiti, Tiboroha, ametangaza kuwa tayari kushirikiana na Msolla endapo atahitaji mchango wake kwa sababu yeye bado ni mwanachama halali wa Yanga.

Makamu Mwenyekiti, Yona Kevela, ameonyesha uanamichezo wake kwa kuridhika na matokeo na kuunga mkono viongozi waliochaguliwa huku akiichangia klabu yake hiyo Sh. milioni 20.

Si hivyo tu, Kevela pia ametangaza kuvunja kundi lake la wakati wa kampeni na kuahidi kuendelea kuwa karibu na viongozi waliochaguliwa.

Hicho ndicho kitu Nipashe tunataka kukiona kikiendelea kutokea kwa wagombea wengine walioshindwa kuvunja makundi yao na Wanayanga wote wakiwa kitu kimoja.

Lengo letu ni kutaka kuona Yanga ikihitimisha rasmi kipindi kigumu cha mtikisiko wa kiuchumi inachokipitia na kuimarika kama ambavyo watani wao wa jadi, Simba wanavyoimarika kila uchao.

Hilo litawezekana tu kama walioshindwa watavunja makundi yao na wanachama wote pamoja na mashabiki wa Yanga watakubali kuwa kitu kimoja na uongozi waliouweka madarakani katika kuipigania klabu yao.

Tunatambua uongozi mpya sasa utakaa na kuanza mikakati ya namna ya kutekeleza yale waliyoahidi ili kuweza kuijenga Yanga imara na kuitoa katika hali ngumu inayopitia.

Lakini ili kufanikiwa katika hilo, amani inatakiwa kutawala klabuni huku ushirikiano mkubwa ukihitajika kutoka kwa wanachama wote.

Sote tunatambua kuwa ubora wa timu ya Taifa, Taifa Stars kwa miaka mingi umekuwa ukitokana na kuimarika kwa klabu zote hususan Simba na Yanga, hivyo tunataka kuona ushindani ukirejea kwa klabu hizo mbili ili kuinua soka letu.

Tunawatakia kila la kheri viongozi wapya Yanga katika kuijenga upya klabu hiyo.

Habari Kubwa