Viongozi wasimuachie Rais kutatua kila kero

04Aug 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Viongozi wasimuachie Rais kutatua kila kero

MAMBO ambayo wengi bila shaka watakuwa waliyaona wiki iliyopita wakati Rais John Magufuli akirejea jijini Dar es Salaam akitokea wilayani Masasi mkoani Mtwara kwenye maziko ya Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, yamedhihirisha kuwa uwajibikaji bado ni tatizo kwa viongozi wengi wa umma.

Rais Magufuli aliamua kutumia usafiri wa barabara kupitia wilaya kadhaa za mikoa ya Lindi na Pwani kwa lengo la kuzungumza na wananchi pamoja na kusikiliza kero zao.

Kuanzia Somanga mkoani Lindi hadi Mkuranga, mkoani Pwani, wananchi walimweleza Rais kero ambazo katika hali ya kawaida zilitakiwa utatuliwa na viongozi wa maeneo hayo kama wakuu wa wilaya, wakurugenzi, wabunge na makatibu tawala wa wilaya husika.

Kero hizo zilijikita katika migogoro ya wakulima na wafugaji, wafanyabiashara kukosa vyoo kwenye masoko, uchakavu wa shule na uhaba wa madawati, kukosekana kwa mabari ya kubebwa wagonjwa, kutojengwa kwa kituo cha afya licha ya serikali kupeleka fedha na viongozi kukosa magari.

Kila Rais magufuli alipokuwa akipokea kero za wananchi na kuwaita viongozi kuzijibu, ilionekana dhahiri kuwa hawakuwa na majibu sahihi, hali iliyokuwa ikimfanya Rais kushangaa.

Jambo la kushangaza ni viongozi hususan wa kuteuliwa nawafanya nini katika maeneo yao ya utawala kama hawafahamu kero za wananchi kisha kuwajibika kwa kuzipatia ufumbuzi.

Kama viongozi hao wanakaa maofisini badala ya kuwafuata wananchi na kuwaulizia kero zao, ina maana hakuna wanachoisaidia serikali, ambayo ndiyo inayowalipa mishahara kila mwezi.

Tatizo tunaloliona ni kuwa viongozi wetu wengi katika ngazi mbalimbali wanashindwa kubadilika kiutendaji, badala yake bado wanaendelea na fikra zile zile za zamani za kufanya kazi kwa mazoea bila kujua kuwa enzi hizo zimepitwa na wakati.

Kinachotakiwa kwa sasa ni viongozi kuwa wabunifu, wachapa kazi kwa tija na ufanisi kwa kuwa mwisho wa siku kinachowapima ni utendaji wao.

Bila hivyo, tutaendelea kuwashuhudia watu wakikaa tu vijiweni wakisubiri kuteuliwa kuwa wakurugenzi, wakuu wa wilaya, makatibu tawala, wakuu wa mikoa na makatibu tawala wa mikoa bila kujua kuwa kukimbilia huko katika awamu hii ya uongozi hakuna kudekezana wala kubembelezana isipokuwa adhabu ya kushindwa kuleta matokeo ni kutumbuliwa.

Ingawa baadhi ya watu wanalalamikia utumbuaji wa majipu, lakini kimsingi hiyo ndiyo dawa kwa viongozi wanaoshindwa kutekeleza wajibu wao na kuwasubiri viongozi wa kitaifa kutatua kero za wananchi wakati ni majukumu yao.

Hatutarajii tena kuwaona wala kuwasikia viongozi wanaoshindwa kutatua migogoro ya wafugaji na wakulima katika maeneo yao wakati hilo ni jukumu lao la msingi, tena ndio wanaoziongoza kamati za ulinzi na usalama kwenye maeneo yao ya kiutawala.

Kwa upande mwingine, viongozi katika ngazi za wilaya na halmashauri wanapaswa kujiongeza kwa kuwa wabunifu kwa kuongexa vyanzo zaidi vya mapato. Kwa mfano, ni jambo lisiloeleweka kuwasikia wakuu wa wilaya na wakurugenzi kuwa wafanyabiashara kwenye masoko hawana huduma za vyoo.

Halmashauri zinaweza kujenga vyoo kwa vyanzo vyaka vya mapato kisha kuweka tozo kwa watumiaji, hivyo fedha hizo kurudia kama mapato yake. Wakati mwingine halmashauri inaweza kuwapa zabuni wawekezaji kutoa huduma hiyo kisha nayo kulipwa tozo.

Tunaona kuwa utaratibu wa Rais Magufuli kupita kwa wananchi anapopata fursa na kuwasikiliza, itamsaidia zaidi kuwabaini wateule wake kama wanatekeleza wajibu wao ipasavyo na kuwaondolea kero wanyonge, ili wasiofanya hivyo watumbuliwe.

Tunaamini kuwa hatua hiyo itawafanya viongozi wenye dhamana kuchacharika kutekeleza majukumu yao ya msingi ya kuwaondolea kero wananchi wanyonge.

Habari Kubwa