Viva miaka 57 ya uhuru mapambanao yanaendelea

09Dec 2018
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe Jumapili
Viva miaka 57 ya uhuru mapambanao yanaendelea

HONGERENI na pongezi nyingi ziwafikie Watanzania leo wanapoadhimisha Siku ya Uhuru wa Tanzania.

Wananchi wameonyesha moyo wa kuipenda nchi yao kujenga amani na utulivu na kuvumiliana hasa kwa kujali kuwa sote ni Watanzania.

Taifa linaposherehekea miaka 57 ya Uhuru kuna mengi ya kujivunia lakini tukiangalia yanayotokea wakati huu ambao serikali imejitolea kwa hali na mali kuifanya siku ya uhuru kuwa ni tukio la kuileta nchi maendeleo.

Tunaipongeza awamu ya tano kwa kuitumia siku hii kwanza kutumia fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili kusherehekea siku hiyo kutumika kujenga barabara kutoka Mwenge hadi Morocco hatua iliyopunguza msongamano kwa kiasi kikubwa jijini Dar es Salaam.

Mwaka huu tunaona tena serikali ikielekeza bajeti ya karibu Sh. bilioni moja iliyokuwa itumiwe kwenye siku ya leo , kuingizwa kwenye ujenzi wa hospitali mkoani Dodoma.

Tunaunga mkono hatua hii kwa kuwa inawekeza siku kuu ya uhuru wa Tanzania katika kuondoa umasikini, ujinga na maradhi. Inajenga uchumi wa taifa kwa kuweka miundombinu na si kuwekeza kwenye vyakula, vinywaji , sherehe ,fulana, mafuta ya magari, kugharamia  burudani na posho. 

Tunaona kuwa kufanya kazi za maendeleo kama kujenga miundombinu, madaraja na  hospitali kunakuwa na faida kubwa kwa Watanzania wote kwa kuwa wengi watanufaika na huduma hizo.

Ni imani yetu kila Mtanzania anapenda kuwa na maisha bora na yenye furaha. Hilo litawezekana kama tutajibidiisha kutumia rasilimali na muda kujenga taifa letu na kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye kupenda na kuvutia majirani wa Afrika Mashariki, Afrika na dunia.

Pamoja na jitihada zinazofanywa na serikali ni wazi kuwa miaka 57 inasherehekewa wakati taifa letu inatukumbusha kuwa tuna mengi ya kujirekebisha. Kama tulivyoshuhudia rasilimali zetu kama madini zimeliwa miaka mingi kutokana na mikataba mibovu.

Yote haya serikali imeyarekebisha na inaweza mifumo bora katika uwekezaji. Si hivyo imekabiliana na changamoto nyingi kama kupunguza tatizo la kukosekana ajira kwa vijana wetu, kuwa na idadi kubwa ya vifo vya wanawake na watoto, mimba na ndoa za utotoni na pia watu wengi kuendelea kuishi na umaskini.

Yote haya tunaona yakifanyiwa kazi na serikali ina ya kubadilisha hali hiyo kwa kuimarisha utawala na uongozi bora na wa umakini. Uongozi uliotukuka katika sekta ya umma unaotenda kazi kwa kuwajibika, watendaji wanaosimamia matumizi ya fedha za umma kwa uadilifu na miradi inayotekelezwa inakuwa na thamani inayolingana na pesa zinazotolewa.

Si hivyo tu miaka 57 ya uhuru, inashuhudia mapambano dhidi ya masuala yanayoangamiza taifa kama ubadhirifu unaopeleka fedha za umma kwa wala rushwa wachache, wizi na udanganyifu katika malipo na matumizi ya umma kama kulipa wafanyakazi hewa na  wastaafu marehemu yanadhibitiwa  ili fedha hizo zitumiwe kwa manufaa ya Watanzania.

Tunaipongeza serikali kwa jitihada nyingi inazofanya ili fedha zinazookolewa zitumika kusaidia kuongeza dawa hospitalini, kulipia gharama za elimu ya msingi, kugharamia wanafunzi kupitia mikopo ya elimu ya juu, kuanzisha Taasisi za mikopo ili kusaidia wakulima kuzalisha kwa tija.Jitihada zote hizi tunaona zinalenga kupunguza umaskini mijini na vijijini ili Watanzania waishi maisha bora zaidi .

Tunaungana na Watanzania wote kumshukuru Mungu kwa kulilinda taifa letu na kulifanya salama kwa miaka 57 ya uhuru. Mungu ibariki Tanzania , Mungu ubariki uhuru wetu.

Habari Kubwa