Viwanda viongeze uzalishaji sukari

01Dec 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Viwanda viongeze uzalishaji sukari

KILA mwezi Machi hadi mwishoni mwa Mei kila mwaka viwanda vya sukari nchini vinapokuwa kwenye matengenezo ambacho ni kipindi cha mvua nyingi, uzalishaji wa sukari husimama kwa muda, hali inayosababisha upungufu wa sukari na wakati mwingine bei kupanda.

Licha ya mikakati ya mara kwa mara kukabili upungufu wa sukari nchini, bado uhaba umekuwapo kiasi cha wananchi wengi kuathirika kwa kushindwa kutumia bidhaa hiyo kwa muda fulani.

Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Kilimo mwaka huu ilisema katika mwaka 2021/22 Wizara kupitia Bodi ya Sukari itahamasisha uzalishaji wa sukari kufikia tani 450,000 ambayo ni mahitaji ya nchi.

Ili kufikia lengo hilo bodi itafunga mitambo miwili ya maji moto itakayotumika kuzalisha mbegu bora za miwa katika mashamba ya pamoja ya wakulima wadogo yenye ukubwa wa hekta 200 katika Wilaya ya Kilombero.

Bodi itahamasisha matumizi ya mbolea na kutoa mafunzo kuhusu mfumo wa ununuzi wa pamoja wa mbolea kwa vyama 28 vya ushirika vya wakulima wa miwa.

Aidha, bodi ilisema itajenga miundombinu ya umwagiliaji katika mashamba mawili ya pamoja yenye ukubwa wa hekta 100 yaliyopo Kilombero, itaanzisha mashamba matatu ya mfano ya miwa katika maeneo yanayolimwa miwa ya Mtibwa, Kagera na Manyara.

Katika kukabiliana na uhaba huo, baadhi ya viwanda vina mkakati wa kuongeza uzalishaji kama ilivyofanya kampuni ya Sukari Kilombero imeongeza mtaji kutoka Sh. bilioni 340 hadi Sh. bilioni 700 kwa mwaka.
 
Kiwanda hicho kinasema mradi huo wa upanuzi utakaohitaji uwekezaji mpya wa awali wa zaidi ya Sh. bilioni 550, ukijumuisha kiwanda kipya kitakachokuza uwezo wa kampuni hiyo wa kutengeneza sukari na kupunguza uhaba nchini.

Wanasema lengo jingine ni kuhakikisha nchi inaondokana na upungufu wa bidhaa hiyo na nchi kujitosheleza ifikapo 2025, kwa kuwa utaongezeka kutoka tani 126,000 hadi 271,000 kwa mwaka na kuisaidia serikali kuokoa dola za Marekani milioni 70 za kuagiza bidhaa hiyo nje.

Pia, kiasi cha miwa kutoka kwa wakulima mwaka 2026/27 kwa takribani tani milioni moja kwa mwaka zaidi ya tani 600,000, ili kuchochea maendeleo ya sekta ya kilimo na kuboresha miundombinu na huduma za kijamii, ikiwamo kuongezeka kwa ajira 2,000 za kudumu na za mkataba 2,440.

Hii ni habari njema kwa kuwa itasaidia kupunguza uhaba wa sukari, pia tunaamini viwanda vingine vina mkakati kama huu kuhakikisha sukari ya kutosha inapatikana nchini.

Uhaba wa sukari uliibuka tena kwenye mkutano wa Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, ambaye alisema nchi hiyo ilitaka kuingiza sukari nchini, lakini walishindwa kutokana na kauli ya Waziri, ndipo Rais alimwambia suala hilo limekwisha wanaruhusiwa kuleta bidhaa hiyo nchini.

Tunaamini viwanda vikiongeza uzalishaji haba wa sukari utakwisha, lakini hilo litawezekana ikiwa wadau wote watahusika ikiwamo serikali kusikiliza kero za wazalishaji.

Kama viwanda hivi vingeanza uzalishaji mpango ulikuwa mzuri wa kuhakikisha wazalishaji wa nje wanauza miwa yao kwa kiwanda, na walihamasishwa kulima lakini hali haikuwa hivyo.

Kuna umuhimu Bodi ya Sukari ikahamasisha wawekezaji kuwekeza kwenye sekta hiyo ili kuepusha kuagiza kutoka nje na badala yake kuuza kwa nchi jirani.

Habari Kubwa