Viwango klabu za Ligi Kuu viimarishwe kuibeba Stars

04Jan 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Viwango klabu za Ligi Kuu viimarishwe kuibeba Stars

WAKATI timu ya soka ya Taifa (Taifa Stars) ikiwa imetinga hatua ya makundi ya kuwania tiketi ya kushiriki katika fainali zijazo za Kombe la Dunia, na kikosi chake cha wachezaji wa ndani kikifuzu kucheza michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (CHAN), maandalizi ya timu hizi yanaanzia kwenye Ligi Kuu

Taifa Stars ambayo sasa inafundishwa na Kocha Mkuu, Etienne Ndayiragije, ilitinga hatua ya makundi baada ya kuwaondoa Burundi, huku timu yake inayokwenda katika fainali za CHAN ilipata tiketi hiyo kufuatia ushindi wa jumla wa mabao 3-2 dhidi ya Sudan.

Kufuzu ilikuwa ni jambo moja, ambalo ni kubwa na la kujivunia kwa Watanzania wote, lakini kinachotakiwa kufanyika sasa ni kuwapo kwa maandalizi sahihi ya timu hizo.

Ili Tanzania iende katika mashindano hayo mawili yanayoandaliwa na kusimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), ikiwa imara, ni lazima kuwapo na Ligi Kuu Bara yenye ushindani na inayochezwa kwa kufuata kanuni na taratibu zilizowekwa.

Kwa nini tunasema haya? Kwa sababu idadi kubwa ya wachezaji wanaounda Taifa Stars wanatoka kwenye Ligi Kuu Bara, ambayo mzunguko wake wa kwanza unatarajia kukamilika wiki hii kwa timu kushuka kwenye viwanja mbalimbali.

Ni wazi kuwa, Ligi Kuu Tanzania inapokuwa yenye ushindani, wachezaji wake watakuwa imara na wenye viwango vizuri ambavyo vitakuwa tayari kushindana na nyota wa mataifa mengine.

Ni wazi kuwa hata kwenye fainali zilizopita za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon 2019), zilizochezwa mwaka jana, Taifa Stars ilikuwa ndio timu pekee yenye wachezaji wengi wanaocheza nyumbani, wakati Senegal ambayo walipangwa kundi moja, haikuwa na nyota hata mmoja anayecheza kwenye ardhi ya nyumbani.

Kama ni hivyo, klabu zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, zinatakiwa kujiandaa vema kuanzia katika mchakato wa usajili na maandalizi ya vikosi vyao, kwa faida ya taifa.

Umefika wakati wadau wa soka kila mmoja akaamini kuwa maandalizi ya kikosi cha Taifa Stars yanatakiwa kuanzia kwenye ngazi ya klabu na kamwe si ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), peke yake.

Ukiondoa timu hiyo, kikosi kilichobakia ambacho kitakwenda kupeperusha bendera ya nchi katika fainali za CHAN zinazotarajiwa kufanyika Aprili huko Cameroon, ndio haswa kinahitaji kuona ushindani katika Ligi Kuu Bara unaongezeka kwa sababu hali hiyo itasaidia kuimarisha na kuwajenga wachezaji.

Kambwe ligi nyepesi, isiyo na ushindani au isiyofuata kanuni na taratibu, haiwezi kutumika kuwaandaa wachezaji na michuano hiyo mikubwa ambayo itawapeleka kukutana na nyota wanaocheza ligi zilizoendelea kama Algeria, Morocco na Misri.

TFF inatakiwa kusimama imara kuhakikisha hakuna timu inayovunja kanuni kwa sababu kwa kufanya hivyo, haitasaidia kuimarisha wachezaji ambao taifa linawategemea.

Nipashe linawakumbusha pia wachezaji binafsi kuendelea kujituma wakapokuwa katika klabu zao na vile vile kujiandalia programu binafsi, ambazo tunaamini zitawasaidia kuwaimarisha na kuwa tayari kukabiliana na ushindani katika michuano wanayokwenda kushiriki mwaka huu.

Mafanikio katika soka hayapatikani kwa miujiza, hayapatikani kwa njia ya mkato, kinachotakiwa nchi kushiriki katika maandalizi sahihi yanayowaweka wachezaji tayari kwenda kupeperusha vema bendera ya Tanzania katika michuano hiyo.

Maandalizi ya zimamoto hayatakiwi kuwapo katika dunia hii, klabu ndio zinakaa muda mrefu na wachezaji na ndio zinawamiliki, hivyo wanatakiwa kuwaweka wachezaji katika hali nzuri na kutekeleza programu za makocha wao kikamilifu, ili pale watakapofika kwenye kambi ya Taifa Stars, wawe kwenye kiwango bora na chenye kusaidia kusaka matokeo chanya.

Habari Kubwa