Viwanja vya CCM kuwekwa nyasi bandia mbona kimya?

10Jan 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Viwanja vya CCM kuwekwa nyasi bandia mbona kimya?

JUNI mwaka jana, Bunge lilipitisha pendekezo la serikali la kusamehe kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwenye nyasi bandia kwa viwanja vya mpira wa miguu katika majiji ili kuendeleza michezo na kukuza vipaji nchini.

Ni wakati Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba alipokuwa akiwasilisha mapendekezo ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2021/22 Bungeni Dodoma kwa ajili ya kujadiliwa.

Nchemba alisema viwanja vingi ni vibovu sana na ubovu wa viwanja hivyo unasababisha baadhi ya timu kutopata matokeo mazuri zinapokwenda kucheza hususan mikoani.

Ikasemwa kuwa mpango huo ukikamilika, basi kwenye bajeti ya msimu huu au misimu ijayo, serikali inaweza kuangalia suala la msamaha hata kwenye mikoa, wilaya na sehemu zingine.

Lakini Nipashe tunaona kimya kikizidi kutawala katika utekelezaji wa mpango huo wa nyasi bandia, kwani tangu msamaha huo kutolewa hakuna juhudi zozote zimeonekana kuendelea hadi sasa.

Wadau wa soka hususan Kampuni ya Azam Media, imekuwa ikifanya marekebisho ya viwanja kwa kuweka taa, na tayari Uwanja wa Jamhuri Dodoma ukiwa umefungwa taa, huku wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi ukiendelea na matengenezo hayo, mchakato ambao tulidhani ungeenda sambamba na uwekaji wa nyasi bandia viwanjani.

Tunakumbuka hata Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, aliwahi kuongelea kuhusu suala la ubovu wa viwanja ambavyo vingi vinamilikiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), akikitaka kurekebisha viwanja vyake na kama hakiwezi, basi waangalie jinsi gani ya kuingia makubaliano na wawekezaji.

Hii inaonyesha kuwa serikali ya Tanzania chini ya Rais Samia bado ina nia nzuri na soka katika kuendeleza soka la nchi hii, lakini inaonekana kuna tatizo mahala, ambalo linahitaji kutatuliwa ama kushughulikiwa ili mambo yaende sawa.

Tunaamini bado kuna baadhi ya watendaji ndani ya chama hicho wenye fikra potofu kwamba michezo ni burudani, afya, upendo, kufahamiana na kudumisha undugu pekee, bila kutambua ni ajira kubwa duniani na inaweza kutua fursa pana kwa vijana kujiajiri na kupunguza mzigo kwa serikali.

Kama hiyo haitoshi, michezo pia kwa sasa inazipatia serikali nyingi mapato mengi kuliko hata baadhi ya kampuni, lakini ni sehemu ambayo inatoa ajira kwenye nyanja nyingi, ikiwamo wanamichezo, wafanyabiashara, makocha, madaktari, wauguzi, mama lishe, machinga ambao wanauza jezi na kadhalika, hivyo suala la ubora wa viwanja haliepukiki kwa sasa.

Tulitegemea hadi leo hii, hata kama nyasi za bandia hazijafika, lakini wadau wa soka wangekuwa wameshapewa mrejesho kuwa yale yaliyotamkwa na rais huku pia yakipitishwa bungeni dalili za utekelezaji zingeonekana, lakini wapi!

Inasikitisha kuona Ligi Kuu Tanzania Bara ikizidi kupata sifa ndani na nje barani Afrika huku wachezaji wengi wakivutiwa kuja kucheza nchini hadi Ligi Daraja la Kwanza (Championship), lakini viwanja vikiendelea kulitia doa soka letu kila uchao ndiyo maana tumeona ipo haja ya kuwakumbusha tena wamiliki wa viwanja hivyo kuna umuhimu wa kuvifanyia maboresho hayo mapema kupitia msamaha huo wa VAT kwa nyasi bandia.

Habari Kubwa