Vyama vya siasa, polisi kukutana ni hatua nzuri

08Sep 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Vyama vya siasa, polisi kukutana ni hatua nzuri

KATIKA siku za karibuni kumekuwapo na hali isiyo rafiki katika tasnia ya kisiasa nchini.

Hali hiyo inatokana na kuibuka kwa malumbano na mivutano kati ya baadhi ya vyama vya siasa dhidi ya Ofisi ya Msajili na Jeshi la Polisi ambapo vyama vinazilalamikia taasisi hizo mbili kuwa hazivitendei haki.

Vyama hivyo ambavyo ni vikubwa vimekuwa vikidai kuwa taasisi hizo mbili zinavikandamiza badala yake zinakipendelea Chama Cha Mapinduzi (CCM) kama chama tawala hususan katika suala la mikutano ya ndani.

Rais Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani aliruhusu vyama vya siasa kufanya mikutano ya ndani, lakini hivi karibuni vyama vya siasa vimekuwa vikilalamikia Jeshi la Polisi katika maeneo kadhaa nchini kuizuia mikutano ya ndani.

Hata hivyo, hakuna sababu rasmi zinazotolewa na makamanda wa jeshi hilo kuhusiana na uamuzi wake wa kuikataza mikutano hiyo wala kueleza ni mamlaka zipi zimetoa maagizo hayo.

Kadhalika, baadhi ya vyama vimekuwa vikitoa malalamiko dhidi ya Ofisi ya Msajili kwamba haivitendei haki, jambo ambalo kimsingi, limekuwa ikionyesha dalili mbaya kwa taasisi zetu kwa umma.

Tunaona hivyo kwa kuwa malumbano na majibishano kati ya wanasiasa wa upinzani na taasisi hizi za umma, kila uchao yamekuwa yakiibua mijadala mbalimbali ikiwamo kwenye mitandao ya kijamii, huku wananchi wakitoa kauli mbalimbali.

Mtazamo wetu ni kwamba hali hii inalitia doa taifa letu ndani nan je ya nchi yetu katika suala zima la haki za binadamu, demokrasia na utawala bora, hivyo kuwapo haja ya kuweka mambo sawa.

Hata hivyo, tumefarijika kusikia taarifa kwamba Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa, vyama vya siasa na Jeshi la Polisi likiongozwa na Mkuu wa Jeshi hilo (IGP), Simon Sirro, wanatarajia kukutana katika mkutano wa maridhiano.

Taarifa hiyo iliyotolewa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi juzi, ilieleza kwamba lengo la mkutano huo ni kuweka sawa namna ya kuendesha shughuli za kisiasa nchini bila kukwaruzana.

Jaji Mutungi akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, alisema lengo pia ni kujadili namna ya kuondoa kile kinachoonekana kwamba upo uhasama kati ya Jeshi la Polisi na vyama vya siasa pamoja na namna ya kuweka vizuri utaratibu wa kuendesha mikutano ya kisiasa.

Kwa upande wetu tunaona kuwa hatua ya kuitishwa kwa mkutano wa maridhiano ni nzuri na muhimu kwa afya ya taifa letu, ambalo limekuwa na utulivu mkubwa tangu baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Pamoja na hatua hii kuchelewa, tunampongeza Jaji Mutungi kwa kueleza ukweli wa mambo kwamba mvutano kati ya vyama hivyo na Jeshi la Polisi, limeanza kujenga taswira hasi kwa umma.

Hivyo basi tunamshauri Jaji Mutungi kuweka mazingira bora na rafiki ili pande husika ziaminiane badala ya kwenda kulumbana badala ya kufuta taswira iliyopo kwa umma.

Habari Kubwa