Vyumba vya kuhifadhi maiti vya hospitali za serikali viboreshwe

04Mar 2016
Mhariri
Dar
Nipashe
Vyumba vya kuhifadhi maiti vya hospitali za serikali viboreshwe

KATIKA toleo letu la jana, tulichapisha habari kuhusu chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali Teule ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi kwamba kimezidiwa uwezo kutokana na majokufu ya kuhifadhia maiti kuharibika.

Kwamba hali hiyo imetokana na jokofu moja kuharibika kwa miaka nane sasa huku moja lililobaki likifanya kazi ‘chemba’ (droo) moja, hali inayosababisha baadhi ya maiti kupangwa mbili mbili katika jokofu moja na nyingine kuwekwa sakafuni.

Pia tulieleza kuwa kuna uhaba wa vitendea kazi zikiwamo dawa za kutunzia maiti ili siharibike haraka. Kutokana na hali hiyo, miili mingi inaharibika na kusababisha Halmashauri ya Kibaha kuamua kuizika. Hata hivyo, pamoja na haki mbaya ya chumba hicho, hospitali hiyo inaendelea kupokea miili na kuihifadhi katika chumba hicho.

Hospitali ya Tumbi imekuwa ikipokea miili mingi hususan ya ajali zinazotokea katika barabara kuu ya kwenda mikoa ya kaskazini.

Hali hiyo inalalamikiwa na wauguzi kwamba wanafanya kazi katika mazingira magumu ikiwamo harufu na kutokulipwa fedha kwa ajili ya kuifanyia miili uchunguzi kama mwongozo wa waraka wa serikali unavyoelekeza kuwa wanaoshirikiana na madaktari kufanya uchunguzi walipwe Sh. 50,000 na daktari Sh. 100,000.

Vyumba vya kuhifadhi maiti karibu katika hospitali zote za serikali nchini viko katika hali mbaya na miundombinu yake ni ya zamani na sababu za kuwa katika hali hiyo hazijulikani.

Hali hiyo inawafanya watu wenye uwezo wa kiuchumi na wenye madaraka kupeleka miili ya ndugu na jamaa zao kuhifadhiwa katika hospitali binafsi.

Hata hivyo, sababu iliyo wazi ni kwamba serikali haijaona umuhimu wa kuweka miundombinu ya kisasa kama vyumba vikubwa, vifaa yakiwamo majokofu ya kutosha na imara, dawa za kutosha kwa ajili ya kutunza maiti pamoja na kuwalipa fedha za motosha madaktari na wauguzi wakati mwafaka.

Ni mazingira hayo rafiki yanaweza kuwafanya madaktari, wauguzi na watumishi wengine katika hospitali za serikali kuwa na ari ya kutoa huduma bora kwa wagonjwa.

Tunatambua kwamba hospitali hutoa kipaumbele kwa mtu aliyehai na kuelekeza rasilimali chache zilizoko katika kuokoa maisha, lakini pia ubora wa vyumba vya kuhifadhi maiti ni muhimu kwa kuwa binadamu anahitaji huduma nzuri hata kama ni marehemu.

Wakati huu ambao serikali ya awamu ya tano imeahidi kuboresha huduma za jamii zikiwamo za afya, hainabudi kuondoa kero hii kwa kuhakikisha kwamba ujenzi na ukarabati wa hospitali na vituo vya afya unakwenda sambamba na uboreshaji pamoja na ujenzi wa vyumba vya kuhifadhi maiti.

Bila shaka kero zilizoko Hospitali ya Tumbi, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu atakuwa amezisikia, hivyo ni matumaini yetu kwamba atakwenda kuzishuhudia na kuzishughulikia haraka.

Hata hivyo, waziri huyo na wasaidizi wake wasiishie Tumbi, bali watembelee hospitali zote za serikali washuhudie jinsi hali ya vyumba vya kuhifadhi maiti inavyotisha kisha waeleza umma ni hatua zipi zitachukuliwa na serikali.

Ikiwa vyumba vya kuhifadhi maiti vitaboreshwa katika hospitali zote za serikali, wananchi wataondokana na kero na kuamini kuwa serikali ya Rais Dk. John Magufuli, ina nia ya dhati ya kuboresha huduma za afya.

Habari Kubwa