Waamuzi wameianika TPLB, mtendaji mpya sasa isafishe

10Feb 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Waamuzi wameianika TPLB, mtendaji mpya sasa isafishe

HABARI ya mjini katika soka la Tanzania Bara kwa sasa ni kuvurunda kwa waamuzi hususan wanaochezesha Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza.

Ni zaidi ya wiki tatu sasa kelele za kuvurunda kwa waamuzi zimetawala kila kona nchini jambo ambalo liliiamsha serikali na kulitaka Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kuketi na Shirikisho la Soka nchini (TFF) kutafuta ufumbuzi.

Matukio yanayolalamikiwa zaidi na wadau wa soka ni waamuzi kutochezesha kwa haki ama kwa madai ya kuchukua rushwa au kushindwa kuzitafsiri vema sheria 17 za soka hususan sheria ya kuotea (offside).

Hali hiyo, imechangia baadhi ya timu kupoteza mechi zao za ligi hiyo, na kuzua malalamiko makubwa kutoka kwa viongozi wa klabu, wachezaji, makocha hadi kwa mashabiki na wadau wa soka.

Awali, suala hilo lilionekana kama lipo kwa ajili ya kuwabeba mabingwa watetezi na vinara wa ligi hiyo, Simba pekee kabla ya kubainika pia kwa Yanga, Azam FC na hatimaye kwa kubainika ni kwa klabu zote za Ligi Kuu na uozo huo pia kubobea Ligi Daraja la Kwanza.

Nipashe ambalo limekuwa likifuatilia kwa makini kila mchezo wa Ligi Kuu na ile ya Ligi Daraja la Kwanza, lilishaeleza udhaifu mkubwa wa kutofuatwa kwa sheria 17 za soka kabla hata ya wimbi hilo nzito kutanda.

Hata hivyo, kilio hicho kilisikika baada ya kelele nyingi na kumuibua waziri mwenye dhamana na michezo nchini, Dk. Harrison Mwakyembe, ambaye alipeleka moto BMT, huku Rais wa TFF, Wallace Karia naye akiwahi kwa kuitaka TPLB kuchukua hatua.

Kwa ujumla TPLB ikionekana kulala na kusahau wajibu wake wa kuhakikisha inatatua kero zote katika ligi hizo mbili za juu nchini, hadi ilipokurupushwa baada ya mambo kuharibika.

TPLB ilikurupushwa na kisha kuketi na kuwachukulia hatua baadhi ya waamuzi akiwamo mwamuzi namba mbili, Kassim Safisha wa mechi kati ya Simba na Namungo FC ambaye alifungiwa kwa kipindi cha miaka mitatu.

Hata hivyo, wadau wa soka wameielezea adhabu, hiyo kama ya kimhemuko zaidi kufuatia kuwa kubwa ikilinganishwa na aina la kosa ambalo ni la kushindwa tu kutafsiri vema sheria ya kuotea na kulikubali bao la mshambuliaji wa Simba, Meddie Kagere.

Kadhalika, adhabu hiyo iliwaibua baadhi ya waamuzi ambao hawakuficha kilio chao cha kutolipwa stahiki zao kwa muda mrefu pamoja na kufichua madudu makubwa katika upangwaji wa kuchezesha mechi hizo.

Ingawa ni mengi waliyoeleza, lakini hilo la kutolipwa posho zao na kulimbikiza hadi baadhi kueleza wapo wanaodai kuanzia Sh. milioni moja hadi kumi, linatufikirisha zaidi hasa tukizingatia waamuzi hawana mishahara.

Ingawa awali kabla ya TPLB kukaa na kuchukua hatua hiyo, Rais Karia kupitia radio moja nchini aliulizwa kuhusu uwapo wa tetesi za waamuzi kudai kutolipwa kwa wakati akageuka mbogo, lakini hili linapaswa kutazamwa kwa jicho la tatu hususan wakati huu ambao TFF imemtangaza Mtendaji Mkuu mpya wa TPLB, Almas Kasongo.

Kwa mtazamo wetu, hatutaki kuamini kwamba waamuzi wote wanahongwa ili kukanyaga sheria 17 za soka, bali tunaamini wapo wanaoshindwa kuzitafsiri vema na wengine pia wakiingia uwanjani huku wakiwa na mawazo ya kimaisha kutokana na hali ngumu ya kutolipwa posho zao.

Hivyo, si wakati tu wakuwaadhibu kwa kuwapa vifungo virefu, bali Mtendaji Mkuu wa TPLB, Kasongo aanze kwa kumulika malipo yao.

Habari Kubwa