Waamuzi wapigwe msasa wasiharibu ligi msimu mpya

04Sep 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Waamuzi wapigwe msasa wasiharibu ligi msimu mpya

KLABU za Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara kwa sasa zipo katika maandalizi makali kuelekea msimu mpya wa 2021/22 utakaofunguliwa rasmi Septemba 25, mwaka huu, kwa mechi ya Ngao ya Jamii kati ya Simba na Yanga itakayopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Baada ya mchezo huo wa Ngao ya Jamii, msimu mpya utaanza rasmi Septemba 29, mwaka huu, ambapo timu 16 msimu huu zitawania ubingwa wa ligi hiyo unaoshikiliwa na Simba kwa misimu minne mfululizo sasa.

Tofauti na miaka iliyopita Ligi Kuu msimu huu inatarajiwa kuwa na ushindani mkali kutokana na historia mpya ya udhamini, iliyowekwa na Kampuni ya Azam Media Limited kwa kuingia mkataba mpya wa haki za matangazo ya Televisheni katika ligi hiyo na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Katika mkataba huo ulioingiwa Mei 25, mwaka huu, utadumu kwa kipindi cha miaka 10 kuanzia msimu ujao wa 2021/22 ukiwa na thamani ya Sh. bilioni 225. 6, ambapo mbali na kiasi hicho, kutakuwa na bonasi kubwa kuanzia bingwa hadi timu itakayoburuza mkia.

Kwa mujibu wa mkataba huo, zawadi za fedha kwa mshindi wa kwanza msimu ujao wa ligi itakuwa Sh.milioni 500, mshindi wa pili milioni 250, watatu milioni 225, wanne milioni 200 na fedha hizo zitakwenda zikipungua hadi timu itakayoburuza mkia huku zile zitakazocheza mechi ya mchujo (play off), kila moja ikilamba Sh. milioni 20.

Hicho ni kiasi pekee kitakachotolewa kutokana na udhamini huo haki za matangazo ya televisheni, ukiacha udhamini wa matangazo ya radio lakini na wadhamini wenza wengine wa ligi hiyo, ikiwamo Benki ya KBC.

Ongezeko hilo la zawadi, limezifanya klabu nyingi kuwa na uhakika wa kuwalipa wachezaji wake, hivyo kuzifanya hata zile zilizokuwa hazifanyi usajili wa wachezaji wakigeni kuingia sokoni kwenye dirisha la usajili lililofungwa rasmi Jumanne saa sita usiku na kusajili nyota kutoka nje ya nchi.

Hilo linatufanya kuamini kwamba ligi ya msimu huu itakuwa na ushindani mkubwa mwanzo mwisho, hivyo ni wakati sasa kwa TFF na Bodi ya Ligi (TPLB) kuwa makini katika usimamizi hususan kwa suala zima la upangaji ratiba ili kutoziumiza baadhi ya klabu.

Mbali na hilo, Chama cha Waamuzi Tanzania (FRAT), hakina budi kuwaandaa waamuzi wake ipasavyo kwa kuzidi kuwapa semina ya kukumbushana kanuni na sheria 17 za soka ili kuchezesha kwa haki na kuondoa malalamiko ambayo tumekuwa tukiyasikia kila msimu.

Tunatambua yapo mabadiliko kadhaa ya kanuni ama sheria za soka ambayo yamefanyika, hivyo ni jukumu pia la kila mwaamuzi kujiongeza kwa kujifunza mabadiliko hayo badala ya kuisubiri FRAT kuandaa semina/darasa kwao, jambo ambalo litawasaidia kutekeleza majukumu yao kwa haki na weledi.

Katika hilo si waamuzi pekee, bali pia kuna haja ya uongozi wa kila klabu kuandaa semina kwa wachezaji wao na kuwaelekeza baadhi ya kanuni zilizobadili ili kuepuka kufanya makosa yasiyo ya lazima, lakini pia kupunguza malalamishi kwa waamuzi pindi ligi hiyo itakapoanza.

Tunatambua wapo wachezaji wengi hata baadhi ya makocha bado hawaelewi baadhi ya kanuni zilizobadilika, jambo ambalo kila uongozi wa klabu hauna budi kutafuta wakufunzi wa soka wabobezi ili kutoa darasa kwa mabenchi yao ya ufundi pamoja na wachezaji, haya yakifanyika kwa makini kuanzia kwa waamuzi, makocha hadi wachezaji, tunaamini tutashuhudia ligi ya viwango zaidi msimu huu.

Habari Kubwa