Waamuzi wasiishie kumulikwa Ligi Kuu, Championship ni tatizo

17Jan 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Waamuzi wasiishie kumulikwa Ligi Kuu, Championship ni tatizo

KUMEKUWA na malalamiko mengi ya kuboronga kwa baadhi ya waamuzi kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara inayoendelea nchini, labda ni kwa sababu ndiko kuna timu pendwa zenye mashabiki wengi wa Simba na Yanga ndiyo maana sehemu kubwa za wanaopiga kelele na kukemea kuboronga kwa marefa ni wale wale wa....

timu hizo.

Pia inawezekana ni kwa sababu watu wengi wanapata nafasi ya kuziangalia mechi nyingi za Ligi Kuu kuliko za Championship.

Ukweli ni kwamba hata huko pia kuna matatizo kama haya kwenye Ligi Kuu, kwani baadhi ya timu zimekuwa 'zikinyongwa mchana kweupe', kwa sababu huko hakuna ushahidi wa mechi kuonyeshwa kwenye televisheni, hivyo ni kama machozi ya samaki tu, yanabaki majini.

Hata hivyo, kama ilivyo Ligi Kuu, pia kwenye Championship kuna timu zimewekeza hasa ukitazama namna ambavyo kumefanyika usajili wa hali ya juu msimu huu, ambapo tumeshuhudia wachezaji wengi wa kigeni baadhi wakiwa wameshawahi kucheza timu kubwa za hapa nchini kama Simba, Yanga na Azam FC.

Mbali na Nipashe kuwa makini katika kufuatilia Ligi ya Championship na kujionea aina ya maamuzi mabovu ambayo yamekuwa yakitolewa, lakini tayari baadhi ya timu zimekuwa zikilia kutokana na uchezeshaji mbaya kutoka kwa baadhi ya waamuzi, ingawa ni vigumu kwa mashabiki wengi kupaza sauti kutokana na kuwa 'bize' na klabu zao pendwa Simba, Yanga na Azam FC.

Lakini ikumbukwe kuwa ligi hiyo ndiyo inayotoa timu zinazopanda daraja kwenda kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara, hivyo uwapo wa waamuzi wanaongozwa na sheria 17 za soka na kutenda haki, ni muhimu ili timu zitakazopanda, ziwe zimestahili kweli na hatimaye kutoa ushindani mkubwa msimu ujao.

Tumeona kwa miaka ya hivi karibuni, timu zinazopanda Ligi Kuu kutoka chini, basi moja au mbili ni lazima zishuke tena daraja msimu huo huo, jambo ambalo linaonyesha kuwa huenda zilipanda kwa mbeleko za waamuzi, hivyo kushindwa kukabiliana na ushindani uliopo Ligi Kuu.

Kwani ni wazi kwamba kama timu ilipanda kwa kuungaunga, hakuna namna lazima itarudi tu ilikotoka, jambo ambalo linazidi kurudisha nyuma ukuaji wa soka letu kila uchao.

Lengo letu ni kutaka kuona kupungua kwa timu Ligi Kuu na kubaki 16, kunaongeza ushindani ili kuifanya ligi yetu kukua na kuwa kivutio, lakini kwa mwenendo huu wa maamuzi mabovu, tutazidi kuona tukipiga hatua mbili mbele na tatu nyuma.

Hivyo, wakati huu ambao tayari mzunguko wa kwanza umemalizika kwenye Ligi ya Championship, tunalikumbusha Shirikisho la Soka nchini (TFF), Bodi ya Ligi (TPLB) na Chama cha Waamuzi Tanzania (FRAT) kuwa makini na waamuzi wenu wanaochezesha mechi hizo kwa kufinyanga sheria 17 za soka.

Ni wakati sasa wa kuanza kuzifuatilia mechi hizo ili kukabiliana na madudu ya baadhi ya waamuzi ambao wanakwenda kinyume cha kiapo cha marefa cha kutoa maamuzi ya haki uwanjani kwa kutimiza sheria 17 za soka.

Tunaamini kama haki ikitendeka, timu zitakazopanda Ligi Kuu, zitaenda kutoa ushindani wa kweli na si kuishia tu kuwa wasindikizaji kwa kucheza msimu mmoja na unaofuata kushuka daraja.

Lakini, ikumbukwe waamuzi wana nafasi kubwa zaidi ya kuliweka soka letu katika viwango vya juu endapo watatenda haki, hivyo ni matarajio yetu kwa baadhi ambao wanahadaika na kutanguliza maslahi yao binafsi, wataacha tabia hiyo mara moja.

Hivyo, TFF, TPLB na FRAT jicho la ziada linahitajika Ligi ya Championship ikiwa ni pamoja na kuwachukulia adhabu kali waamuzi wote watakaobainika kufinyanga haki kwa kutotekeleza sheria 17 za soka dimbani.

Habari Kubwa