Wachezaji, timu zijipange kwa usajili

19Jul 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Wachezaji, timu zijipange kwa usajili

LIGI Kuu Tanzania Bara kwa msimu wa 2020/21 imefikia tamati jana, kwa mabingwa Simba kukabidhiwa kombe lao ikiwa imelitwaa kwa mara ya nne mfululizo.

Simba ilikabidhiwa taji hilo baada ya mchezo wake dhidi ya Namungo FC mchezo uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Kumalizika kwa ligi hiyo maana yake sasa ni maandalizi kwa ajili ya msimu mpya wa 2021/22.

Timu sasa zinafanya tathmini ya kile ilichovuna kuanzia mwanzo wa mashindano hadi mwisho, kama wamefikia malengo au wamekwama.

Ikiwa wamefikia malengo ni jambo zuri, lakini kama wamefeli waangalie wapi walipojikwaa na kurekebisha baadhi ya makosa waliyofanya ili yasijirudie katika msimu ujao wa ligi.

Kumalizika kwa ligi hiyo sasa timu zimeanza kuimarisha vikosi vyao kama kufanya sajili za wachezaji wapya ili tu kuimarisha mabenchi yao ya ufundi kwa ajili ya msimu unaokuja wa Ligi Kuu ya Tanzania.

Licha ya kuwa dirisha la usajili bado halijafunguliwa, tayati timu zimeanza kuangalia na kuwataja wachezaji ambao wanawania kuwasajili ili kuimarisha vikosi vyao.

Katika madirisha ya usajili mara nyingi kumekuwa na utata hasa kwa wachezaji kusaini timu zaidi ya moja, tuliwahi kuona kwa nyota kama winga Mrisho Ngasa mwaka 2013 wakati akijua fika ana mkataba na Azam FC, lakini alisaini mkataba wa siri na Yanga jambo lililomfanya apigwe faini ya Sh. milioni 45 kwa kosa hilo.

Kiungo mshambuliaji Mohamed Mkopi mwaka 2016 alijikuta akikaa nje ya uwanja mwaka mzima baada ya kusaini timu mbili wakati akijua fika bado hajamalizana na waajiri wake Tanzania Prisons, akasaini kwa watani wao wa jadi Mbeya City jambo lililomfanya akutane na rungu hilo.

Pius Buswita, ambaye alidumu katika kikosi cha Yanga kwa miaka miwili wakati anaondoka Mbao aliingia kandarasi na Simba lakini baadaye akasaini Yanga, jambo ambalo likamfanya apitiwe na rungu la kufungiwa na kutakiwa kurudisha fedha za Simba.

Naye kiungo wa zamani wa Kagera Sugar, Ludovic Venance mwaka 2017 alipitiwa na rungu baada ya kusaini mkataba mpya na African Lyon, wakati akijua fika kuwa bado ni mwajiriwa wa Mbao FC, ambapo alijikuta akikosa michezo minne ya timu yake mpya.

Sakata kama hili pia limetokea msimu wa 2020/21 ambapo kiungo Benard Morrison, amesaini kandarasi na Simba wakati klabu ya Yanga ikidai kuwa ina mkataba na mchezaji huyo ambapo hadi sasa kesi ya wawili inaendelea katika mahakama ya usuluhishi CAS.

Wakati tukisubiri Shirikisho la Mpira wa Miguu kutangaza tarehe ya ufunguzi wa dirisha la usajili nataka kutoa rai kwa wachezaji pamoja na klabu kuwa makini kipindi hiki ili kukwepa kukutana na adhabu za kufungiwa na kulipishwa faini kwa kosa ambalo limekuwa likijirudia misimu nenda rudi.

Nipashe tunaamini timu pamoja na wachezaji watajifunza kupitia kwa mifano hii ambayo iko wazi ili kulinda taswira ya Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na wao katika jamii ya wapenda soka.

Kwa sababu mchezo wa soka ni wa burudani hivyo, haipendezi kuona wachezaji wakifungiwa kwa kutokuwa makini kwenye usajili, hivyo tunaamini kwamba, sakala hilo halitatokea kuelekea kwenye dirisha la usajili.

Habari Kubwa