Wachezaji waheshimu mikataba kulinda vipaji

04Sep 2017
Mhariri
Nipashe
Wachezaji waheshimu mikataba kulinda vipaji

KATIKA msimu huu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara, tumeshuhudia wachezaji wengi wakihama timu moja na kujiunga na nyingine.

Wapo wachezaji waliomaliza mikataba yao kwenye klabu walizotoka na kuamua kutoongeza, ili kuweza kupata nafasi ya kujiunga na timu nyingine.

Kimsingi katika kipindi kama hiki kilichomalizika cha usajili, ndicho cha mavuno kwa wachezaji kwa kujiingizia mamilioni ya pesa pale wanaposaini mikataba mipya kwenye timu zao au wanazohamia.

Mfano ni kiungo raia wa Rwanda, Haruna Niyonzima, na mshambuliaji mzawa, Ibrahim Ajibu baada ya kumaliza mikataba yao kwenye timu zao hawakuongeza na kuamua kujiunga na timu nyingine.

Kisheria inawezekana na inakubalika mchezaji kuachana na timu moja na kuijiunga na timu nyingine, ili mradi tu asivunje kanuni ama taratibu zilizopo katika mkataba wake wa awali.

Nipashe tunaamini kuna haja ya wachezaji wetu sasa kuheshimu mikataba yao wanayoingia na timu zao, kwa mfano tayari tumesikia kiungo wa Mbao FC, Pius Buswita akifungiwa kwa kosa la kujisajili klabu mbili tofauti.

Na tayari Shirikisho la Soka nchini (TFF), limechukua hatua kwa kumfungia kucheza soka kwa kipindi cha mwaka mmoja kutokana na kosa hilo, hatua ambayo tunaamini Buswita amevuna alichopanda na alichostahili.

Kusaini mikataba miwili kwenye timu mbili tofauti ni ‘uhuni’ na wala haumnufaishi mchezaji bali unamletea matatizo ambayo yanaepukika.

Ni vyema sasa yale yaliyomkuta Buswita anayetuhumiwa kwa kusaini timu mbili za Simba na Yanga, iwe fundisho kwa wachezaji wengine ambao hawaheshimu mikataba yao.

Mkataba ni makubaliano ya kisheria, na mchezaji anaposaini na timu moja anamaanisha kuingia makubaliano ya kisheria kuitumikia timu husika na anapoenda kinyume na mkataba wake klabu yake inauwezo wa kumshtaki katika vyombo husika.

Dunia ya sasa imebadilika na mambo yanaendeshwa kisasa, wachezaji wetu wanapaswa kubadilika na kufanya mambo kisasa na kuachana na uhuni wa miaka ya zamani.

Buswita alipaswa kujifunza kwa wale waliomtangulia ambao walifanya makosa kama hayo na kile kilichowakuta kutokana na adhabu walizokutana nazo.

Wapo wachezaji kwa makosa kama hayo walijikuta wakifungiwa au kulipishwa mamilioni ya pesa, Athuman Idd ‘Chuji’ alikaa nje kwa mwaka mzima baada ya kudaiwa kusaini mikataba kwenye timu mbili tofauti.

Ni vyema sasa kwa wachezaji wetu wakaheshimu mikataba yao na kama wanataka kuivunja basi wanapaswa kufuata taratibu zilizowekwa ili kuepuka migogoro inayoweza kuwaingiza kwenye adhabu.

Soka ni ajira na wanasoka wanatajirika kupitia mchezo huu, hivyo ni vema wachezaji kutambua umuhimu wa kuheshimu ajira zao kwa kuepuka tamaa zinazoweza zikawafanya kufungiwa.

Hili lililomtokea Buswita, liwe fundisho kwa wachezaji wengine kuchukulia kama somo kwao kwa kuhakikisha hawaingii kwenye migogoro kama hiyo inayoweza kupeperusha vipaji vyao kutokana na kufungiwa kwa muda mrefu.

Tunatambua kama Buswita angekuwa mwaminifu na kusaini timu moja kati ya Simba ama Yanga, angeweza kutangaza kipaji chake kwenye michuano ya kimataifa ambayo timu hizo mbili zinashiriki, hivyo kujitafutia soko nje ya nchi na kupata fedha nyingi zaidi ya hizo kidogo zilizompeleka ‘jela’ ya soka kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Tumeona wachezaji kama Samatta na Msuvu, wote vipaji vyao vilioneka ama wakati wakizichezea klabu zao au timu ya Taifa, Taifa Stars, jambo ambalo kwa Buswita fursa hiyo ameipeperusha kwa sasa kutokana na tamaa zisizo na maana kwa mustakabali wa afya ya soka lake.

Habari Kubwa