Wachezaji waisome na kuielewa mikataba ya usajili msimu ujao

23May 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Wachezaji waisome na kuielewa mikataba ya usajili msimu ujao

LIGI Kuu Bara imefikia tamati jana kwa timu zote kushuka dimbani baada ya kuchezwa takribani kwa miezi minane. Tunachukua nafasi hii kuipongeza Yanga kwa kutwaa ubingwa msimu wa pili mfululizo.

Kama kawaida, ligi inapomalizika timu huanza kujipanga kwa ajili ya usajili wa wachezaji ili kujiweka vizuri msimu unaofuata wa ligi.

Uzoefu unaonyesha kuwa kwa miaka ya karibuni, hakuna kipindi cha usajili kilichowahi kupita bila kuwapo na malalamiko kutoka klabu au wachezaji wenyewe.

Mara kadhaa klabu zimefikishana mbele ya mamlaka ya usimamizi wa soka nchini (TFF), kuomba suluhu kutokana na migongano katika usajili wa wachezaji.

Lakini pia migongano na malalamiko katika usajili, kumesababisha chuki na mivutano baina ya klabu, wakihusishwa viongozi, wanachama na hata mashabiki.

Hali hii kwa kiasi fulani imekuwa ikichangia kuleta uadui, jambo ambalo ni kinyume na sera za michezo, zinazobainisha kuwa ‘michezo ni furaha’.

Tunachukua nafasi hii kuzikumbusha klabu zote umuhimu wa kuwa makini wakati wa usajili wa wachezaji ili kuepuka kuingia kwenye matatizo.

Tumeshuhudia baadhi ya klabu zikifanya usajili katika mtindo wa zima moto na hii ni kwa sababu kazi hiyo imekuwa ikifanywa na viongozi badala ya benchi la ufundi.

Benchi la ufundi ndilo lenye dhamana ya kupendekeza kwa uongozi aina ya wachezaji wa kusajili kutokana na namna watakavyoona.

Kinachoshangaza katika soka letu ni kwamba, viongozi wamekuwa na nguvu ya kufanya usajili kuliko benchi la ufundi na matokeo yake timu inashindwa kufanya vizuri kwenye mashindano.

Kama wadau wa michezo, tunaona uwapo wa sababu kwa viongozi wa klabi kuacha kazi ya usajili kufanywa na kitengo husika, ambacho mwisho wa siku ndicho hulaumiwa timu inapofanya vibaya kwenye mashindano.

Haina maana klabu kumtimua kocha kutokana na kufanya vibaya timu kwenye mashindano, wakati kocha huyo hakuhusika na usajili mbovu uliofanywa na viongozi.

Tunazishauri klabu kuwa makini katika usajili hasa zile zenye utamaduni wa kupenda kusajili wachezaji wa kigeni.
Klabu zijiridhishe kwa vitendo kama kuna ulazima wa kusajili wachezaji wa kigeni kutokana na ukweli kuwa, baadhi ya wachezaji wa kigeni hawana viwango vya kimataifa.

Ni heri kusajili wachezaji wa ndani wenye viwango kuliko kusajili wachezaji wa kigeni na kuwalipa fedha nyingi wakati uwezo wao ni mdogo kulinganisha na wachezaji wazalendo.

Lakini pia Nipashe, tunatoa angalizo kwa wachezaji kuwa makini na kusoma vizuri mikataba wanayoingia klabu.
Kutokusoma kwa makini mikataba na kuielewa, kunaweza kuwaingiza kwenye matatizo na kukosa hazi zao za msingi kama wachezaji.

Tutokana na wachezaji kutokuwa makini, tumekuwa tukiwashuhudia baadhi yao wakisaini mikataba, lakini baadaye wanaingia katika migogoro na klabu na mwishowe kujikuta wakikosa haki zao za msingi.

Hata hivyo wako wachezaji wchache makini, ambao tumewashuhudia wakilipwa haki zao na klabu kutokana na kwenda kuzidai katika mamlaka husika za soka baada ya kuingia kwenye migogoro na viongozi wa klabu husika.

Tunaamini, kama wachezaji na klabu, kwa maana ya viongozi watakuwa makini katika usajili msimu ujao, hapana shaka malalamiko hayatakuwapo.

Habari Kubwa