Wadaiwa NHC dawa ni kulipa

13Feb 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Wadaiwa NHC dawa ni kulipa

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, ameiagiza Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuhakikisha waliohama kwenye nyumba za shirika hilo na kuacha madeni wanalipa fedha hizo kabla ya Juni mwaka huu.

Taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa wapangaji waliohama bila kulipa wanadaiwa Sh. bilioni 4.353, wakati wapangaji waliopo wanadaiwa kiasi cha Sh. bilioni 1.286, hivyo kufanya deni lote lifikie Sh. bilioni 5.641.

Majaliwa ameitaka bodi hiyo kuwaandikia barua wapangaji wote, ikiwamo baadhi ya taasisi za serikali wanaodaiwa kodi na shirika hilo na wahakikishe zimelipwa ifikapo Mei 30, mwaka huu. Alitoa agizo hilo juzi wakati akizungumza na viongozi na wajumbe wa Bodi ya Shirika jijini Dar es Salaam, huku akitaka wote hao wafuatilie na walipe madeni yao.

Miongoni mwa wapangaji wa nyumba hizo ni taasisi zote za serikali ambazo nazo zimetakiwa zilipe madeni. Ni wazi kuwa agizo hilo la Waziri Mkuu ni kaa la moto kwa viongozi wa taasisi zilizopanga na kuamua kuhama kwenye majengo hayo kabla ya kulipa madeni.

Waziri Mkuu aliweka bayana kuwa chombo chochote cha serikali kinaishi na bajeti, kwa hiyo hata kama wamejenga ya kwao, walipaswa walipe madeni ya pango kabla hawajahama.

Tunaunga mkono hatua hii ya agizo la Waziri Mkuu kwa kuwa linalenga kuhakikisha matumizi mazuri ya fedha za umma na kuondoa mianya ya kuikosesha mapato serikali, uzembe na uwajibikaji.

Katika kuonyesha kuwa hataki ujanja ujanja katika jambo hilo Waziri Mkuu aliagiza apatiwe orodha ya taasisi za serikali zinazodaiwa ili azifuatilie mwenyewe. Aliahidi kuwa atawaita wakuu wa taasisi hizo mmoja mmoja ili apate mrejesho kuhusu madeni hayo.

Waziri Mkuu alitaja madeni ambayo taasisi za serikali zinadaiwa yanafikia Sh. bilioni 4.3, ambazo kama zitalipwa, zitalisaidia shirika kuendelea na mpango wake wa ujenzi wa nyumba nafuu kwenye maeneo mbalimbali.

Hatua ya Majaliwa ni mwendelezo wa jitihada za serikali kuwataka wadaiwa wote sugu wa shirika hilo kulipa madeni yao. Kwa mfano, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, ameshawatangazia wapangaji wote na kuwapa notisi kuwa wataondolewa kwa nguvu katika nyumba hizo. Shirika pia limeshatoa notisi kama hiyo kupitia vyombo vya habari.

Wadaiwa hao kwa hakika wanapaswa kubanwa kulipa madeni yao, kwa kuwa kuchelewa ama kukwepa kulipa ni kuminya hatua za maendeleo zinazopaswa kufikiwa na shirika hilo na kunufaisha serikali na jamii kwa ujumla.

Miongoni mwa mambo ambayo shirika hilo linatakiwa lijikite nalo ni pamoja na ujenzi wa nyumba bora na za bei nafuu, kwa sababu mahitaji ya nyumba nchini bado ni makubwa. Aliyoagiza Majaliwa yakitelekezwa, yatasaidia wananchi wa kipato cha chini kumudu na kunufaika na uwapo wa shirika hilo, hivyo kuonyesha maana halishi ya kuwapo kwa shirika hilo.

Viongozi wa NHC wanapaswa kuchukua hatua kadhaa ili kulifanya shirika kujiendesha na kutoa huduma bora kwa wateja na taifa kwa ujumla, zikiwamo kuimarisha mfumo wa ukusanyaji wa mapato kwa kuhakikisha kodi zinakusanywa kwa njia ya kielektroniki.

Utaratibu wa kuruhusu maofisa kwenda nyumba kwa nyumba na kudai Sh. 500,000 kwa risiti za kuandika unatia shaka na kutoa mwanya wa kufanyika udanganyifu.

Pia utaratibu huo unazua maswali kwa nini NHC linajichelewesha katika kutumia control number, ili mwananchi kulipia kwa simu au benki ili fedha ziingie moja kwa moja katika shirika kama inavyofanywa na mashirika kadhaa ya umma yakiwamo Tanesco, Dawasa kwa kutaka baadhi.

Habari Kubwa