Wadau kodi anzeni kushirikiana na TRA

11Jan 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Wadau kodi anzeni kushirikiana na TRA

MAMLAKA ya Mapato (TRA), imeonyesha ukomavu wa kiutendaji kwa kuamua kuwa kuanzia sasa itakutana na wateja kila Alhamisi kusikiliza hoja, dukuduku, kero na mapendekezo yao ili kuwa na uhusiano wa kimaridhiano.

Kwa ujumla huu tunauona kama ni ukomavu, kwa kuwa kupitia mazungumzo TRA itazitambua changamoto ili kuzitatua na kumaliza sintofahamu zinazowakwaza wateja au walipa kodi nchini.

Sintofahamu za ulipaji kodi zinaweza kuwa hali ya kutokubaliana baina ya walipaji na wasimamizi au TRA na kusababisha mteja kutoridhika na hata kususa.

Kwa ujumla tunayaona mazungumzo baina ya TRA na wateja wake ni barabara ya kuifikisha serikali kwenye mafanikio, kwa kuwa ndiyo njia inayoweza kuongeza mapato na makusanyo zaidi.

Aidha, ni suala lenye tija kwa wote wawe wafanyabiashara na walipa kodi wengine wakiwamo wafanyakazi kuzungumzia kilio na kero zao.

Wafanyakazi wana kilio cha siku nyingi cha punguzo ya kodi ya mshahara (PAYE), ambayo watumishi mara nyingi wamekuwa wakitoa ya moyo kuwa ni kubwa ipunguzwe kwa kuwa kiwango cha chini ni asilimia 10 ambacho wengi hukiona kinawaumiza, hata hivyo hufanya hivyo mara nyingi kwenye sikukuu ya Mei Mosi.

Mikutano ni fursa yao pia kutoa ya moyoni kupitia wawakilishi wa vyama vya kuwatetea na kusimamia maslahi yao.
Uzoefu unaonyesha kuwa eneo jingine linalowakwaza walipa kodi ni suala la marejesho ya kodi ambalo kwa muda mrefu wafanyabiashara hasa walioagiza sukari ya viwandani wamelilalamikia mno.

Tunaamini kuwa kupitia mikutano hiyo baina ya viongozi, watendaji na wateja changamoto hizo zitatatuliwa kuepuka kufunga biashara au kuzifanya kwa njia za kuikosesha serikali mapato.

Kwa ujumla mijadala hiyo itawapa darasa wateja, TRA pia itajulishwa kuhusu upungufu wake na namna ambavyo inaweza kurekebisha taratibu kumvuta zaidi mlipa kodi.

Tunategemea kuwa katika kujadiliana baina ya TRA na wateja itakuwa fursa kwa walipakodi kufahamishwa kuhusu rufani za kodi, kuelezwa ni wakati gani zinazotokea.

Ni imani yetu kuwa yote hayo yanalenga kuwa vuta karibu wateja na kuwaeleza kuwa wasiporidhika si kufunga biashara zao, kisha, waelimishwe kama ndiyo wakati mteja asiporidhika na makadirio anayopewa aende wapi kupeleka rufani ya kodi.

Ndiyo fursa kwa wateja kuelezwa kuhusu rufani za kodi, wakati gani wa kufikisha malalamiko kwa Kamishna Mkuu wa TRA ni muda gani wa kukutana na Waziri wa Fedha na masuala yote na ngazi wanazoweza kupitia ili kufikia mwafaka.

Kwa mujibu wa sheria zilizopo mojawapo ni pamoja na mteja kufanyiwa makisio ya kodi. Hili ni moja ya eneo ambalo wateja wengine wanakataa au kutoridhika, huenda baadhi wakafikia kufanya maamuzi ya hasira hatua ambayo haina tija kwa serikali wala kwa mlipa kodi.

Tunashauri kuwa katika mikutano hiyo ndiyo wakati wa mamlaka za juu kamishna mkuu wa TRA, makamishna wengine pamoja na kitengo cha elimu ya walipa kodi, hata Waziri wa Fedha kukutana na wafanyabiashara na wafanyakazi wanaolipa PAYE kuweka mipango na mikakati.

Tunaamini kuwa mitafaruku ya kodi si jambo la mtu na ofisa wa TRA, bali ni migogoro kati ya mtu na serikali yake kwa kuwa kodi ni mali ya serikali na kila raia ana haki na wajibu wa kulipa kodi kwa serikali ili kuleta maendeleo ya nchi hii.

Habari Kubwa