Wafanyabiashara usafirishaji binadamu wakomeshwe

01Aug 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Wafanyabiashara usafirishaji binadamu wakomeshwe

MAPEMA wiki hii serikali ilitoa taarifa ya kuwapo kwa baadhi ya watu wanaofanya biashara ya kusafirisha binadamu kwa kuchukua watoto wenye ulemavu na kuwapeleka nje ya nchi kuwa ombaomba.

Taarifa hiyo ilitolewa katika maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Kupinga Biashara Haramu ya Usafirishaji Binadamu, iliyofanyika juzi.

Serikali imeonya wanaofanya biashara hiyo haramu, mwisho wao umefika na kuwataka watafute shughuli nyingine.

Takwimu zilizotolewa katika maadhimisho hayo zimeonyesha kuwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2016, wadau wameokoa jumla ya waathirika 390. Kati yao wanawake ni 373 na 320 walikuwa chini ya umri wa miaka 18.

Biashara ya usafirishaji binadamu imeshamiri duniani na walengwa wakubwa ni wasichana na watoto ambao hudanganywa kwenda nje ya nchi kutafutiwa ajira, lakini kinyume chake wamekuwa wakipata mateso makubwa na wengine huishia kutumikishwa kingono.

Wengine hupata mateso ya kupigwa na kunyimwa chakula na baadhi yao hupoteza maisha.

Kuibuka kwa biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu dhidi ya watu wenye ulemavu wa miguu kwa ajili ya kuwatumikisha kama ombaomba kwenye mitaa yenye mkusanyiko wa watu au barabara zenye foleni, ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.

Kibaya zaidi wanaondolewa kwenye nchi yao na kupelekwa nchi ya kigeni ambayo hata kupata msaada ni vigumu.

Watu hao wanahitaji kusaidiwa sio kutumikishwa kwa kukaa barabarani na kupigwa jua kuanzia asubuhi mpaka jua linapozama, pengine bila kupata chakula.

Ni jambo linalotia faraja baada ya serikali kugundua watu wanaofanya biashara hiyo na kufanya mawasiliano na mamlaka za Kenya ili kuwarejesha watoto watatu wa Kitanzania waliookolewa nchini humo wakiwa wanatumikishwa kama ombaomba, wawili kati yao wakiwa na ulemavu.

Serikali imeonya mtu yeyote atakayemchukua mtoto au kumdanganya na kumfanya mtumwa ama wa kumbebea dawa za kulevya, kuuza pombe, kufanya uhalifu mwingine wowote pamoja na danguro, kuacha mara moja.

Imegundulika pia kuwa baadhi ya watu huwachukua binadamu wenzao na kwenda kuwatumikisha kwenye mashamba, viwandani na wengine nyumbani.

Kwa Tanzania mikoa iliyotajwa kuongoza kwa utumikishaji wa biashara hiyo kuwa ni Dar es Salaam, Mwanza, Kigoma, Geita, Dodoma, Singida, Shinyanga, Tanga na Morogoro.

Katika kipindi cha miaka minne kuanzia mwaka 2016, Jeshi la Polisi lilifanya upelelezi wa matukio 50 ya aina hiyo dhidi ya watuhumiwa 76 na 60 walipatikana na hatia na kuhukumiwa kulipa faini au kutumikia kifungo. Kati ya hao wanawake ni saba.

Waathirika wa biashara haramu ya binadamu wengi ni wanawake wenye umri kati ya miaka 16 hadi 26 ambao hupelekwa nchi za India, Thailand, China, Indonesia na Malaysia kwa ajili ya kutumikishwa  ukahaba.

Wanaopelekwa kutumikishwa kazi za ndani hupelekwa nchi za Oman na baadhi  Uarabuni ikiwamo Irak.

Kamati ya Kitaifa ya Kupambana na Biashara imesema mwaka 2018/19, wahalifu waliokamatwa ni 36, kesi zilizofikishwa mahakamani ni 33, waathirika waliookolewa ni 147. Kati yao 141 walikamatwa Tanzania na sita nje ya nchi.

Wananchi wanatakiwa kutoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama kila kunapokuwa na kiashiria cha biashara hiyo ili kuondoa tatizo hilo nchini.

Habari Kubwa