Wafanyabiashara wajenge utamaduni wa kukata bima

30Jul 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Wafanyabiashara wajenge utamaduni wa kukata bima

WAFANYABIASHARA 12 waliokata bima mbalimbali, kati ya waliounguliwa moto maduka yao katika Soko la Kariakoo, Dar es Salaam, wamelipwa bima ya Sh. milioni 438.4.

Benki ya NMB kupitia Kampuni ya Reliance Insurance, imetoa malipo kwa waathirika hao wa tukio la Julai 10, mwaka huu, huku wakikiri kuwa hasara na maumivu yao ya kuunguliwa yamepozwa na malipo hayo ya haraka ya bima.

Kitendo chao kukiri kupozwa machungu yao na bima, sisi tunakichukulia kama chachu ya wao kuhamisisha wafanyabiashara wenzao kujenga utamaduni wa kukata bima za biashara, ili itapotokea ajali kama ya Kariakoo, wawe na pa kukimbilia.

Ikumbukwe kwamba kumekuwapo na kasi ya matukio ya kuungua moto masoko na maduka makubwa sehemu mbalimbali nchini, hali ambayo tunaona kuwa inatosha kuwashtua wafanyabiashara kuchukua hatua ya kukata bima.

Wafanyabiashara wamekuwa wakihamasishwa kukinga biashara zao dhidi ya hasara zitokanazo na majanga ya moto, wizi, uharibifu wa mali au akiba, majeraha kwa wafanyakazi au matatizo mengine yoyote.

Tulichukulia tukio la moto sokoni Kariakoo na jinsi ambavyo baadhi ya wafanyabiashara wamelipwa kiasi hicho cha fedha kama fursa ya kuwafanya wenzao wasio na bima kutambua umuhimu wa kuwa nayo.

Hivyo tunachukua nafasi hii kuwakumbusha wafanyabiashara wote kuwa tukio la moto Kariakoo ni nafasi ya kujifunza na kuchukua hatua ambazo zitawasaidia kufidiwa mali zao pale majanga yakiwamo ya moto yanapotokea.

Jambo la kusikitisha ni kwamba watu wengi katika jamii yetu hawana uelewa kuhusu faida ya kuwa na bima ama wanakaidi tu, hivyo ni suala ambalo linahitaji kutolewa elimu zaidi, kususan kwa wafanyabiashara ili wawe na uelewa wa kuwa na bima.

Kufidiwa kunakuja pale mhusika anapokuwa amekata bima tu, vinginevyo inakuwa ni vilio kwa wale watakaonguliwa mali zao bila kuwa na bima ambayo angalau ungesaidia kupoza machungu.

Kwa maneno mengine, tunaweza kusema kuwa, kujihadhari na majanga ni kukata bima, kwani mali zinaweza kuteketea kwa moto, lakini mhusika anaweza kufidiwa kuliko kubaki mtupu.  

Mara kwa mara jamii imekuwa ikikumbushwa kuwa bima sio kwa ajili ya pesa za mikopo, bali zipo za moto, magari, nyumba, afya, mali na nyinginezo, tunaona sasa ni wakati mwafaka wa kuchukua hatua.

Tunashauri hivyo, kwa sababu ya kuwapo kwa majanga ya moto maeneo mbalimbali nchini kuanzia katika masoko na maduka makubwa, ambapo mali za watu huteketea na wao kubaki bila kitu na matokeo yake unakuwa mwisho wa biashara zao ama kulazimika kuanza upya.

Kwa tukio la Kariakoo ambalo bado halijasahaulika vichwani mwa wakazi wa Dar es Salaam, tunaliona kama sehemu ya watu kujifunza kuchukua hatua, hasa kutokana na baadhi ya wafanyabiashara kufidiwa.

Kauli za baadhi ya waliolipwa bima kwamba wamefutwa machozi zinadhihirisha kwamba pamoja na hasara waliyopata, lakini baada ya kulipwa fidia wamepata ujasiri na kujiamini katika kuendelea kufanya biashara zao.

Watu katika biashara, kuna tofautia kubwa ya mitaji, lakini inapotokea mtu amewekeza fedha nyingi katika biashara fulani bila kuwa na bima, tunaona kama anateketeza mali yake mwenyewe.

Tunaendelea kukumbusha wafanyabiashara kuwa, tukio la Kariakoo na jinsi baadhi yao walivyolipwa bima ni funzo kwa wengine ambao hawana bima kwa kutambua kuwa majanga hayabishi hodi.

Habari Kubwa