Wafungwa waliosamehewa waangaliwe wasikengeuke

13Dec 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Wafungwa waliosamehewa waangaliwe wasikengeuke

MSAMAHA kwa wafungwa takribani 5,533 uliotolewa na Rais John Magufuli, kwenye sikukuu ya Uhuru wa Tanzania mapema wiki hii, bila shaka umeleta faraja na amani kwao na familia zao.

Mojawapo ya vigezo vya msamaha ni pamoja na kuwasaidia wale wanaoelekea kumaliza vifungo na kuwahurumia wagonjwa wakiwamo wenye maradhi sugu.

Utaratibu wa kusamehe unaonyesha heshima na kuthamini utu wa watu kwa kuwarejeshea uhuru wao ili kujenga maisha kama walivyo raia wengine waliohuru mitaani.

Pamoja na nia njema kuna taarifa kuwa baadhi ya wafungwa wameanza kutumia vibaya heshima kwa kurudia mienendo ya kihalifu iliyowaingiza jela.

Tunasema hivyo kwa sababu zipo taarifa kuwa mfungwa aliyesamehewa Jumatatu wiki hii, anadaiwa kuvunja, kuiba na kushambuliwa na raia.

Mtuhumiwa huyo kutoka Gereza la Makambako mkoani Njombe, anaripotiwa na polisi kuwa alivunja nyumba ya wageni na kutaka kuiba fedha licha ya kwamba alisamehewa kwa kosa linalifanana na hilo lakini bila kuchelea analolirudia tena.

Matendo hayo ya baadhi ya wafungwa hawa wanaonyesha kuwa pengine wangehitaji kwanza maandalizi ya kuingia mitaani na kuishi maisha ya uraiani baada ya kutoka vifungoni.

Ndiyo maana tunasema pengine kuna haja ya kuwafanyia wafungwa utaratibu wa mafunzo na maandalizi ya kuishi mitaani ili wanapotokana wasirudie uhalifu.

Mtuhumiwa huyo anadaia kuwa hana uhusiano mzuri na jamaa zake ndiyo sababu ya kuzurura na kuingia mitaani na hata kuvunja na kuiba.

Ni wakati wa kutizama iwapo msamaha unaweza kuangalia kama mfungwa anayesamehewa ana makazi, ndugu na msaada wa kumwezesha kuanza tena maisha upya.

Tunashauri pia kuwa kabla ya kuwaachia wafungwa ni vyema kuwapa hamasa za namna ya kuanza tena maisha kwa kuwa wanapoondoka magerezani wapo ambao hawana chochote cha kuanzia maisha wala makazi ya kwenda kufikia.

Tunaona kuwa maofisa ustawi wa jamii na wanaotoa ushauri nasaha wana jukumu la kuwapa ushauri Watanzania hawa ili wanapotoka magerezani wawe wameiva na kujitayarisha kwenye maisha mapya na kuepusha wasianguke tena kwenye uhalifu.

Tunashauri kuwa ni vyema wakafunzwa hata ujasiriamali na uwekezaji ili iwe rahisi kuanza maisha na kujichanganya badala ya kubaki kujilaumu na kurejea kwenye uhalifu wa awali uliowapeleka gerezani.

Tunazipongeza juhudi zilizofanywa na viongozi wa mkoa wa Katavi katika kuwahudumia wafungwa ambao wamepatiwa hekari 370 ziwasaidie kwa kilimo.

Wafungwa hao 74 wakiwamo 43 kutoka Gereza la Mpanda na 31 kutoka Kalinankulukulu wamepata hekari tano kila mmoja ili waanze maisha baada ya kurejea uraiani.

Licha ya mpango huo mwema ni wazi kuwa wafungwa hao watahitaji pembejeo-mbegu, mbolea na dawa za kuua wadudu.

Kilichofanyika Katavi ni mfano wa kuigwa lakini tunaona kuwa ni vyema kwenda mbele zaidi kwa kuwasaidia wafungwa kwa vitendea kazi na pembejeo ili kufanikisha lengo la kuwasaidia kuchangamana na jamii za uraiani.

Wapo baadhi ya wafungwa ni wazee au wagonjwa huenda inakuwa vigumu kumudu maisha yao. Kadhalika nao pia wanahitaji kufanyiwa maandalizi na hata kupatiwa msaada wa tiba kwa vile hali zao zinafahamika.

Ni vyema pia wafungwa hao wanaoachiwa huru wakafuatiliwa kwa karibu ili kujua mienendo yao kwa vile wapo baadhi ambao hawaachi uhalifu.

Pengine ni vyema kuandaa mkakati wa kuwahusisha viongozi wa mtaa mijini, vijijini na kwenye vitongoji pamoja na polisi na polisi jamii ili kufuatilia na kuzijua hatua anazopitia mfungwa huyo na shughuli anazofanya ili iwe rahisi kumsaidia kujipanga upya au kumuonya pale anapokengeuka.

Habari Kubwa