Wahusika kashfa watumishi hewa sasa washughulikiwe

26Jun 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Wahusika kashfa watumishi hewa sasa washughulikiwe

MIONGONI mwa matukio yaliyotikisa nchini katika miezi ya hivi karibuni ni kufichuka kwa kashfa ya kuwapo kwa utitiri wa watumishi hewa.

Taarifa kuhusiana na kadhia hii zimetwaa nafasi kubwa katika mijadala ya Watanzania walio wengi.

Hali imekuwa hivyo pia katika vyombo mbalimbali vya habari, hasa baada ya Rais John Magufuli kuvalia njuga suala hilo.

Hadi kufikia sasa, viongozi kadhaa wameshachukuliwa hatua kuhusiana na kashfa hiyo.

Hakika, hii ni hatua muhimu katika kuhakikisha kuwa rasilimali fedha haipotei kiholela kupitia mikononi mwa watu wasiokuwa waaminifu.

Nipashe tunaendelea kuunga mkono hatua zote zinazohusiana na udhibiti wa vitendo hivyo ambavyo kwa namna yoyote ile, havistahili kuvumiliwa hata kidogo.

Ni kwa sababu mabilioni ya fedha za walipa kodi hupotea kwa kuangukia mikononi mwa wachache wasiokuwa na huruma hata chembe kwa taifa lao changa kiuchumi.

Na uhalifu huo ambao huambatana na mishahara hewa unafanyika wakati taifa likikabiliwa na changamoto mbalimbali zinazohitaji fedha ili kutatuliwa, zikiwamo za kukosekana kwa huduma muhimu za kijamii kama maji safi na salama ya kunywa.

Hata hivyo, lipo jambo moja ambalo sisi tunadhani kwamba bado halijafanyika kwa kasi inayostahili. Ni kwamba, licha ya jitihada nzuri zilizofanywa za kufanya uhakiki wa kina katika kila mkoa ili kubaini watumishi hewa, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Magufuli, hatua za kukamilisha uchunguzi nchi nzima na kuwafikisha wahusika mbele ya mkono wa sheria bado hazijawa na kasi ile iliyoonyeshwa na timu ya uhakiki.

Mwishoni mwa wiki, wakati akihutubia katika madhimisho ya Wiki ya Watumishi wa Umma, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, alisema hakuna mtumishi atakayeachwa bila kuchukuliwa hatua iwapo itathibitika kuwa ameshiriki katika udanganyifu wowote ule kuhusiana na kashfa hiyo.

Sisi tunaunga mkono kauli hiyo, huku tukiamini kuwa ni kupitia hatua ya kuwapeleka wahusika kortini ndipo vitendo vya aina hiyo vitapungua au kumalizika kabisa.

Kwamba, uchunguzi mkali na wa haraka ufanyike na kila aliyehusika akamatwe na kufikishwa mahakamani ili sheria itwae mkondo wake.

Inatia moyo kusikia kutoka kwa katibu wa watumishi kuwa hakuna atakayesalimika ikiwa amejihusisha na kashfa hiyo. Hata hivyo, tunadhani kwamba sasa iko haja ya kuongeza kasi hiyo ya kuwabaini na kuwanasa wahusika ili wakapatiwe haki yao kortini.

Sisi tunasisitiza hilo kutokana na kile tunachoamini kuwa vitendo hivyo ni zaidi ya jinai ya kawaida. Ni uhujumu uchumi, ni ufisadi usistahili kuachwa bure bure.

Badala yake, jitihada ziongezwe katika kuhakikisha kwamba wahusika wanapatikana haraka iwezekanavyo na kufikishwa kortini kwa hatua zaidi za kisheria.

Ni matumaini yetu kuwa vyombo vya uchunguzi vitaongeza kasi katika kuwafuatilia wahusika kokote waliko, bila kujali majina yao na vyeo walivyokuwa au wanavyoendelea kushikilia.

Kwa kufanya hivyo, ni imani yetu kuwa jitihada za Rais Magufuli katika kupiga vita vitendo viovu kama vya kuwapo kwa watumishi hewa wanaolipwa mabilioni ya fedha kila mwezi kupitia mishahara zitakuwa zimepata uungwaji mkono wa kweli.

Aidha, ikumbukwe kuwa Watanzania wengi ambao huvuja jasho kila uchao ili kulipa kodi na kuiwezesha Serikali kutimiza majukumu yake watakuwa wamepata faraja kusikia kuwa wahujumu wa fedha za umma kupitia watumishi hewa wanachukuliwa hatua.

Shime, kasi ya uchunguzi iongezwe ili wahusika wote wa kashfa hiyo ya kuwapo kwa watumishi hewa na mishahara hewa wafikishwe mahakamani.

Habari Kubwa