Wakati mwafaka wakazi Dar kuondolewa maeneo hatarishi

09Nov 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Wakati mwafaka wakazi Dar kuondolewa maeneo hatarishi

TUME ya Sayansi na Teknolojia (Costech), imebaini maeneo hatarishi kwa kuishi katika kata 29 jijini Dar es Salaam, na kupendekeza serikali iwahamishe wakazi wa maeneo hayo kuepusha majanga yanayoweza kutokea.

Costech kwa kushirikiana na wataalamu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU) kupitia mradi wa ‘Ramani Huria’, imeainisha maeneo hayo ambayo yamekuwa yakisababisha adha kubwa kwa wakazi wake.

Tume hiyo imebaini maeneo hayo ambayo mengi ni ya mabondeni, yameorodheshwa na kuonekana kuwa hatarishi kutokana na kugharimu maisha ya wakazi na kuwa chanzo cha magonjwa ya milipuko kikiwamo kipindupindu.

Kipindupindu kushindwa kudhibitiwa Dar es Salaam huku waathirika wengi wakiwa ni wakazi wa maeneo hatarishi.

Msimamizi Mkuu wa mradi huo, Innocent Maholi, alisema utafiti huo umegundua kuwa katika wilaya za Temeke, Kinondoni na Ilala kuna maeneo mengi ambayo ni hatarishi kwa kuishi, na kushauri serikali ichukue hatua kwa kuwahamisha wakazi wa maeneo hayo.

Ramani hiyo inaonyesha maeneo ya mabondeni likiwamo Bonde la Msimbazi na maeneo ya Tandale ambayo yamejengewa mitaro inayojaa na kusababisha maji mengi kuingia katika nyumba za wakazi hao na kuwa kero kwa wakazi.

Mbali na Kata ya Tandale, maeneo mengine hatarishi yaliyoorodheshwa ni ya kata za Mzimuni, Kigogo, Vingunguti, Ndugumbi, Mburahati, Mabibo, Magomeni na maeneo yote yaliyopitiwa na Mto Msimbazi.

Kwa miaka kadhaa wakazi wa maeneo hatarishi jijini Dar es Salaam wamekuwa wakiaswa kuondoka katika maeneo hayo ili kuepukana na athari kadhaa yakiwamo mafuriko, lakini wamekuwa wakikaidi.

Sababu kubwa ambayo wamekuwa wanaitoa ni kutokuwa na mahali pa kwenda kutokana na kutokuwa na uwezo wa kununua viwanja.

Hata hivyo, sababu hiyo haina ukweli kwa kuwa hata pale walipopewa viwanja na serikali hawakuwa tayari kuhamia. Kwa mfano, athari za mvua za mwaka 2011 zilizoua watu zaidi ya 40 na kuwaacha wengine takribani 5,000 bila makazi, ziliifanya serikali kutoa viwanja kwa waathirika katika eneo la Mabwepande, wilayani Kinondoni.

Kilichoshangaza ni kuwa wengi waliviuza viwanja vyao kwa bei ya kutupwa na kurejea katika maeneo yao ya awali likiwamo la Jangwani na baadhi wanaendelea kuishi hapo hadi leo.

Yako maeneo mengine hatarishi ambayo wakazi wake wanaendelea kung’ang’ania kuishi huku wakiwa wameweka zuio mahakamani kupinga kuondolewa kwa nguvu na mamlaka husika hususani halmashauri.

Kutokana na taarifa za utafiti wa Costech, tunaona kuwa hakuna sababu za serikali kuendelea kuwavumilia wakazi wakaidi wa maeneo hatarishi, badala yake wapewe muda ili waondoke kwa hiyari yao na baada ya hapo waondolewe kwa nguvu. Ifike mahali watu waheshimu na kufuata sheria na maelekezo ya serikali.
Tunaunga mkono pendekezo la Costech la kuwaondoa wakazi wote katika maeneo yote hatarishi jijini Dar es Salaam kwa kuwa lengo lake ni kwa manufaa yao.

Tunashauri kwamba mamlaka za serikali zikiwamo halmashauri kuweka alama za kudumu katika maeneo yote hatarishi na kueleza wazi kuwa hakuna ruhusa ya kujenga, na watakaojaribu kujenga majengo yao yabomolewe katika hatua za awali ili liwe fundisho kwa wengine.

Habari Kubwa