Wakulima limeni mazao yanayostahimili ukame

11Jan 2017
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Wakulima limeni mazao yanayostahimili ukame

MVUA za mwaka huu zilizoanza kunyesha tangu mapema ya Novemba, mwaka jana katika baadhi ya mikoa, zimekuwa za shaka kiasi cha kutishia hali ya chakula mwaka huu.

Kwa kawaida, katika baadhi ya maeneo nchini Tanzania, hupata mvua vipindi viwili kwa msimu mmoja yaani mvua za vuli na mvua za masika huku maeneo mengine yakipata mvua kwa kipindi kimoja kwa msimu.

Baadhi ya mikoa ambayo hupata mvua za vipindi viwili yaani vuli na masika ni karibu yote ya pwani na baadhi ya mikoa ya Kanda ya Ziwa ikiwamo Kagera, Mara na sehemu kadhaa za Mkoa wa Mwanza.

Hali kadhalika, visiwa vya Pemba na Unguja, hupata mvua za vuli.

Mikoa mingine iliyobaki hutegemea mvua za masika ambazo hunyesha kwa kipindi kimoja tu kati ya Novemba na Machi.

Hata hivyo, zipo taarifa kwamba mikoa mingi ambayo hutegemea kupata mvua za vuli, zilipata mvua za chini ya wastani huku mingine kutoambulia chochote.

Aidha, mikoa inayotegemea mvua za masika, mingi hivi sasa inapata mvua za chini ya wastani.

Hali hii inaashiria kwamba msimu huu kutakuwa na uhaba wa chakula hasa kwa mazao yanayotegemea mvua za kutosha.

Ni kwa mantiki hii, tunaona upo umuhimu wa kuwashauri wakulima katika mikoa yote ambayo mpaka sasa inaendelea kupata mvua za chini ya wastani, kulima mazao yanayostahimili ukame ili kuchukua tahadhari ya baa la njaa.

Baadhi ya mazao yanayostahimili ukame ni muhogo, mtama, uwele na viazi.

Tunafahamu kwamba wakulima wengi hulima kilimo cha mazoea, kwa mfano; maeneo wanayolima mahindi ama mpunga, ni vugumu kubadilika na kulima mazao ya aina nyingine ukiwamo mtama na muhogo hata kama wanaziona dalili zote za uhaba wa mvua.

Sisi tungependa kuwashauri wakulima kwamba zama za kung'ang'ania kilimo cha aina moja ya mazao, sasa kimepitwa na wakati.
Tunaamini kwamba kilimo chenye tija, ni kile kinachozingatia hali halisi ya mvua kwa msimu husika.

Haitakuwa na maana wakulima wakapoteza nguvu na rasilimali zao kwa kuwekeza katika kilimo cha mazao waliyoyazoea hata kama mvua si za kuridhisha.

Mathalani, zao la muhogo licha ya kutokuwa na thamani kubwa likilinganishwa na mazao mengine, lakini ni mkombozi mkubwa wakati wa njaa.

Inakadiriwa kuwa zaidi ya tani milioni 200 za muhogo huzalishwa duniani kote kila mwaka na pia likiwa ni chakula tegemezi kwa watu zaidi ya milioni 800 kote ulimwenguni.

Tanzania inakadiriwa kuzalisha zaidi ya tani milioni mbili za muhogo kwa mwaka.

Zao la muhogo kwa sasa halipaswi kupuuzwa na kuchukuliwa kama ni chakula kwa watu wa vipato duni, bali lichukuliwe kama chakula bora na chanzo cha pato muhimu kwa wakulima.

Ni muhimu basi zao hili lisionekane kama halina thamani na kukumbukwa wakati wa ukame tu, bali lipewe kipaumbele sawa na mazao mengine kama mahindi ama mpunga.

Tunawahimiza viongozi wa ngazi mbalimbali kilimo cha mazao yanayostahimili ukame iwe kama ajenda kuu kwa wakulima ili kulinusuru Taifa katika baa la njaa.

Ni muhimu kuelewa kwamba adui mkubwa wa maendeleo ni njaa kwani jamii isiyoshiba, haiwezi kufanya kazi za kujiletea maendeleo.

Habari Kubwa