Wakurugenzi wasipige chenga kujibu hoja za CAG

16Jul 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Wakurugenzi wasipige chenga kujibu hoja za CAG

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Everist Ndikilo, amewaka wakurugenzi na wakuu wa idara katika wilaya za mkoa huo kuacha tabia ya kuwakaimisha watumishi kuingia katika mikutano ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Selikari,(CAG) kujibu maswali yanayohusu ofisi zao.

Kauli hiyo ya Ndikilo aliitoa katika kikao maalumu cha Baraza la Madiwani, Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, ambacho kiliandaliwa kwa ajili ya kujibu hoja 32 za nje za CAG.

Hiyo ni kauli nzito ambayo inaonyesha kuwa Mkuu wa mkoa huyu yupo makini, kwa kuwa hayupo tayari kuona uzembe, ujanja ujanja unafanywa na watendaji wake.

Tunasema hivyo, kwa kuwa kumekuwapo na matukio kadhaa ya viongozi wenye dhamana katika halmashauri zetu ambao ni wakurugenzi na wakuu wa idara kukaimisha nafasi zao kwa wasaidizi wao, hivyo wakati mwingine kujikuta wanakwenda kujibu hoja mbalimbali za ukaguzi wa CAG, kuhusiana na matumizi ya fedha za walipakodi.

Hakusita kuwaeleza anachotaka ni kuwa wakuu wa idara na wakurugenzi wajibu mambo wanayoyasimamia badala ya kukwepa au kutioichukulia umuhimu mikutano ya kujibu hoja za CAG.

Ni wazi kwamba kuwa hoja za CAG zinahitaji majibu sahihi yasiyotia shaka, yawezekana pia zimechangia halmashauri kupata hati chafu.

Hati chafu husababisha maswali mengi ikiwamo ofisi husika kuonekana ina watendaji ambao wanadokoa ama ‘wanatafuna’ fedha za umma kama vile mchwa.

Ndikilo kuipongeza Halmashauri ya Wilaya Mkuranga kwa kupata hati safi mara tatu mfululizo, akieleza kuwa hatua hiyo inaonyesha jinsi viongozi husika walivyo na ushirikiano mzuri wa kusimamia fedha za maendeleo kiufasaha.

Alisema halmashauri wilaya zote za mkoa wake zimefanikiwa kupata hati safi hali inaonyesha jinsi ilani ya chama tawala (CCM) inatekelezwa katika kusimamia masuala ya maendeleo.

Tunatambua kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali,Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Ilianzishwa kwa mujibu wa Ibara ya 143 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Madaraka na wajibu wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali yameelezwa kwenye Ibara ya 143 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (iliyorekebishwa 2005) na kufafanuliwa zaidi katika Kifungu cha 10 (1) cha Sheria ya Ukaguzi wa Umma Na.11 ya mwaka 2008.

Dira ya CAG ni Kuwa kituo cha ufanisi katika ukaguzi wa hesabu za serikali na taasisi za umma.Dhamiri Kutoa huduma ya ukaguzi wa hesabu yenye tija ili kuimarisha uwajibikaji na thamani ya fedha katika kukusanya na kutumia rasilimali za umma

Pia imekusudiwa kuimarisha ubora wa utoaji huduma kwa kuchangia ubunifu kwa matumizi bora ya rasilimali za umma, pamoja na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa wadau wetu kuhusu mapungufu katika uendeshaji wa shughuli zao.

Miaka kadhaa tumekuwa tukishuhudia ripoti ya CAG ikiibua madudu yanayofanywa na baadhi ya halmashauri ambayo yamekuwa yakitokana na matumizi mabaya ya fedha za umma.

Tunategemea kwamba wakuu wengine wa mikoa wataungana na Ndikilo katika kuwahimiza wakuu wa idara kwenye halmashauri zao kutambua umuhimu wa kutoa ushirikiano wa kufanikisha ripoti ya CAG.

Kwa kufanya hivyo, itasaidia halmashauri kuwa na maendeleo kwa kuwa kila kiongozi atahakikisha anatumia fedha aliyopewa ya idara iwe kwa ajili ya miradi ya huduma au maendeleo inatumika ipasavyo.

Habari Kubwa