Wakuu wa mikoa wapya sasa wapeni wananchi maendeleo

15Mar 2016
Mhariri
Nipashe
Wakuu wa mikoa wapya sasa wapeni wananchi maendeleo

RAIS John Magufuli, ameendelea na mchakato wa kuunda serikali yake kwa kuteua wakuu wa mikoa.

Juzi, Rais Magufuli aliwateua wakuu wa mikoa 26, kati yao 10 ni wapya huku akiwaacha kadhaa na baadhi yao kuhamishiwa katika vituo vipya vya kazi.

Tunawapongeza wote walioteuliwa kwa kuwa tumaanini kuwa Rais Magufuli amefuatilia na kujiridhisha pasi na shaka kuwa ni waadilifu, weledi na wachapakazi ambao watakwenda sambamba na kasi yake ya utendaji.

Tunasema hivyo kwa kuwa Rais Magufuli kabla ya uteuzi huo alisema wazi kuwa alichelewa kuwateua wakuu wa mikoa na wilaya ili kufuatilia utendaji wao kwanza.

Pamoja na pongezi zetu kwa wateule hao, tunachukua fursa hii kuwakumbusha kwamba wauchukulie uteuzi huo kama ni changamoto kwao. Wajitathmini na wajipange kuhusiana na watakavyowahudumia wananchi kwa kuwaondolea kero mbalimbali pamoja na kuwaletea maendeleo.

Changamoto zinazoikabili nchi yetu kwa sasa ni nyingi na zinajulikana, hivyo ni jumumu la kila mkuu wa mkoa kuhakikisha kwamba anakuwa na mipango na mikakati ya kukabiliana na kero hizo.

Kwa kukumbushia baadhi yake ni kwamba mpango wa elimu bure kwa shule za msingi na sekondari unaotekelezwa na serikali, unakabiliwa na changamoto kadhaa zikiwamo uhaba wa vyumba vya madarasa na madawati.

Ukubwa wa tatizo hilo umetokana na mwitikio mkubwa wa wazazi kuwaandikisha watoto wao kuanza elimu ya msingi kwa kuwa hawatakuwa na mzigo wa kulipia.

Kwa hiyo kila mkuu wa mkoa katika eneo lake la kazi atawajibika kuhakikisha kwamba uhaba wa madawati na vyumba vya madarasa vitanafutiwa ufumbuzi, lakini bila kuwalazimisha wananchi kuchangia.

Maeneo kadhaa ya nchi yanakabiliwa na uhaba wa chakula, hivyo ni jukumu la wakuu wa mikoa kuhakikisha kwamba wanasimamia kilimo na kupanga mikakati ya kuhakikisha kwamba hata kama njaa inatokea kutokana na sababu zilizoko nje ya uwezo wao, basi wasimamie ugawaji wa chakula kinachotolewa na serikali kwa waathirika walengwa.

Halmashauri nyingi nchini zimeshamiri wizi na ubadhirifu wa fedha za umma, hali inayosababisha mara kwa mara kupata hati chafu kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG). Hili litapaswa kuwa jukumu la msingi kwa kila mkuu wa mkoa kuhakikisha anazisimamia halmashauri zote zilizoko mkoani kwake na kudhibiti hali hiyo.

Wilaya nyingi nchini zimekithiri migogoro ya ardhi ambayo imesababisha mapigano ya kila uchao kati ya wakulima na wafugaji katika baadhi ya maeneo kama Mvomero na Kiteto, kwa kutaja baadhi.

Ni wakati mwafaka sasa kwa wakuu wa mikoa kushughulikia migogoro hiyo na kuitatua, na hicho kiwe kigezo cha kupima utendaji wa kila mmoja, ili atakayeshindwa uteuzi wake utenguliwe au ajiweke kando mwenyewe.

Suala hili limeshazungumzwa mara kadhaa na Rais Magufuli, hivyo ni imani yetu kuwa atakuwa ameliweka katika orodha ya majukumu ya wakuu wa mikoa aliowateua mwenyewe.

Hatutazungumzia mambo yote ambayo wakuu wa mikoa wanatakiwa kuyashughulikia, lakini pia hawanabudi kusimamia ukusanyaji wa mapato, kuhakikisha matumizi ya serikali yanadhibitiwa, kusikiliza kero za wananchi na kuzipatia ufumbuzi badala ya kuwaacha wazipeleke katika wizara na Ikulu.

Ni matarajio yetu kuwa kila mkuu wa mkoa aliyeteuliwa anatambua kuwa jukumu lake la msingi ni kuwaletea maendeleo wananchi na watapimwa kwa kigezo hicho.

Habari Kubwa