Wakuu wapya wa wilaya wasifanye kazi kwa mazoea

28Jun 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Wakuu wapya wa wilaya wasifanye kazi kwa mazoea

RAIS John Magufuli juzi alitangaza uteuzi wa wakuu wapya wa wilaya 139.

Katika uteuzi huo, wakuu wa wilaya waliopo sasa ambao wamebaki katika nafasi zao ni 39. Pia aliwateua wakurugenzi wa halmashauri 22 kuwa wakuu wa wilaya kutokana na utendaji wao mzuri.

Aidha, nafasi 78 za uteuzi wa wakuu wa wilaya zimejazwa na Watanzania wengine ambao wameteuliwa kwa mara ya kwanza.

Uteuzi huo ni hatua nyingine ya Rais Magufuli ya kukamilisha uundaji wa serikali yake, baada ya kuwateua mawaziri, makatibu wakuu na wakuu wa mikoa.

Tunawapongeza wote walioteuliwa kushika nafasi hizo na bila shaka Rais Magufuli amewapa fursa hiyo kutokana na kuwamini baada ya kuwapima na kujiridhisha bila kuacha shaka yoyote kwamba wana sifa zinazotakiwa.

Hata hivyo, wanapaswa kufahamu kwamba wanakabiliwa na changamoto nyingi za kuhamasisha, kusimamia shughuli za maendeleo na kuwatatulia wananchi kero mbalimbali.

Serikali hivi sasa imejielekeza katika kuboresha elimu kwa kuhakikisha wanafunzi wa elimu ya msingi na sekondari wanasoma bila kutozwa malipo, hivyo ni jukumu ya wakuu wa wilaya kuhakikisha mpango huo unatekelezwa kama Serikali ilivyoagiza.

Pia, Serikali inatekeleza mpango wa kuhakikisha shule zote nchini zinakuwa na madawati na jukumu hilo wamepewa wakuu wa wilaya na mikoa kulisimamia na ni miongoni mwa vigezo vya utendaji watakavyopimwa.

Kuna kero kadhaa zinazowakabili wanancnhi katika maeneo mengi ambazo wakuu wa wilaya wanawajibika kuzitafutia ufumbuzi.

Migogoro ya ardhi inakumba maeneo mengi na tatizo hilo limesababisha mapigano na watu kadhaa kupoteza maisha kutokana na viongozi wa maeneo hayo wakiwamo wakuu wa wilaya kutoishughulikia na wengine wanalalamikiwa kuwa na maslahi nayo.

Kuongezeka kwa uhalifu katika maeneo kadhaa hususan wilaya za mipakani ni changamoto kwa wakuu wa wilaya wapya kuhakikisha wanaudhibiti.

Aidha, maeneo kadha yamekuwa yakikumbwa na ukosefu wa chakula kutokana na viongozi wenye dhamana wakiwamo wakuu wa wilaya kuhimiza kilimo, hivyo, wakuu wapya wa wilaya hilo litakuwa moja ya vipimo vya utendaji wao.

Moja ya mambo ambayo serikali imeyapa umuhimu mkubwa ni kusimamia na kuweka nidhamu ya matumizi ya fedha za umma pamoja na kuwabaini na kuwaondoa watumishi hewa katika orodha ya malipo ya mishahara.

Kutokana na hali hiyo, wakuu wapya wa wilaya watapaswa kujua kuwa wanawajibika kusimamia uhakiki na kuwaondoa watumishi hewa katika halmashauri zilizoko kwenye maeneo yao sambamba na kudhibiti matumizi mabaya ya fedha katika halmashauri hizo.

Tunawakumbusha wateule hao kwamba wanawajibika pia kulinda heshima ya Serikali katika maeneo yao kwa kufanya kazi kwa bidii, weledi, uaminifu, uadilifu na kushirikiana na walioko chini yao pamoja na wananchi. Hatutarajii kusikia baadhi yao wakigeuka kuwa wababe na kuwaonea wananchi.

Zimekuwapo taarifa kwamba baadhi ya wakuu wa wilaya wamekuwa wakifanya vitendo vya kuishushia heshima Serikali kama ulevi, uzinzi na hata kukopa fedha kwa watu bila kuzirejesha. Tunawapa angalizo kwamba watakaoshindwa kuzingatia hayo, wasije kushangaa uteuzi wao unatenguliwa baada ya kipindi kifupi.

Tunasema hivyo kwa kuwa Rais Magufuli hana suluhu kwa hilo na ameonyesha mfano kwa kutengua uteuzi wa wakuu kadhaa wa mikoa aliowateua hivi karibuni kutokana na kutoridhishwa na utendaji wao.

Kikubwa ni kwamba tunatarajia kuwa wakuu hao wilaya watatekeleza majukumu yao kwa tija na ufanisi kama watakuwa wabunifu badala ya kufanya kazi kwa mazoea.

www.guardian.co.tz/circulation

Habari Kubwa