Walioathiriwa tetemeko la ardhi wasaidiwe haraka

13Sep 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Walioathiriwa tetemeko la ardhi wasaidiwe haraka

TETEMEKO la ardhi lililotokea katika mikoa ya Kanda ya Ziwa Jumamosi iliyopita na kusababisha vifo vya watu 16, 253 kujeruhiwa, nyumba zaidi ya 800 kuanguka na nyingine 1,264 zikipata nyufa mkoani Kagera, ni tukio ambalo linakuwa katika historia nchini ya majanga makubwa.

Ni janga kubwa kwa nchi yetu kwa sababu ni tetemeko kubwa kutokea nchini kulinganisha na mengine yaliyotokea bila kuacha madhara kama la Jumamosi. Janga hilo lilisababisha Rais John Magufuli afute safari ya kiserikali nchini Zambia ya kuapishwa kwa rais wa nchi hiyo, Edgar Lungu, leo mjini Lusaka.

Tetemeko hilo lililotokea saa 9:20 alasiri limeelezwa kuwa na ukubwa wa 5.9 katika vipimo vya majanga hayo kimataifa, na kwa mujibu wa mtandao wa kompyuta wa earthquaketrack.com ndilo kubwa zaidi katika historia kutokea nchini.

Takribani miaka mitatu iliyopita kuna matetemeko yaliyotokea katika maeneo kadhaa nchini, ambayo hata hivyo, hayakuwa makubwa kama la Jumamosi.

Mfano, kipimo cha 5.1 na kina cha km 10 lililikumba eneo la Msanga, Dodoma miezi miwili iliyopita. Miezi mitano iliyopita lilitokea tetemeko la kipimo cha 5.2 na kina cha km 10 eneo la Madimba, Mtwara, ambalo lilitanguliwa na lingine la ukubwa wa 4.8 na kina cha km 10 lililokumba eneo la Galappo, Manyara, miezi sita iliyopita.

Miezi 10 iliyopita lilitokea la ukubwa wa 4.3 na kina cha km 10 eneo la Kigoma pamoja na la ukubwa wa 4.8 na kina cha km 10 lililotokea Vikindu, Pwani, mwaka mmoja uliopita, kwa kutaja baadhi.

Hata hivyo, maeneo yote ambayo kumetokea tetemeko ni kwamba yako katika eneo la bonde la ufa, ambalo wataalamu wa miamba wanasema kuwa ni kawaida kutokea tetemeko.

Ukubwa wa janga hilo la asili unawafanya waathirika wastahili kupatiwa msaada wa kibinadamu na serikali pamoja na jamii nzima kutokana na baadhi kupoteza makazi, wengine nyumba zao kuhitaji ukarabati na wengine kuhitaji matibabu ili warejee katika maisha yao ya kawaida.

Ahadi iliyotolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alipokuwa mjini Bukoba juzi kufuatia tukio hilo, kuwatembelea majeruhi na kushiriki katika maombolezo kwamba serikali itahakikisha inawasaidia waathirika baada ya kukamilisha tathmini ya athari hizo, bila shaka itatekelezwa na mamlaka zote zinazohusika.

Kuna majengo takribani 44 ya taasisi mbalimbali za umma yaliyoharibika katika tukio hilo zikiwamo shule, hivyo ni wajibu wa serikali kuhakikisha kwamba wanafunzi wa shule hizo ikiwamo Shule ya Sekondari ya Nyakato wanatafutiwa mahali pa kulala huku jitihada za kukarabati majengo hayo zikifanyika ili wanafunzi waendelee na masomo kwa wakati mwafaka, ikizingatiwa kwamba wanafunzi wa kidato cha nne wataanza mtihani wa taifa siku chache zijazo.

Tukio hilo linapaswa kuwa fundisho kwa jamii nzima ya Watanzania kwamba kila mmoja anapaswa kuishi kwa tahadhari kwa kuwa sio rahisi kwa mamlaka zetu kutabiri tetemeko la ardhi litatokea lini.

Tunashauri kwamba wataalamu wa miamba wasidie kutoa elimu kwa umma mara kwa mara kuhusu namna ya kujiepusha na tetemeko ikiwamo aina ya majengo yanayopaswa kujengwa katika maeneo ambayo yana uwezekano mkubwa wa kukumbwa na tetemeko.

Habari Kubwa