Waliotekeleza viwanda, mashamba wanyang'anywe

07Feb 2016
Mhariri
Nipashe Jumapili
Waliotekeleza viwanda, mashamba wanyang'anywe

Wakati taifa linajiandaa kuingia katika uchumi utakaotegemea uzalishaji wa bidhaa za viwandani kwa kutegemea malighafi itakayozalishwa na wakulima nchini, wapo baadhi ya waliomilikishwa viwanda na mashamba wanaoendelea kuhodhi rasilimali hizo bila kuzalisha.

Tunatambua kuwa Serikali imeruhusu wawekezaji wa ndani na nje katika sekta za viwanda, kilimo, madini na maeneo mengine ambayo yanaweza kulinufaisha taifa kutokana na uzalishaji wenye tija utakaowezesha kukusanya kodi kubwa kwa maendeleo ya wananchi. Cha kushangaza zaidi ni kuwa baadhi ya waliopata fursa ya kuwekeza katika sekta hizo, wameacha kujihusisha na uzalishaji kulingana na mikataba yao waliokubaliana na Serikali na kusababisha Serikali kupoteza mapato na pia wananchi kuendelea kukosa ajira nchini. Mwishoni mwa wiki hii, Rais John Magufuli amewataka watu wote waliotelekeza mashamba pamoja na viwanda walivyouziwa na Serikali kufufua viwanda hivyo pamoja na mashamba mapema iwezekanavyo, akisisitiza kabla Serikali haijavinyang'anya na kuwagawia wanaoweza kuviendesha. Rais Magufuli alitoa maagizo hayo alipokuwa akizungumza na wananchi waliosimamisha msafara wake katika maeneo ya barabara ya Morogoro na Dodoma ambapo aliwaambia kuwa mkoa wa Morogoro ulikuwa na viwanda vingi pamoja na mashamba makubwa lakini waliopewa dhamana ya kuendesha shughuli za kilimo pamoja na viwanda waliamua kuacha kuzalisha. Kutokana na hali hiyo, Rais alisema wananchi wamekosa fursa za ajira pamoja na kutopatikana kwa uzalishaji wa bidhaa za viwandani na mazao ya kilimo, aidha Rais amebani kuwa inawezekana waliouziwa rasilimali hizo wameamua kubadilisha matumizi yake kinyume na makubaliano au wengine wameamua kuombea mikopo katika mabenki, jambo ambalo alisema Serikali yake haitakubali. Tunaamini kuwa kila aliyeomba kuwekeza, alifanya hivyo kwa madhumuni ya kutaka kuzalisha na hatimaye apate faida, tunaelewa pia kuwa tafiti zilifanyika na mwekezaji kabla ya kuamua kwa dhati kuanza uzalishaji wake, ni kutokana na hulka ya kukosa uadilifu kwa mwekezaji anayeama kuhodhi rasilimali bila kuziendeleza na kuwasababishia wengine kukosa fursa za kunufaika kiuchumi. Inawezekana baadhi ya wawekezaji waliamua kutumia mashamba waliyouziwa na Serikali kwa ajili ya kuchukulia mikopo kwenye mabenki badala ya kufanya uzalishaji, jambo ambalo ni ukiukwaji wa makubaliano, Serikali inatakiwa iangalie kwa kina na kuchukua hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kunyang'anya mashamba ya aina hiyo. Tunaamini matatizo ya wawekezaji ya kutotekeleza makubaliano ya uwekezaji kulingana na makubaliano, yapo katika maeneo mengi nchini, ni wakati muafaka sasa kwa Serikali kufuatilia kwa kila mwekezaji ili kujiridhisha na mikataba ya makubaliano ya uwekezaji wa wahusika. Kukua kwa uchumi kunategemea rasilimali zilizopo na namna zinavyotumika katika kuzalisha kwa faida ambayo ndiyo inayoweza kutafsiri hatua za maendeleo, kama rasilimali zitaachwa zikae tu bila kuzitumia na kuziendeleza, taifa linaweza kujikuta linaendelea kuwa maskini miaka yote.

Habari Kubwa