Wamachinga waendelezwe kwa kuwainua huko waliko

23Sep 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Wamachinga waendelezwe kwa kuwainua huko waliko

SERIKALI imetangaza mpango wa kuunda idara mahususi ya kushughulikia viwanda, biashara na uwekezaji kwa kila halmashauri pamoja na kuanzisha dawati litakalotatua kero za wamachinga.

Hatua hiyo ni kutekeleza maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan, ya kuwapanga upya wafanyabiashara hao na kwamba utekelezaji umeanza kwa kufufua idara ya uendelezaji miji na vijiji, ili maofisa mipango miji na vijiji watime kazi zao kiufanisi.

Hatua hiyo, inatangazwa wakati wa kuzindua mpango wa kuwapanga wamachinga kwenye vibanda 652 katika Soko Kuu la Chifu Kingalu, Manispaa ya Morogoro vilivyogharimu Shilingi milioni 81.7.

Aidha, ni maagizo ya serikali kila halmashauri itenge maeneo maalum kwa ajili ya wafanyabiashara hao, ambayo pia yataendelezwa ili kuzuia wimbi la vijana kutoka vijijini kuhamia mijini.

Tunaunga mkono utaratibu wa kuwapanga machinga kwenye miji yetu, ili kuondoa usumbufu wanaopata watumiaji wengine wa barabara na maeneo mengine ya biashara.

Wamachinga wamekuwa kero, wamejaa kwenye vituo vya mabasi, ndani ya barabara na hifadhi zake, wapo kwenye madaraja na njia za wanaotembea na wengine wamevamia baraza na viambaza vya maduka kwenye maeneo ya biashara bila kujali.

Yote hiyo ni kwavile idadi ya vijana wanaotoka vijijini kukimbilia mijini ni kubwa mno kutokana na ukosefu wa miundombinu ya kuendeleza ‘kusapoti’ biashara zao.

Ni ukweli kuwa maendeleo vijijini si makubwa, hakuna huduma za jamii kama barabara, umeme, wala miundombinu ya kufanikisha biashara zao, lakini mzunguko wa fedha ni mdogo hivyo suluhisho jepesi ni vijana kuondoka.

Serikali inathibitisha kuwa idadi ya wanaotoka vijijini kwenda mjini ni kubwa, hivyo tunaona kuwa kuna haja ya kupata suluhisho la kupunguza idadi ya wanaokimbilia mjini.

Hii itawezekana iwapo serikali itawaandalia mazingira ya kuwekeza sehemu walizopo na siyo vingine, mathalani kuona namna bora ya kuzitumia barabara kuu kutoka mikoani kwenda kwenye majiji kuweka vituo vikuu vya kibiashara.

Kila halmashauri za miji na majini kuweka maeneo maalumu ya kibiashara yanayowawezesha wakulima, wafugaji, wavuvi, wasukaji na wachongaji kuuza bidhaa zao kupitia vituo hivyo.

Iwapo vitaboreshwa na kuuza bidhaa zinazozalishwa vijijini na kwenye maeneo yao ni dhahiri wafanyabiashara kutoka miji mikubwa na majiji watasafiri kuwafuata wamachinga huko waliko na kununua bidhaa zao.

Ni wazi kuwa wamachinga wengi mijini wanauza bidhaa kutoka nje ya nchi kama mavazi (nguo, viatu, mikoba vya mitumba), wapo wanaouza vyombo, toi na kundi jingine vyakula kuanzia matunda, mboga hadi vilivyopikwa kama chips na nyama, ambavyo si endelevu.

Tunaona kuwa ni muhimu kuweka mkazo kwenye kuendeleza miji, vijiji na maeneo mbalimbali kwa kuvipelekea umeme, maji, barabara, viwanda, makazi ya kisasa, masoko, minada na vituo vya biashara ili wananchi vijana wapende kubaki kwenye maeneo yao badala ya kukimbilia mijini na majijini.

Tunashauri kuwa huo utakuwa ufumbuzi muhimu kwavile tumekuwa tukiwajengea vizimba mijini na kuwagawia, hicho kimekuwa kichocheo cha kuwavuta wenzao kuhamia kwa wingi.

Tunapendekeza walioko mijini na majijini kwenye vizimba kuwe na ufuatiliaji kujua wafanyabiashara hawa wanakua kibiashara au miaka yote wanabaki kuwa machinga kwa kuwa kuna mteremko hasa kwavile hawana wasiwasi na kodi ya pango kwasababu pango kizimba au mikono yao.

Lakini tusiishie hapo serikali ikomeshe ujanja wa kuwatumia kuuza bidhaa ili kukwepa kodi kunakofanywa na wafanyabiashara wakubwa ili mpango huo wa kuwaendeleza uwe na tija.