Wamachinga waliotafsiri vibaya agizo la Magufuli wabadilike

03Jan 2017
Mhariri
Nipashe
Wamachinga waliotafsiri vibaya agizo la Magufuli wabadilike

MKUU wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla, amewapa siku saba wafanyabiashara ndogo maarufu kama wamachinga jijini Mbeya, kuondoa biashara zao na kuingia nazo ndani ya Soko la Kimataifa la Mwanjelwa.

Makalla alifanya uamuzi huo kutokana na wamachinga hao kuwa kero na kusababisha usumbufu katika baadhi ya barabara kutokana na kuweka bidhaa hadi katikati ya barabara hizo.

Mkuu huyo wa mkoa alitoa agizo hilo kwa wamachinga akisema kwamba baadhi yao walilitafsiri vibaya agizo la Rais John Magufuli kwa wakuu wa mikoa na kufanya ovyo biashara mitaani bila kuzingatia sheria, kanuni na taratibu.

Agizo la Makalla lilitokana na wamachinga hao kuvamia barabara inayoelekea katika Kituo cha Afya cha Mwanjelwa na kusababisha usumbufu mkubwa kwa watumiaji wake.

Alisema shughuli zao zisizozingatia taratibu, mgonjwa anayetakiwa kupata huduma ya haraka katika kituo hicho au kutakiwa kutoka hapo kupelekwa haraka katika Hospitali ya Mkoa au ya Kanda ya Rufani, anaweza akapoteza maisha katika eneo hilo kutokana na kuziba barabara.

Katika kuonyesha kwamba hana utani katika hilo, Makalla aliliagiza Jeshi la Polisi kuwaondoa kwa nguvu wafanyabiashara watakaokaidi agizo lake.

Tunakubaliana na Makalla kwamba kuna baadhi ya wamachinga waliolitafsiri vibaya agizo la Rais Magufuli kwa maana wanayotaka wao, kiasi cha kupanga bidhaa zao mpaka katikati ya barabara.

Agizo alilolitoa Rais Magufuli kwa wakuu wa mikoa ni kuwataka wahakikishe wamachinga hawabughudhiwi. Hakuna alikosema kwamba waachwe wafanye shughuli zao za kujipafitia riziki mahali popote bila kufuata sheria, taratibu, kanuni na miongozo.

Ndiyo maana hata Makalla alipowaagiza kuondoka baaadhi ya maeneo, amewapa mbadala kwa kuwataka waingie ndani ya Soko la Kimataifa la Mwanjelwa ambalo lina nafasi ya kutosha ili waendelee kujipatia riziki kwa kufuata taratibu.

Pale ambapo viongozi wa serikali hususani wakuu wa mikoa wanaona wamachinga wanakiuka sheria na taratibu, wasisite kuchukua hatua kama Makalla alivyofanya, badala ya kunyamaza kimya kwa kisingizio cha agizo la rais, ambalo lilitafsiriwa vibaya na baadhi ya watu hususani wamachinga.

Tunampongeza Makalla kwa hatua hiyo, baada ya kusikiliza malalamiko ya watu akiwamo Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk. Seif Mhina, ambaye alisema msongamano wa wamachinga katika barabara hiyo ulikuwa ni changamoto kubwa kwa huduma ya afya hasa inapotokea dharura, na kwamba kuondolewa kwao kutarahisisha upatikanaji wa huduma za haraka.

Ushauri wetu kwa wakuu wengine wa mikoa ni kwamba wawasaidie wanyonge wakiwamo wamachinga kwa kuhakikisha hawabughudhiwi na ikiwezekana kuwatengea maeneo mazuri ya kufanyia shughuli zao, lakini pia wasisite kuchukua hatua mara moja pale wanapoona wanakiuka sheria.

Kwa upande wao wamachinga watambue kwamba Rais Magufuli alipotoa agizo kwa wakuu wa mikoa wahakikishe hawabughudhiwi, hakumaanisha kwamba waachwe wafanye biashara zao kiholela bila kufuata sheria, taratibu, kanuni na miongozo.

Wanapaswa kutambua kuwa biashara sio mahali popote na kwamba shughuli zao zisisababishe kero na usumbufu kwa watu wengine.

Habari Kubwa