Wanamichezo waeleza kuwa bado walimhitaji Dk. Mengi

04May 2019
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Wanamichezo waeleza kuwa bado walimhitaji Dk. Mengi

WAKATI taarifa kutoka katika familia ikisema kuwa mwili wa Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi, unatarajia kuwasili nchini Jumatatu ukitokea Umoja wa Falme za Kiarabu, bado salamu za pole zimeendelea kutolewa kutoka kwa wanamichezo mbalimbali wa hapa nchini.

Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi.

Marehemu Dk. Mengi ambaye alionekana wazi zaidi akishiriki katika kusaidia maendeleo ya mpira wa miguu nchini kupitia timu za Taifa (Taifa Stars na Serengeti Boys), pia alikuwa akisaidia michezo mingine kwa namna mbalimbali.

Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia, alisema katika taarifa yake kuwa bado nchi ilikuwa inahitaji zaidi mchango wake katika kufikia malengo ya kufanya vema katika mashindano mbalimbali.

Karia alisema kuwa mfanyabiashara huyo alikuwa ni kiongozi ambaye hataki kuona timu inataka tamaa hapa pale ilipobainika kwamba hakuna nafasi ya kufanya vizuri.

Alisema kuwa hilo peke yake lilionyesha wazi mapenzi yake kwa nchi na kila siku alikuwa ni mtu mwenye kuamini Tanzania itaweza kufanya vema na kusahau maumivu ya kuvurunda yaliyokuwa yanazizunguka timu za hapa nchini kila zilizoshiriki mashindano ya kimataifa.

Alieleza kwamba tangu alipotangazwa kuwa mlezi wa Timu ya Taifa ya Vijana wa umri chini ya miaka 17 maarufu Serengeti Boys, alitaka kujua maendeleo ya kikosi hicho na programu zake ili kuwapa chipukizi hao mazoezi ya kutoka kuelekea Fainali za Vijana za Afrika (AFCON U-17) ambazo zilimalizika hivi karibuni kwa Cameroon kutwaa ubingwa.

Licha ya Serengeti Boys ambao walikuwa wenyeji wa fainali hizo kufanya vibaya kuanzia katika mchezo wa ufunguzi dhidi ya yosso wenzao kutoka Nigeria kwa kufungwa mabao 5-4, marehemu Dk. Mengi aliwataka Watanzania kuendelea kuishangilia timu hiyo akiamini ndio kwanza safari ya mafanikio imeanza.

Kauli mbiu yake maarufu ya I can, I Must, I Will pia ilikuwa ni sehemu ya maneno ya kila siku ya wachezaji wa Serengeti Boys tangu walipokuwa wanacheza mechi za maandalizi kuelekea fainali hizo.

Alifanikiwa kuwajenga ujasiri yosso hao na hii iliwasaidia kufanya vema wakati wa maandalizi kwa kubeba makombe mbalimbali na kuonekana kuwa ni moja ya timu tishio.

Ukiondoa ushiriki wake huo katika soka la vijana, marehemu Dk. Mengi alishiriki kikamilifu kuiongoza Kamati ya Ushindi ya Taifa Stars wakati ikisaka tiketi ya kucheza Fainali za Afrika za mwaka 1994.

Chini ya uongozi wake, Taifa Stars ilifanya vema kwa kushinda mechi zake zote za nyumbani ilipocheza dhidi ya Algeria, Sudan na Uganda, lakini iliteleza kwenye michezo ya ugenini.

Pia katika kuhakikisha anapenda maendeleo, alikuwa katika mstari wa mbele kutatua mgogoro uliokuwa unawatafuna vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga ambao uliwagawa katika makundi mawili yaliyojulikana kwa jina la Yanga Asili na Yanga Kampuni.

Aliwataka wanachama wa Yanga kukubaliana na mazingira halisi akiamini kwamba mabadiliko ya mfumo ndiyo suluhisho pekee litakalowaondoa kwenye hali ya utegemezi, jambo ambalo sasa miaka 25 limepita na wanachama hao wanalidai.

Kama mzalenzo, aliwapa nafasi Watanzania wenzake mwaka 1994, kushuhudia fainali za Kombe la Mataifa Afrika kwa kuweka "screen" kubwa katika maeneo mbalimbali bila ya gharama zozote, hasa ikizingatiwa miaka hiyo idadi kubwa ya familia zilikuwa hazina televisheni.

Pia mafanyabiashara huyo aliwapa burudani nyingine wadau wa soka nchini kwa kushuhudia fainali za Kombe la Dunia mwaka huo huo kupitia kituo chake cha televisheni cha ITV bila malipo yoyote, tofauti na ambavyo sasa makampuni yanayomiliki ving'amuzi yanavyoshindana kujitangaza.

Mungu aipumzishe roho ya Dk. Mengi mahali pema peponi. Amen.

Habari Kubwa