Wananchi wajifunze kuheshimu sheria

21Dec 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Wananchi wajifunze kuheshimu sheria

PAMOJA na elimu kutolewa kwa wananchi mara kwa mara kuhusiana na kutojichukulia sheria mkononi, wananchi katika maeneo mengi nchini wanaendelea kupuuza.

Hilo linathibitishwa na matukio mengi yanayotokea nchini kuwahusisha wananchi wakijichukulia sheria mkononi badala ya kuyaripoti katika mamlaka husika, vikiwamo vyombo vya dola hususani Jeshi la Polisi.

Katika toleo la jana, tulichapisha habari ikieleza tukio la kuuawa kwa mtu mmoja na wengine saba kujeruhiwa katika mapambano makali kati ya wananchi na Jeshi la Polisi wilayani Chunya Mkoa wa Mbeya.

Kwamba katika mapambano hayo, pia kituo cha polisi kilichomwa moto, wananchi kadha na polisi kujeruhiwa.

Kwa mujibu wa habaru hizo, chanzo cha mapambano hayo ni wakazi wa Mamlaka ya Mji wa Makongolosi wilayani Chumya kugombea watuhumiwa wa mauaji.

Habari zinaeleza kuwa watu wawili walimuua mtu mmoja kwa tuhuma za ushirikina na baada ya polisi kuwakamata na kuwashikilia ndipo wananchi waliokuwa na hasira wakaenda kituoni kutaka kuwaua.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Dhahiri Kidavashari, alisema tukio hilo lilitokea juzi, baada ya kukivamia Kituo cha Polisi Makongolosi walikichoma moto na kuharibu baadhi ya mali zilizokuwapo zikiwamo pikipiki, mbao na magogo yaliyokuwa yamehifadhiwa kituoni hapo.

Tumesikitishwa na tukio hilo ambalo lina sura mbili. Ya kwanza ni watuhumiwa wa mauaji ya mtu ambaye anadaiwa kujihusisha na vitendo vya ushirikiana bila kujiridhisha kama tuhuma hizo zina chembe ya ukweli.

Hata hivyo, hata kama zingekuwa za kweli, mamlaka pekee ambazo zingepaswa kupelekewa tuhuma hizo ni vyombo vya sheria.

Ukiacha tukio hilo, yamekuwapo matukio mengi ya mauaji ya watu kwa hisia tu kwamba ni wachawi bila kuwapo ushahidi wa tuhuma hizo.

Sura ya pili ya wananchi kujichukulia sheria mkononi ni kundi kubwa la wananchi wa Makongolosi kuhamasishana kwenda kuvamia kituo cha polisi, kukichoma kisha kuharibu mali katika tukio lililosababisha kujeruhiwa kwa polisi wanne na watu wengine kadhaa.

Kwa kuwa Jeshi la Polisi lilishawakamata watuhumiwa wa mauaji ya mtuhumiwa wa ushirikina, kulikuwa na sababu gani wananchi hao kwenda kituo cha polisi kutaka kuwaua watuhumiwa hao, badala ya kuliachia jeshi hilo kuendelea na mchakato wa uchunguzi na baada ya hapo kuwapeleka mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake?

Wananchi hao walichotakiwa kukifanya ni kulipa Jeshi la Polisi ushirikiano hususani kutoa taarifa sahihi na za kina za mauaji ya mtuhumiwa wa ushirikina ili zitumike katika kufungua kesi dhidi ya watuhumiwa.

Kibaya zaidi ni kuwa wananchi hao pia walikosa busara na uvumilivu kutokana kukataa kutii sheria bila shuruti licha ya kutakiwa na polisi kuondoka kituoni.

Tukio la Makongolosi ni mwendelezo wa matukio ambayo yanaonyesha kuwa watu wengi hawajatilia maanani dhana nzima ya kuheshimu utawala wa sheria, badala yake wanaona suluhisho la kero zao ni kuchukua sheria mkononi.

Hata hivyo, athari za kujichukulia sheria mkonono ni kubwa na mbaya zaidi kwa kuwa kuna watu wanapoteza maisha, wengine wanapoteza viungo, baadhi kujikuta wanafunguliwa kesi za muda mrefu na wengine kufungwa.

Tunawashuri wananchi pia waachane na imani za ushirikina ambazo ni kichocheo kikubwa cha uvunjani wa sheria, kwani zimepitwa na wakati na hazina nafasi katika dunia ya sasa ya sayansi na teknolojia.

Habari Kubwa