Wanaoacha kutumia ARV wasilaumiwe, wasaidiwe

07Dec 2018
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Wanaoacha kutumia ARV wasilaumiwe, wasaidiwe

KUMEKUWAPO na malalamiko kwamba baadhi ya watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi (VVU) walioanza kutumia dawa za kufubaza Virusi vya Ukimwi (ARV), wanazitelekeza dawa hizo kwa sababu zisizojulikana.

Malalamiko hayo yamekuwa yakitolewa na madaktari katika maeneo mbalimbali nchini, huku wakionya kuwa kwa kufanya hivyo watu hao wanayaweka maisha yao hatarini kiafya.

Kutolewa kwa malalamiko hayo mara kwa mara kunaashiria ukubwa wa tazito katika jitihada za taifa za kukabiliana na ugonjwa wa Ukimwi. Tunasema hivyo kwa kuwa taifa linatumia muda na rasilimali nyingi katika vita dhidi ya Ukimwi.

Rasilimali hizo zimekuwa zikielekezwa katika kudhibiti maambukizi mapya ya VVU, kuwahudumia watu wanaoishi na VVU na matibabu kwa wagonjwa.

Hatuwezi kuwalaumu wanaoacha kutumia ARV bila kushauriwa na madaktari, lakini inawezekana kuna changamoto kadhaa ambazo zinasababisha wachukue uamuzi huo.

Kwa mfano, inawezekana baadhi wakaamini kuwa wamepona kabisa na wengine kukumbana na changamoto ikiwamo ya umbali wa kufuata dawa hizo.

Jambo hili halipaswi kutufanya tuwalalamikie wanaotelekeza ARV, bali tuwasaidie kwanza kwa kubaini sababu kisha kufikia ufumbuzi.

Mamlaka za afya kwa kushirikiana na viongozi wa katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu hawanabudi kufanyakazi pamoja katika kupata ufumbuzi.

Kuna baadhi ya maeneo ambayo wahusika wamelibaini tatizo hilo na kuanza kuchukua hatua za kulipatia ufumbuzi. Kwa mfano, kuna taarifa kuwa Hospitali ya Rufani mkoani Morogoro inatarajia kutoa ARV kwa kuwafuata wagonjwa kila nyumba kuanzia ngazi ya kaya.

Imeelezwa kwamba lengo la mpango huo ni kuwarahisishia wagonjwa kuzifuata dawa hizo katika vituo vya afya.

Hayo yalibainishwa na Mganga wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Frank Jacob, alipokuwa akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Ukimwi duniani yaliyofanyika kimkoa wilayani Mvomero, na kueleza kuwa hatua hiyo itawezesha wananchi wengi kujitokeza kupima afya zao kwa hiari na kutumia dawa hizo kwa wakati, hivyo kupunguza maambukizi mapya.

Alisema wameamua kuchukua hatua hiyo kutokana na baadhi ya wagonjwa walioanzishiwa dawa hizo wakati mwingine kushindwa kufika katika vituo vya afya au hospitali kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo kuogopa kunyanyapaliwa katika jamii.

Alisema ili kukabiliana na maambukizi mapya, mkoa umeamua kujipanga ili watakaopimwa na kubainika kuwa wameambukizwa VVU waanze kupelekewa dawa hizo majumbani kwao.

Hatua hii ya Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Morogoro ni nzuri na inapaswa kuwa mfano kwa hospitali zingine pamoja na vituo vya afya.

Mojawapo ya sababu alizozibainisha Dk. Jacob kwamba inawezekana baadhi ya wanaotumia dawa hizo kutokwenda katika vituo vya huduma kuzichukua ni kuogopa kunyanyapaliwa.

Sababu hiyo ina mashiko kwa sababu uzoefu wetu unaonyesha kuwa unyanyapaa kwa watu wanaoishi na VVU ni changamoto kubwa. Ni changamoto kubwa kwa kuwa miongoni mwa wanaotajwa kuwanyanyapaa ni baadhi ya watumishi wa sekta ya afya.

Tunatarajia kusikia na kuona hospitali na vituo vingine vya huduma za afya vikichukua hatua ya kumaliza changamoto hiyo zikiwa ni hatua za kuongeza kasi ya vita dhidi ya Ukimwi nchini.

Haitakuwa vibaya kama na wengine pamoja na hatua nyingine wataamua kuwapelekea nyumbani watumiaji wa ARV. Kuwashauri na kuwasaidia itakuwa silaha sahihi dhidi ya vita hivyo kuliko kuwalaumu.