Wanaomilikishwa silaha waangaliwe afya ya akili

20Jul 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Wanaomilikishwa silaha waangaliwe afya ya akili

JUNI 17, mwaka huu, eneo la Sinza, jijini Dar es Salaam, kulifanyika mauaji ya kutisha baada ya mfanyabiashara Alex Koroso (37), kumshambulia kijana mwenzake Gift Mushi, kwa risasi wakati wakiwa wanapata kinywaji.

Inadaiwa mfanyabiashara huyo alianzia baa nyingine alikokesha usiku kucha na baadaye kuhamia kwenye baa hiyo akiendelea kunywa na kutokea mabishano na wenzake.

Mabishano hayo yalisababisha mauaji hayo ambayo yamekuwa gumzo kutokana na matumizi mabaya ya silaha.

Tukio hilo limeshtua wengi na kuwa gumzo kwenye mitandao ya kijamii. Wapo wanaouliza kama wanaomilikishwa bastola wanapimwa akili na kuangaliwa mienendo yao kabla ya kupewa.

Wenye baa nao wameingia kwenye lawama kutokana na kutodhibiti watu wanaoingia na silaha wakiwa wamelewa kupita kiasi huku wakifanya vurugu kutoripotiwa polisi.

Video zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha awali, alivyokuwa anafundishwa kutumia bastola hiyo na pia Juni 13, mwaka huu, wakati wa kumbukumbu ya siku yake ya kuzaliwa moja ya keki ilikuwa na picha ya bastola yake.

Tukio hili linaamsha hisia na kuonyesha umuhimu wa kupitia upya utaratibu wa kummilikisha mtu silaha, na usalama kwenye maeneo ya starehe.

Kama marehemu Alex alianza kurusha risasi hewani wakati anapishana na wenzake huku akimwaga risasi mezani, ilikuwa ni ishara tosha ya kutoweka kwa amani, ilipaswa waliokuwapo kutoa taarifa polisi kwa siri.

Upo umuhimu wa kupitia upya mienendo ya wanaomiliki silaha, lakini uwapo utaratibu wa kupima akili za wenye silaha hizo mara kwa mara bila kusubiri matukio ya mauaji, kama inavyotokea kwenye nchi zilizoendelea duniani.

Kwa uchache, Mei 11, mwaka huu, mtu mmoja nchini Urusi, aliua wanafunzi kadhaa kwa kuwafyatulia risasi wakiwa shuleni kwenye mji wa Kazan.

Juni 20, mwaka huu, watu 12 waliuawa kwa kupigwa risasi na wengine 40 kujeruhiwa baada ya kupigwa risasi wakati wanatazama filamu mjini Denver nchini Marekani.

Mwaka 2017 waumini 26 wa Kanisa la First Baptist Church mji wa Sutherland Springs moja ya Jimbo la Texas waliuawa kwa kupigwa risasi wakiwa kanisani na kijana aliyekadiriwa kuwa na miaka 20.

Haya ni matukio ya mfano kwenye nchi zilizoendelea ambazo kumiliki silaha ni jambo la kawaida na zinauzwa maduka maalum, hata kijana wa miaka 20 anaweza kununua, na mauaji mengi nchini humo hutokana na kupigwa risasi.

Ni muhimu kujifunza kwa kuhakikisha ukaguzi unafanyika maeneo yenye mikusanyiko ya watu wengi kama uwanja wa taifa ambapo wengine hushindwa kujizuia dhidi ya utani wa mashabiki, wanaweza kufanya jambo baya (ingawa hatuombi litokee).

Kwenye maeneo mengine ya mikusanyiko ni muhimu kuimarisha ukaguzi, ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza na kuelimisha jamii umuhimu wa kutoa taarifa.

Wapo wanaomiliki silaha na kuona ni sifa kuzionyesha wakati mwingine kuvaa nguo za kubana zikionyesha silaha husika kiunoni, na wengine wanapokwenda sehemu za starehe wanazitoa na kuweka mezani au kuonyesha wengine jambo ambalo huchukuliwa rahisi, lakini ni hatari kwa usalama wa watu.

Habari Kubwa