Wanaosaka uongozi wawe watumishi wa wananchi

15Jul 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Wanaosaka uongozi wawe watumishi wa wananchi

MCHAKATO wa kusaka uongozi wa nchi yetu ngazi ya udiwani, ubunge na urais kwa kupitia uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba, sasa ni rasmi.

Ni rasmi kwa sababu baadhi ya vyama vimeanza kupata wagombea, huku vingine vikiendelea na mchakato wa kuwashindanisha kupitia kura za maoni.

Karibu kila chama hivi sasa kiko katika pilikapilika za kuhakikisha kinakamilisha mchakato wa kupata wagombea kabla ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutangaza ratiba rasmi ya uchaguzi kuhusu. Mchakato wa NEC unahusisha uchukuaji fomu, urejeshaji, mapingamizi, uteuzi, kampeni na upigaji kura.

Jambo moja kubwa tofauti na miaka iliyopita ya uchaguzi mkuu, safari hii wamejitokeza watiania wengi katika vyama vya siasa ambao wanaomba kuteuliwa kupeperusha bendera za vyama vyao.

Idadi kubwa ilishuhudiwa katika Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika baadhi ya majimbo, lakini pia jana ikiwa siku ya kwanza kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuanza uchukuaji wa fomu za uteuzi hali hiyo ilijirudia.

Kuna majimbo ambayo waliochukua fomu wameanzia zaidi ya 40 hadi kufikia 40 huku mchakato huo ukiendelea hadi Julai 17, mwaka huu.

Ingawa uchukuaji fomu haujaanza katika baadhi ya vyama, lakini kujitokeza kwa wanachama wengi kutaka ubunge ni ishara kwamba demokrasia imechipukia ndani ya vyama vya siasa.

Inawezekana kuwa kuna sababu zingine zilizohamasisha wengi kuchangamkia kugombea, ikiwamo kuamini kuwa haki itachukua nafasi kutokana na dhamira ya dhati ya serikali ya kudhibiti vitendo vya rushwa kwa kuipa ‘meno’ Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuwakamata na kuwachukulia hatua wale watakaobainika kujihusisha na rushwa.

Tunaona hivyo kwa kuwa huko nyuma kulikuwa na ugumu kwa mtu kwenda kugombea ubunge au udiwani bila kuwa na fedha nyingi kwa ajili ya kutafuta kuungwa mkono na wajumbe wanaopitisha wagombea katika vikao vya vyama na vile vile kwa wapigakura wakati wa mchakato wa uchaguzi.

Ni jambo la kufurahisha kuona wanachama wa vyama vya siasa kuchangamkia kugombea nafasi za uongozi kwa ajili ya kuwatetea na kuwaletea maendeleo wananchi. Hali hiyo inaonyesha jinsi gani kila mmoja alivyo na haki ya kikatiba ya kuchagua na kuchaguliwa.

Hata hivyo, ushauri wetu walioshajitokeza na watakaojitokeza baadaye kuomba nafasi za kuteuliwa kuwania urais, ubunge na udiwani ni kuwa na nia na dhamira ya dhati ya kuwatumikia wananchi naTanzania kwa ujumla.

Hatutarajii kuona mtu anasukumwa na maslahi binafsi kwenda kugombea nafasi anayoombea uteuzi hususan kupata fedha, maana kuna dhana iliyojengeka nchini kuwa njia rahisi ya kupata utajiri ni kuwa mbunge.

Tunawakumbusha waliojitokeza kwamba ubunge ni utumishi wa umma, hivyo nafasi hiyo inawahitaji watu wanaokerwa na matatizo ya wananchi, ambao watakwenda kuyazungumza kwenye vikao vya uamuzi vya Bunge na Mabaraza ya madiwani ili yapatiwe ufumbuzi.

Yako pia matatizo yanayoikabili Tanzania kama Taifa, hivyo yanawahitaji watu wenye nia ya dhati ya na uwezo wa kuishauri serikali kupitia Bunge kwa lengo la kuyatafutia ufumbuzi.

Wakati huu hauwahitaji watu wasio na sifa za utumishi kwenda bungeni kwa sababu tu wamewapa rushwa wananchi wakawachagua
Tunatoa rai kwa vyama vya siasa kuwa makini katika michakato yao ya uteuzi wa wagombea wao ikiwamo kutenda haki, kuteua wagombea wenye sifa zilizoainishwa pamoja na uadilifu, uaminifu, weledi na ujasiri.

Tunatarajia kuwa la jinsia litapewa kipaumbele; kwa maana kundi la wanawake pamoja na kutoa nafasi wanazostahili watu wa makundi mengine maalum ya vijana na watu wenye ulemavu.

Habari Kubwa