Wasafiri, wananchi wanahitaji vyoo visafi

25Nov 2018
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Wasafiri, wananchi wanahitaji vyoo visafi

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amepiga marufuku uchafuzi wa mazingira unaoitwa‘kuchimba dawa’ wakati wa safari ambao sasa unaelezwa kuwa mazoea kutokana na wasafiri kuacha vinyesi na haja ndogo njia nzima hasa barabara kuu yanakopita mabasi ya abiria.

Ni agizo tunalounga mkono ili kuhakikisha kuwa mazoea ya uchafu yanadhibitiwa na watu kuondokana na taratibu za kizamani za kujisaidia maporini au pembeni ya barabara na kusambaza magonjwa kwa wakazi wa maeneo jirani na mifugo inayokula nyasi pembeni ya barabara.

Tunaunga mkono makatazo haya kwa kuwa ni kosa kujisaidia njiani wakati vyoo vipo kama alivyofanya Waziri Mkuu kwa kuagiza mamlaka za Wizara ya za Afya, Mambo ya Ndani, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra) na Chama cha Wamiliki wa Mabasi (Taboa), kuandaa mikakati ya kuondokana na mienendo hiyo mibovu inayotishia afya za wananchi.

Pamoja na kuunga mkono hatua hiyo, tunaona kwamba mamlaka za halmashauri zinatakiwa kuwajibika kutimiza wajibu zisingojee maagizo kutoka juu.

Tunaona hivi kwa sababu baadhi ya sehemu ambazo zilihitaji kuwa na vyoo havipo hasa kwenye barabara kuu na hata kwenye masoko. Halmashauri zisingojee Waziri Mkuu atoe maagizo, zihakikishe kuwa kunakuwa na vyoo vya umma kwenye vituo vya mafuta na majengo yote yanayojengwa pembeni ya barabara.

Ni vyema pia kusisitiza kuwapo na vyoo safi na vyenye maji na huduma muhimu kama sabuni na karatasi za chooni hata kwenye barabara ndani ya miji. Hii haimaanishi kuwa ni lazima kuwe na jengo linaloelekeza kuwa ‘kuna choo cha kulipia’.

Halmashauri zinaweza pia kuweka utaratibu kwa kushirikiana na watu binafsi kuweka vyoo vya umma kwenye gereji rasmi zilizo pembeni ya barabara, hoteli na migahawa ambavyo vitahudumiwa na wahudumu wanaosafisha na kutunza huduma hiyo kwa muda wote.

Tunasema hivi kwa sababu kuwapo kwa vyoo ni jambo jema lakini kuwa na vyoo vichafu kupindukia visivyofaa kutumiwa na binadamu ni kero kubwa kwa kila mtu anayeshikwa na haja. Kwa hiyo haitoshi kuwa na choo kwenye kituo cha mafuta lakini jambo la muhimu ni je choo hicho kinaingilika?

Tunaona kuwa ni muhimu pia kuwa na vyoo kwa ajili ya watoto kwani vilivyopo ni vigumu kutumiwa na watoto hasa wadogo wanapokuwa safarini.

Lakini wakati kampeni hii ya kutokomeza mazoea ya kuchimba dawa inapopamba moto , tunajiuliza hivi haiwezekani kukawa na kiwango cha choo kwa ajili ya wasafiri ? Vingi ni vichafu, havisukumi wala kuvuta maji , tena kuna vingine havina mabomba wala maji ya kunawa baada ya kutumia choo yote haya ni kero kwa wasafiri.

Tunaziomba halmashauri na Taboa zisisubiri Waziri Mkuu aziagize kukagua vyoo zifanyekazi na kujituma kulinda afya za wasafiri. Kama ambavyo mabasi yanalazimishwa kuingia vituoni kila wilaya ili kulipa tozo kadhalika na huduma ziwepo ili kuwa na uwiano wa sawa kwa sawa. Siyo kukusanya fedha lakini hakuna huduma kwa wananchi.

Shime Taboa, kama wanachama wenu wanavyoshindana kujenga migawaha na kuuza vyakula ghali kwa kasi hiyo changamkeni kujenga vyoo bora na visafi kwa ajili ya wateja wenu.

Habari Kubwa