Wasimamizi uchaguzi wazingatie maelekezo yanayotolewa na NEC

05Aug 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Wasimamizi uchaguzi wazingatie maelekezo yanayotolewa na NEC

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeendelea kutoa maelekezo kwa wasimamizi wa Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28, mwaka huu.

Katika maelekezo hayo yanayotolewa na viongozi waandamizi wa NEC, wakiwamo makamishna, yanajielekeza kuwakumbusha wasimamizi wa uchaguzi kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao kwa kutenda haki kwa wadau wote wa uchaguzi, lengo likiwa kuufanya uchaguzi huo uwe huru na haki.

Wasimamizi hao kadhalika, wanasisitizwa kutenda haki kwa kuwa wao ndio marefa wanaochezesha mchezo, ambao kwa namna yoyote ndio wahusika wakuu katika kuufanya uchaguzi uwe huru na haki au kinyume chake.

Pale ambapo msimamizi anashindwa kutenda haki kwa makusudi au kwa kushindwa kutafsiri na kufuata sheria, taratibu, kanuni, miongozi na maelekezo ya NEC, matokeo yake ni kuibuka kwa malalamiko kutoka kwa wagombea, vyama vya siasa, wafuasi na wadau wote wa uchaguzi.

Uchaguzi unaotawaliwa na malalamiko dhidi ya wasimamizi hauleti afya njema kwa kuwa katika hali ya kawaida, ndicho kichocheo kikuu cha vurugu na upotevu wa amani katika nchi.

Katika uchaguzi mbalimbali ambao umekuwa ukifanyika nchini, kuna malalamiko yanayotolewa dhidi ya wasimamizi wa uchaguzi, ambayo kwa kiasi fulani yana ukweli.

Hata hivyo, yanayolalamikiwa ni makosa yanayofanywa na wasimamizi binafsi, hivyo kuharibu jina la NEC, ambacho ndicho chombo kilichowekwa kikatiba na kupewa dhamana ya kuratibu na kusimamia shughuli za uchaguzi nchini.

Wakati huu ambao NEC inaendelea na mchakato wa maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao, ikiwamo kuwapa semina za mafunzo wasimamizi, tunadhamini kuwa ndio wakati mwafaka kwa tume kuhakikisha kwamba inawafunda ipasavyo wasimamizi hao na wasaidizi wao.

Ikumbukwe kuwa NEC kuwaacha wasimamizi waendelee kufanya makosa yale yale yanayolalamikiwa mara zote na wadau wa uchaguzi, maana yake ni kuwakosesha wadau hao na umma kwa ujumla imani kwa chombo hicho.

Katika semina hizo zinazoendelea, tumewasikia viongozi wa NEC wametahadharisha kuhusu mambo kadhaa. Kwa mfano, tumesikia wasimamizi wa mikoa ya Simiyu na Shinyanga wakiagizwa na mmoja wa maofisa wa tume kuhakikisha simu zao zinakuwa wazi kwa kipindi chote cha uchaguzi hadi utakapomalizika.

Alisema lengo ni kuhakikisha wanakuwa tayari kila wakati kupata maelekezo yanayohusu masuala ya uchaguzi na upokeaji wa vifaa vya uchaguzi vitakapoanza kugawiwa katika maeneo mbalimbali wanayosimamia.

Mbali na kuwataka wasimamizi simu zao kuwa wazi kila wakati, sisi tunaona kuwa NEC inapaswa kuwasisitiza kasoro zilizotokea na kulalamikiwa sana wakati wa uchaguzi mdogo wa marudio wa kata 24 mwaka juzi na uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka jana, wawe makini zisijirudie.

Uchaguzi wa marudio wa kata 24 ulitawaliwa na malalamiko ya vyama vya siasa kwamba wasimamizi walikuwa wanazima simu, hivyo kusababisha wagombea wa upinzani kukosa ushirikiano na matokeo wengi kushindwa kurejesha fomu zao siku ya mwisho kutokana na kukuta ofisi zimefungwa.

Katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka jana, malalamiko mengi yalihusu wasimamizi kuwaengua wagombea wa vyama vya upinzani kwa madai kuwa walishindwa kuzijaza fomu za uteuzi kama inavyotakiwa. Tunashauri kwamba safari hii NEC iwape wasimamizi maelekezo ya namna ya kushughulikia kasoro kama hizo zinapojitokeza.

Utaratibu mzuri na ambao utasaidia kutatua kasoro hizo na kuondoa malalamiko mbalimbali, ni wasimamizi kukaa ofisini wakati wote na pale mgombea anaporejesha fomu ikiwa na kasoro, asaidiwe kuzirekebisha ili fomu yake ipokelewe.

Habari Kubwa