Wataalamu watasaidia kubaini dosari za vitabu

18May 2017
Mhariri
Nipashe
Wataalamu watasaidia kubaini dosari za vitabu

BAADA ya wabunge kuchachamaa kuhusu makosa waliyoyabaini kwenye vitabu vya kujifunzia na kushauri kuzuia matumizi yake ili kuepuka kuendelea kuwaharibu wanafunzi, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako, ameanza kuchukua hatua kadhaa.

Hatua ya kwanza ni kuwasimamisha kazi Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE), Dk. Elia Kidga na Kaimu Kamishna wa Elimu, Nicolaus Buretta ambao ndio wenye dhamana ya kusimamia ubora wa vitabu.

Hatua hiyo iliyochukuliwa Jumatatu ilitokana na malalamiko ya wabunge waliochangia mjadala wa hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka ujao wa fedha 2017/18 iliyowasilishwa Jumamosi iliyopita na Prof. Ndalichako.

Walisema vitabu hivyo vilivyosambazwa na serikali katika shule za msingi na sekondari vilivyogharimu Sh. bilioni 108 vina makosa mengi ya lugha ya Kiswahili na Kingereza, jambo ambalo linaua elimu nchini.

Makosa yaliyobainika katika vitabu hivyo ni ya kisarufi, mpangilio wa kurasa, tafsiri sisisi na kimantiki.

Akisoma maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Suzan Lyimo, alisema pia makosa hayo yamekithiri katika herufi kubwa na ndogo pamoja na matumizi ya nukta pacha. Pia matatizo hayo yamo kwenye vitabu vyote hasa vya kujifunza kusoma, kuandika, kuhesabu, afya na mazingira, michezo na sanaa.

Kilichotokea ni aibu na kuwasimamisha kazi vigogo hao hakutoshi, bali zinahitajika hatua zaidi kwa kuzingatia kuwa fedha za walipakodi zilizotumika ni nyingi na ni hasara kwa taifa, kwa kuwa zingeweza kutumia kugharimia miradi mingine ya maendeleo.

Tunakubaliana na pendekezo la wabunge la kumtaka Prof. Ndalichako kuunda kamati maalum ya kuchunguza vitabu hivyo kuzibaini dosari hizo.

Zipo hatua nyingine ambazo tunaona zinafaa kuchukuliwa ili kuepusha mambo kama hayo kutokea katika siku za mbeleni.

Miongoni kwa hatua hizo ni serikali kufanya uhakiki wa taaluma na weledi wa watumishi wa TIA ili kujiridhisha kama wana sifa stahiki, uwezo na weledi katika kufanya kazi ya utunzi wa vitabu. Tunapendekeza hilo kwa kuwa elimu ya msingi ni msingi wa kila kitu na kutolewa kwa vitabu vyenye makosa ni aibu wakati kuna wataalamu walioajiriwa na ambao wanashinda wakivipitia.

Kutokana na hali hiyo, ndio maana tunaona kuna umuhimu mkubwa wa kuundwa kwa kamati maalum ya wataalamu kupitia dosari hiyo na kuchunguza kwa nini wametoa vitabu vyenye makosa.

Tunampongeza Prof. Ndalichako, kwa kuonyesha utayari wa kuunda kamati hiyo, baada ya kuainisha hadidu tano za rejea zitakazoongoza uchunguzi wa kiini cha kuwapo kwa dosari zilizobainika katika vitabu hivyo.

Akizungumza na gazeti hili juzi mjini Dodoma, kuhusu utekelezaji wa azimio hilo la Bunge, Prof. Ndalichako alisema muda wowote ataunda kamati ya wataalamu ya kuchunguza suala hilo.

Alisema juzi alitarajia kukutana na Katibu Mkuu (Wizara ya Elimu) ili washauriane kuhusu wataalamu watakaokuwamo katika kamati hiyo.

Kwamba wataalamu watachunguza mchakato wa kuwapata waandaaji wa vitabu na kujiridhisha kama kweli wana sifa za kuandaa vitabu.

Prof. Ndalichako pia alisema wataalamu hao watachunguza wataalamu walioitiwa na TIE kupitia vitabu hivyo na mchakato uliofanywa mpaka vikapewa ithibati ya kutumika kwenye shule.

Ni matumaini yetu kwamba hadidu za rejea za Prof. Ndalichako zitasaidia sana kupatikana kwa majibu sahihi kuhusiana na kilichosababisha kuandaliwa kutolewa kwa vitabu vyenye dosari nyingi, ambayo yatasaidia kuchukuliwa hatua stahili.