Watanzania tuchangamkie fursa eneo huru la biashara

30Jun 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Watanzania tuchangamkie fursa eneo huru la biashara

JUZI Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Leberata Mulamula, alisema serikali imekamilisha mambo yote ya msingi yanayotakiwa kuwa kwenye mkataba wa biashara kwa nchi za Afrika na sasa serikali itaridhia.

Nchi nyingi za Afrika zimesharidhia mkataba huo mwaka 2018 na utekelezaji ulianza mwaka 2019, lakini Tanzania ilibaki nyuma kwa mwaka mmoja.

Waziri alikutana na Katibu Mtendaji wa Eneo huru la Biashara la Afrika (AfCFTA), Wamkele Mene, na kumhakikishia kuwa Tanzania imeshakamilisha kila kinachotakiwa na iko tayari kuridhia na kusaini mkataba huo kwa manufaa ya watu wake.

Hii ni habari njema kwa kila Mtanzania kwa kuwa faida ya kuridhia mkataba huo ni uhakika wa soko kubwa la zaidi ya watu bilioni moja kwa kuuza na kununua bidhaa bila vikwazo, na sasa ni wakati wa Watanzania kwa nyakati na nafasi tofauti kuchangamkia fursa zote muhimu.

Huu siyo mkataba wa kwanza kwa Tanzania kuridhia katika eneo la biashara, ipo mingi ikiwamo mkataba wa mpango wa soko la AGOA (African Growth and Opportunity Act).

Katika bajeti ya mwaka huu, serikali ilieleza kuwa nchi imeendelea kunufaika na Mpango wa AGOA kwa kuruhusiwa kupeleka zaidi ya bidhaa 6,400 bila kulipa ushuru wa forodha.

Aidha, katika kutekeleza mkakati wa kitaifa wa AGOA, Wizara ya Viwanda na Biashara imeendelea kuhamasisha wafanyabiashara wa Tanzania kuwekeza, kutumia ipasavyo fursa za soko hilo ili kukuza mauzo ya bidhaa zetu, kuongeza fedha za kigeni, kuchochea ukuaji wa viwanda pamoja na kukuza ajira nchini.

Sasa imekuja fursa ya eneo huru la biashara, ni wakati wa Watanzania kuuza mazao na bidhaa mbalimbali zinazozalishwa nchini na kuwa na utambulisho wa nchi yetu.

Ni muhimu katika hili changamoto zote zikatatuliwa na kubwa ni vifungashio ambavyo hutumika vya nje ya nchi, jambo ambalo linaitambulisha nchi husika ilhali bidhaa zinazalishwa Tanzania.

Mathalani, wakati wa Bunge la Bajeti, wabunge kutoka maeneo yanayolima maparachichi ya kisasa walisema kuna nchi jirani inauza vifungashio na wakati mwingine wanachukua bidhaa nchini na kwenda kuzipakia kwenye vifungashio hivyo na kusafisha katika masoko ya Ulaya, Marekani na Uarabuni na kuonyesha bidhaa hiyo imetoka nchi hiyo.

Hili si jambo dogo ni salamu kuwa sasa nchi iwe na mpango wa kuzalisha vifungashio vyake vya kuitambulisha kokote kulingana na bidhaa husika ili kuendelea kutambulisha bidhaa zetu zenye ubora.

Lakini wakati hilo likifanyiwa kazi, ni wajibu wa Wizara ya Kilimo kuhakikisha wanatoa elimu kwa wakulima kuzalisha kwa ubora na huduma zote muhimu za ugani.

Katika soko la ushindani kinachokubeba ni bidhaa bora na siyo jina la nchi yako, kama utaweza kuzalisha bidhaa na mazao bora maana yake utajitangaza duniani.

Tunaona ni muhimu sana kwa Wizara za Viwanda kushirikiana kwa karibu katika kuhakikisha bidhaa na mazao yanayolepekwa nje ziwe na ubora unaotakiwa, na hili litafanikiwa ikiwa huduma za ugani zitatolewa kikamilifu ikiwamo kuwezesha wajasiriamali kuzifikia fursa hizo.

Pamoja na jihitaha za serikali pia ni wajibu wa sekta binafsi kupitia Jumuiya ya Wafanyabiashara na wajasiriamali nchini kuchangamkia kikamilifu fursa hiyo na sasa bidhaa za Tanzania ziendelee kuuzwa nchi za Afrika, na kuliwezesha taifa kupata fedha za kigeni na ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Habari Kubwa